BAADA ya mkutano wa Jumanne wiki hii, baina ya Rais Jakaya Kikwete na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani nchini, Bunge sasa litapewa fursa ya kujadili vipengele vinavyohitaji kufanyiwa marekebisho kwenye Muswada wa Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba, Raia Mwema limeambiwa.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Rais Kikwete kwanza atausaini muswada huo na kisha utarejeshwa kufanyiwa mabadiliko kwa kuzingatia baadhi ya hoja za wapinzani ambao ni pamoja na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, Freeman Mbowe wa CHADEMA na James Mbatia wa NCCR-Mageuzi. Mbali na wapinzani hao, maoni ya wadau wengine pia yatazingatiwa katika mapendekezo ya mabadiliko yatakayowasilishwa bungeni.
Uamuzi uliofikiwa katika mkutano wa Jumanne kati ya akina Lipumba na Rais Kikwete, katika Ikulu ya Dar es Salaam unamaliza mvutano wa zaidi ya mwezi mmoja baina ya serikali na vyama vya upinzani kuhusu muswada huo.
Hali hiyo ya mvutano ilifikia kilele chake wakati wa mkutano uliopita wa Bunge ambapo baadhi ya wabunge wa kambi ya upinzani walisusia mjadala wa muswada huo kwa kutoka ndani ya ukumbi wa Bunge, huku vurugu zikijitokeza kwa mara ya kwanza katika Bunge la Tanzania.
Pamoja na mambo mengine, wapinzani walilalamikia kuchomekwa kwa mambo ambayo hayakuwa yamejadiliwa kwenye vikao vya Kamati za Bunge, kutoshirikishwa kwa maoni kutoka Zanzibar kwenye uandaaji wa muswada huo na utimilifu wa kazi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Vyanzo vya gazeti hili, hata hivyo, vinaeleza kwamba mazungumzo baina ya Kikwete na viongozi hao wa upinzani yalikwenda vizuri na yalitawaliwa na nguvu za hoja kuliko hoja za nguvu.
“Unajua sisi tulisema mapema kwamba hatuendi Ikulu kunywa chai au soda na ndiyo maana tuliondoka makwetu tukiwa tumeshiba kabisa.
“Tulikwenda kuzungumza na Rais kwa sababu tunataka Katiba ambayo itawafaa Watanzania wa sasa na wa kizazi kijacho. Tanzania si CCM, CUF au CHADEMA…. Ni ya hadi wale wasio na vyama na ndiyo maana tulikubali kuonana na viongozi wa serikali,” alisema mmoja wa viongozi wa upinzani waliozungumza na gazeti hili kabla ya kuanza kwa mkutano huo.
Tofauti na picha zilizotolewa na Ikulu wakati wa mkutano wa kwanza baina ya Kikwete na viongozi wa upinzani mwaka jana, picha zilizotolewa jana, Jumanne, ziliashiria kufanyika kwa mkutano wa pamoja na viongozi wote, wakiwamo wa CCM, chini ya uwakilishi wa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula.
Katika hotuba yake ya Septamba, mwaka huu, Rais Kikwete aliahidi kukutana na viongozi wa upinzani ili kujadiliana kuhusu mchakato wa kupata Katiba Mpya.
Mkutano huo wa jana, Jumanne, ulikuwa wa pili kwa Kikwete kukutana na wapinzani kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, hasa baada ya kutokea mivutano ndani ya Bunge.
Katika mkutano wao huo, waliohudhuriwa ni pamoja na mawaziri watatu wa serikali ya Kikwete; Stephen Wassira (Ofisi ya Rais- Uhusiano), Mathias Chikawe (Sheria na Katiba) na William Lukuvi (Ofisi ya Waziri Mkuu-Bunge na Uratibu) – ambao vyama vya wapinzani vilikuwa vinataka wajiuzulu kutokana na msimamo wao mkali kuhusu mabadiliko ya Katiba.
Viongozi waliohudhuria mkutano wa jana na majina ya vyama vyao kwenye mabano ni Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Freeman Mbowe (CHADEMA), Isaac Cheyo (UDP), Habib Mnyaa (CUF), Tundu Lissu (CHADEMA), Julius Mtatiro (CUF) na Nancy Mrikaria (TLP).
Chanzo:- Raia Mwema
No comments:
Post a Comment