Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro amewahakikishia wafanyabiashara mkoani humo kuwa malalamiko yao kuhusu mashine za kutolea risiti za ‘kieletroniki’ yametua kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kwamba majibu yatapatikana kabla ya Oktoba 15 mwaka huu.
Kandoro alitoa kauli hiyo juzi jioni alipokuwa akizungumza katika kikao cha dharura cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na viongozi wa wafanyabiashara hao waliogoma kufungua maduka yao kwa siku mbili wakipinga kile wanachodai kuwa ni bei kubwa ya kununulia mashine za kieletroniki.
Serikali inataka kila mfanyabiashara wa duka kununua na kutumia mashine hiyo, kama njia ya kuhakikisha kuwa analipa kodi halisi ya biashara yake.
Hata hivyo, kwa upande wao, wafanyabiashara wa Mbeya wanadai kubwa bei za mashine hizo ni kubwa kuliko uwezo wao.
Hata hivyo, jana wafanyabiashara hao walifungua maduka na kuendelea na biashara zao.
Juzi, baadhi ya wamiliki wa maduka katika eneo la Mwanjelwa, waliamua kufunga maduka baada ya kundi la vijana wasiokuwa na kazi kuwatishia na kuziba barabara kwa lengo la kusababisha ghasia, ili wapate fursa ya kupora mali.
Hata hivyo, mbinu hizo hazikuzaa matunda baada ya polisi kuingilia kati kwa kufyatua mabomu ya machozi na maji ya kuwasha, yaliyowalazimisha vijana hao kutawanyika.
Katika mazungumzo yake na viongozi wa wafanyabiashara, Kandoro alisema tayari amepokea malalamiko kuhusu bei za mashine hizo na usumbufu wanaoupata kutoka kwa watumishi wa TRA.
“Nimepokea malalamiko ya wafanyabiashara hao na malalamiko yao ni ya msingi, lakini mimi sina uwezo wa kutolea uamuzi, nimeyachukua kama yalivyo na kuyapeleka kwa Waziri Mkuu,” alisema huku akiwasihi wenye maduka kuyafungua.
Baadaye, Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Charles Syonga, alisema wamekubali kufungua maduka yao kwa maelekezo ya mkuu wa mkoa na kwamba wanaamini kuwa atafuatilia malalamiko yao.
Chanzo:- Mwananchi

No comments:
Post a Comment