SAA 51 tangu kutekwa kwa Kituo cha Biashara cha Westgate, zimeshuhudia jana milio mizito ya risasi na mabomu kutoka ndani ya jengo hilo. Mapambano kati ya askari wa vikosi vya ulinzi na usalama vya Kenya, yalipamba moto jana mchana na kusababisha moshi mzito kutoka ndani ya jengo hilo.
Tukio hilo lilitokea baada ya askari wa kikosi maalumu cha Kenya, wakisaidiwa na maofisa usalama kutoka nchi za Israel, Marekani na Uingereza, kuanza kazi ya kuwafikia wanamgambo wa Kiislamu wa Al-Shabaab. Waziri wa Mambo ya Ndani, Joseph Ole Lenku, alisema katika mapambano hayo, magaidi wawili waliuawa na mateka kadhaa waliokolewa.
“Wanamgambo wote ni wanaume, japokuwa baadhi walivalia kama wanawake.
“Tunadhani operesheni itafikia mwisho muda si mrefu,” alisema. “Tunadhibiti sakafu zote, magaidi wanakimbia na kujificha katika baadhi ya maduka. Hakuna sehemu ya kutorokea,” alisema Waziri Lenku.
Alisema kuna hofu idadi ya vifo huenda ikaongezeka, wakati askari wakiendelea kutafuta watu walionusurika na miili katika maeneo mbalimbali ya maduka.
Alisema karibu mateka wote wameokolewa kutoka jengo hilo, saa chache bada ya kukumbwa na mlolongo wa mashambulizi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi, David Kimaiyo, alisema katika ujumbe wake wa Twitter kuwa katika siku ya tatu ya shambulio hilo, waliwaokoa mateka baada ya kuingia jengoni huku wakizidi kupata mafanikio dhidi ya washambuliaji.
Alisema jana mchana, kuna watu kadhaa waliokamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Nairobi, wakijaribu kutoroka.
MSEMAJI AONYA
Wakati askari wa Kenya na magari zaidi ya maofisa usalama yakielekea katika jengo hilo, msemaji wa kundi hilo la al Shabaab, Ali Mohamud Rage, alitoa onyo.
Alisema katika taarifa aliyoiweka kwenye tovuti ya kundi hilo kuwa wale wanaoshikiliwa wataonja maumivu ya nguvu zitakazochukuliwa na jeshi la Kenya dhidi ya wanamgambo.
Taarifa ilisema: “Tumewaagiza mujahedeen ndani ya jengo wachukue hatua kali dhidi ya wafungwa wao wakati watakapohisi kubanwa.
“Tunawaambia Wakristo wanaoelekea walipo mujahedeen wawaonee huruma wafungwa wao ambao wataonja makali ya nguvu yoyote itakayoelekezwa kwa mujahedeen.”
TAKWIMU
Wanamgambo hao, walivamia eneo hilo la maduka na kulizingira na kufanya mauaji, ambapo hadi tunakwenda mitamboni jana, idadi ya watu waliouawa iliripotiwa kuwa 69 na wengine 63 hawajulikani waliko, huku wengine takribani 180 wakijeruhiwa.
Takwimu hizo, ni kwa mujibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, wakati Serikali ya Kenya ikisisitiza watu aliouawa ni 62 tu.
Wanamgambo hao, wanaokadiriwa kuwa kati ya 10 na 15, wamejichimbia katika chumba kimoja cha jengo hilo kisichopenya risasi wakiwa na mateka ambao wametishia kuwaua.
Huku hali ya mshikemshike ikiendelea kushuhudiwa, ufyatulianaji risasi ulisikika ndani ya jengo hilo lenye maduka na migahawa zaidi ya 80 katika eneo la matajiri la Westlands.
Milio hiyo ilidumu kwa dakika tatu na kufuatiwa na moshi mkubwa juu ya jengo hilo.
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana badaye kuhusu moshi huo zilikanganya.
Walioshuhudia walieleza kusikia milipuko mikubwa minne, ikifuatiwa na moshi mzito na sauti za risasi, wakati jeshi lilipojaribu kwa nguvu kuingia ndani walipo magaidi hao kupitia paa la jengo hilo.
Ilihofiwa baadhi ya wanamgambo, ambao wanatoka kwenye kundi lenye uhusiano na Al Qaeda, huenda walijaribu kujilipua.
Lakini, ofisa mwandamizi wa serikali ya Kenya alisema wnamgambo waliyateketeza kwa moto baadhi ya magodoro katika jengo hilo na kurusha risasi ili kuwaghilibu akili.
Al-Qaeda yatambia
Kuna utata kuhusu utambulisho wa magaidi waliojichimbia katika kituo cha biashara cha Westgate.
Kundi la Al Shabaab limedai katika mtandao wa Twitter usiku uliopita, wanamgambo hao wanaopambana na askari wa Kenya wanaongozwa na mama wa watoto watatu, Samantha Lewthwaite.
Kundi hilo, lilimsifu raia huyo wa Uingereza kuwa mwanamke shupavu ambaye wanaona fahari kuwa naye.
Mwanamke huyo, ni mjane wa marehemu, Jermaine Lindsay, mmoja wa watu waliojitoa mhanga wakati wa tukio la kigaidi la Julai 7, 2005, nchini Uingereza.
Akijulikana zaidi kama Mzungu Mjane, au Dada Mzungu, amekuwa akisakwa na polisi wa Kenya akihusishwa na genge la magaidi lililopanga mashambulizi ya mabomu nchini humo.
Kuhusishwa kwa Lewthwaite na shambulio la Westgate kulifuatia madai ya askari na baadhi ya mashahidi kumuona au kumsikia mwanamke wa kizungu aliyevalia baibui akiamrisha wenzake kwa Kiarabu.
Akaunti ya Twitter, inayodai kuwakilisha Al- Shabaab ilijigamba kuwa wana mseto mzuri wa utaifa wa wapiganaji wao. Walidai kuwa hawatoki Somalia tu, bali mataifa saba, yakiwamo Marekani Uingereza na Canada.
Akaunti yao ya Twitter, HSM Press Office ambayo ilisimamishwa mara mbili, iliwataja wanamgambo hao kuwa ni pamoja na Ahmed Nasir Shirdoon, 24, kutoka London, Uingereza, Jenerali Mustafe Noorduiin, 27, kutoka Kansas City, Marekani.
Wengine ni Abdifatah Osman Keenadiid, 24, kutoka Minneapolis, Marekani na Ahmed Mohamad Isse, 22, kutoka Saint Paul, Marekani; Ismael Guled, 23, kutoka Helsinki, Finland; Abdirizak Mouled, 24, kutoka Ontario, Canada; na Zaki Jama Caraale, 20, na Sayid Nuh, 25, wote kutoka Somalia.
Aidha ofisa mmoja mwandamizi wa Jeshi la Kenya alisema kuwa washambuliaji hao wanatoka mataifa mbalimbali duniani.
Tunataka Wakenya, Wamarekani
Mwanamke mmoja wa Ufaransa, alisema aliachiwa na magaidi hao kwa sababu walimweleza lengo lao ni kuwaua Wakenya na Wamarekani.
Mwanamke huyo, Paulina, alisema aliachiwa yeye na watoto wawili ambao waliwapatia chocolate za Mars.
Alisema aliombwa msamaha na magaidi hao kwa kitendo chao, wakimwambia kuwa hawakuwa wanyama.
Mama huyo wa watoto wawili, ambaye alikuwa katika jengo hilo wakati shambulio lilipoanza, alisema aliwakubalia wanamgambo hao kuwa Waislamu si watu wabaya, kisha wakawapatia watoto wake, Emily, (6) na Eliot (4) chocolate.
“Waliniambia: ‘Tunataka kuwaua Wakenya na Wamarekani’. Kisha akaniambia ninapaswa kubadili dini yangu kuwa Mwislamu na nikajibu niko tayari na kisha wakasema ‘je, unatusamehe, je, unatusamehe?'”
MPWA RAIS AUAWA
Wakenya zaidi ya 50 wameuawa katika shambulio hilo, akiwamo Mpwa wa Rais Uhuru Kenyatta sambamba na mchumba wa mpwa huyo.
Raia wa kigeni waliouawa nchini Kenya ni kama ifuatavyo
GHANA
Balozi wa zamani wa Ghana nchini Brazil na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa,Kofi Awoonor ameuawa. Waziri wa Habari wa Ghana,Said Awaonor amedhibitisha.
CANADA
Rais wawili wa Canada, wamekufa katika tukio hilo.Waziri Mkuu wan chi hiyo,Stephen Harper alidhibitisha.
INDIA
Raia wawili wa India,Parmashu Jain (8) na Sridhar Natarajan (40), wamekufa na wengine wanne wamejeruhiwa vibaya.
Uingereza
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza, imedhibitisha kuwa raia wake wanne wameuawa.
Ufaransa
Rais wa Ufaransa, Francois Hollande amedhibitisha raia wake wawili wameuawa.
Afrika Kusini
Rais mmoja wa Afrika Kusini, wameuawa hii ni mujibu wa idara ya uhusiano wa kimataifa.
Uholanzi
Raia wa Uholanzi,Elif Yavuz (33).Waziri wa Mambo ya Nje, Frans Timmermans alidhibitisha.
CHINA
Raia mmoja wa China, Zhou (38) aliuawa.Shirika la Habari la Xinhua limeripoti.
PERU
Mfanyakazi mstaafu Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, raia wa Peru aliuawa.
MAREKANI
Raia watano wa Marekani, walijeruhiwa vibaya. Serikali ya nchi hiyo imedhibitisha.
NEW ZEALAND
Rais wa New Zealand, Andrew McLaren (34) aliuawa. Waziri wa Mambo ya Nje wan chi hiyo alidhibitisha.
chanzo:- Mtanzania.
No comments:
Post a Comment