Social Icons

Friday, 18 October 2013

HADITHI: NGUO MPYA ZA MFALME.

Kwanza kabisa napenda kushukuru sana serikali yetu tukufu kwa kuninyima nafasi ya kuandika. Vidole vyangu vimepumzika vizuri na nilipata nafasi ya kusoma pia kidogo. Tena niliamua kusoma hadithi ya zamani sana.

Nadhani na wengi wenu mmesoma pia lakini safari hii kwa kuwa sikuweza kuandika, nikabaki natafakari zaidi.

Hadithi yenyewe ni Nguo Mpya za Mfalme. Yaani ile hadithi ya mfalme mwenye kiburi cha kaburi, aliyejiona hadi akashindwa kuona wengine. Sasa watu kama hao wanadanganyika kirahisi maana inatosha kumsifia tu kupita kiasi, ataamini chochote kile. Ndiyo maana wale matapeli wa kimataifa waliweza kumdanganya kwamba wamemtengenezea suti nzuri kiasi kwamba ni wale wenye akili tu wanaweza kuiona.

Sasa kwa kuwa mfalme alijiona mwenye akili kupita kiasi, angekubali kweli kwamba haoni? Akajiangalia kwenye kioo na kujiona alivyo bila nguo lakini wala hakutafakari kwamba iwapo wasio na akili hawaoni suti, wataona nini?

Akakubaliana na sifa za matapeli moja kwa moja na kuwapatia pesa zao taslimu badala ya kuwapatia karatasi na kusema kwamba ni wenye akili tu wataona zile karatasi ni manoti ya fedha. Matapeli walijiondokea harakaharaka, kabla hawajaanza kucheka maana ….

Baada ya hapo, mfalme, bila kujiuliza tena ataonekeanaje na wasio na akili akajipeleka mitaani kutamba na suti yake. Alitanguliwa na matarumbeta na ngoma kibao kuwaita watu kuja kuona suti ya kipekee, akasindikizwa na mawaziri wake na wengine wengi ambao wote walikuwa wanaimba wimbo wa kusifia jinsi mfalme alivyovaa na kwamba nguo yake ni sifa kubwa kwa nchi yao, inaonyesha jinsi nchi ilikuwa imeendelea.

Sasa hebu fikiria wewe ungekuwa mmoja wa watazamaji, ungejisikiaje? Ungefumba macho ili usione mambo ya siri ya mfalme? Lakini hata kama usingeona wewe, wengine wote wanaona. Au ungewashawishi wengine wafumbe macho pia. Lakini hata kama wote wangefumba macho, hali ya mfalme ingebadilika?

Mmh! Ungejiunga na waliokuwa wanamsifia usionekane mtu asiye na akili wala uzalendo? Hapa roho isingekusuta? Kwa kweli wananchi walipata tabu sana lakini mwisho wa siku badala ya kutazamana na kukubaliana kusema kwa sauti moja.

‘Mfalme hana nguo!’

Watu waliamua kusifia tu. Wakashindana kushangilia kwa vigelegele na viherehere. Kweli uoga ni ugonjwa mbaya sana. Unaona kabisa siri ya wazi hadi wachefuka, lakini bado kunyamaza tu.

Hadi mtoto akapasua anga ya uoga na unafiki

‘Jamani mbona mfalme yuko uchi?’

Chanzo:- Mwananchi

No comments:

 
 
Blogger Templates