Social Icons

Sunday 13 October 2013

WASOMI WAWASHANGAA VIONGOZI WA SERIKALI KUTOFAUTIANA KAULI.


HALI ya utendaji ndani ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), si shwari kutokana na mawaziri, manaibu wao na watendaji wengine kufanya kazi kwa visasi, chuki na kutoaminiana, Tanzania Daima Jumapili limedokezwa.

Kutoaminiana huko na utendaji wa kusuasua kunaelezwa ni dalili za kufa kwa serikali hiyo iliyodumu madarakani kwa muda usiopungua miaka 35.

Wakizungumza na Tanzania Daima Jumapili, wasomi, wanasiasa na wadau mbalimbali wameshtushwa na uendeshwaji wa serikali ambapo kila mtendaji huamua au kutoa kauli kwa utashi binafsi.

Miongoni mwa mambo yanayoelezwa kutia hofu ni kupingana kati ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli juu ya uzito unaoruhusiwa kwa wasafirishaji wa mizigo ya ndani na nje.

Hata hivyo Waziri Mkuu Pinda, aliufuta uamuzi huo huku akitaka watendaji wa serikali kuacha kutoa uamuzi bila kuwashirikisha wadau wa sekta husika.

Ingawa Pinda hakumtaja Waziri Magufuli kuwa ni mbabe, lakini mara kwa mara amekuwa akitajwa kufanya uamuzi unaokiumiza chama, wananchi na serikali yake.

Waziri Magufuli alitangaza kufuta msamaha wa asilimia tano uliokuwepo kwa magari yanayozidisha mzigo unaotakiwa katika mizani mbalimbali za hapa nchini, akisisitiza anasimamia sheria ya usalama barabarani sura ya 168 ya 2001 na kanuni zake.

Kanuni hizo zinataka malori kutozidisha uzito ghafi ambao kwa Tanzania ni tani 56 na endapo itatokea gari limezidisha basi usizidi asilimia tano ya unaotakiwa.

Uamuzi huo uliwafanya wamiliki wa malori nchini kupitia chama chao, TATOA, kugoma na hivyo kusababisha mizigo kukwama kuingia na kutoka jijini Dar es Salaam sambamba na bandari kuelemewa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana alisema yanayofanyika ndani ya serikali yanatokana na ulegevu unaosababishwa na wachambuzi wa sera na sheria za nchi kufanya kazi hiyo chini ya kiwango.

Alisema tatizo la mawasiliano kutoka idara moja hadi nyingine linamaanisha kifo cha utawala unaofanya kazi kwa mazoea.

“Hata sisi tulioko nje ya wigo wa serikali suala hili linatupa tabu sana, sheria ni ya serikali inapotungwa, Bunge linakuwa limeitunga na serikali kazi yake ni kuitekeleza.

“Inashangaza tunawapinga wanaosimamia sheria kwa kufuata masuala ya kisiasa, nadhani labda kuna tatizo la mawasiliano au tunaendesha nchi bila sheria kwa kuogopa kupoteza kura wakati wa uchaguzi,” alisema Dk. Bana.

Aliongeza kuwa waziri anapotoa tangazo la sheria kutekelezwa halafu mwingine anampinga au kutengua, inamaanisha wale waliokuwa wanapinga wana akili kuliko washauri wa serikali.

Dk. Bana alisema alishangaa kumsikia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Steven Wassira akisema kuwa wapinzani wasitarajie kuitwa tena Ikulu kuzungumzia mchakato wa katiba mpya kama vile alishaongea na Rais Jakaya Kikwete.

Alisema Wassira aliwafungia milango wapinzani, lakini Rais Kikwete amewaita keshokutwa azungumze nao, hivyo kumfanya waziri huyo aonekane alikurupuka kuzungumzia jambo hilo.

“Waziri wa Katiba na Sheria naye alijitokeza kuongelea jambo hilo zito, mimi nikajua kuwa huenda wameshaongea na rais kumbe hawajaongea naye ila walikurupuka tu, hii ni hatari kwa uongozi,” alisema.

Mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema kupingana huko ni dalili ya ugonjwa unaosababishwa na kutokuwepo miiko ya uongozi iliyowekwa na Azimio la Arusha.

“Wote wanaopingana labda wana nia nzuri ya kujenga taifa letu, lakini hakuna dira na mwelekeo, tumekuwa katika utawala wa familia ya kambale ambapo mjukuu na babu wote wana sharubu,” alisema.

Mnadhimu wa Upinzani, Tundu Lissu (CHADEMA), alipohojiwa kuhusu serikali kupingana alisema maana yake ni kushindwa kazi.

“Mimi nilitarajia waliotoa matamko yaliyopingwa na wakubwa zao hadharani walipaswa kujiuzulu kulinda heshima,” alisema.

Aliongeza kuwa anamshangaa Rais Kikwete ambaye baada ya kugundua kuwa watendaji wake wana kasoro ameshindwa kuwafukuza na badala yake amebaki anapingana nao.

CCM yawakingia kifua

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu viongozi hao kupingana, alisema haoni tatizo kwakuwa mfumo wa utawala bora una fursa hiyo.

“Sioni tatizo kiongozi wa juu kumpinga kiongozi wa chini, muundo huo upo na unazingatia ngazi za kiutendaji kwa mkubwa kutengua mamlaka ya aliye chini yake, hata hivyo sheria ni lazima zitumikie wananchi sio wananchi kutumikia sheria,” alisema.

Kauli za mawaziri zilizotenguliwa

Machi 2011, Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli alinukuliwa akisema: “Mheshimiwa rais, niliapa kulinda sheria na katiba ya nchi, hivyo ninaomba nipewe ruhusa kutekeleza sheria ya kubomoa nyumba zilizojengwa ndani ya hifadhi ya barabara, kwa madai kwamba waliojenga ndani ya barabara wamevunja sheria namba 13 ya mwaka 2007 na kwamba hawastahili kulipwa fidia.”

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwa mbele ya wananchi wa Chato licha ya kumsifu Magufuli, alisema serikali imemuagiza asimamishe zoezi hilo hadi litakapojadiliwa na Baraza la Mawaziri.

Rais Kikwete pia akiwa jijini Dar es Salaam alimzuia asiendelee na ubomoaji huo huku akimtaka pia aangalie ubinadamu katika bomoabomoa hiyo pamoja na historia ya eneo husika.

Wiki chache zilizopita, Waziri Mkuu Pinda alitengua tangazo la Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki la kuligawa eneo la Pori Tengefu la Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro, kwa kutenga kilomita za mraba 1,500 kwa ajili ya uhifadhi na kilomita za mraba 2,500 kuwa chini ya serikali za vijiji.

Machi 19, mwaka huu, Waziri Kagasheki alitoa tangazo la serikali la kuligawa pori hilo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 4,000 ili serikali iweze kuhifadhi eneo la kilomita za mraba 1,500 ambalo alieleza kuwa ni mapito na mazalia ya wanyamapori, pia kutunza ikolojia ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Tangazo hilo liliibua mgogoro mkubwa.

Hali hiyo haijaisha ambapo hata kwenye suala la mchakato wa mabadiliko ya katiba kumeonekana kupingana wazi wazi kati ya Rais Kikwete na Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge William Lukuvi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu Stephen Wassira, waliobeza kuhusu uwezekano wa rais kuonana na wapinzani kujadili suala la mchakato wa katiba.

Wassira alisema: “Wanasiasa wa upinzani kususia na kutoka ndani ya Bunge kwa hoja ya kutowashirikisha wananchi wa Zanzibar, hili si kweli, kwa sababu Kamati ya Katiba na Sheria ilikwenda huko, sasa wasitake kulalamika na kutaka kukutana na Rais Kikwete.

“Hawa tumewalea siku nyingi na sasa wanafanya mazoea, ninachotaka kuwaeleza wasitarajie tena kuitwa Ikulu, nchi hii inaongozwa na misingi na kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.”

Chikawe alisema endapo Rais Kikwete hatasaini muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013, kama wapinzani wanavyotaka atakuwa ameingia kwenye mgogoro na Bunge.

Kuyumba yumba kwa serikali pia kumeonekana siku za hivi karibuni katika suala la kufunga na kufungulia magazeti ya Mwananchi na Rai.

Chanzo:- Tanzania Daima.

1 comment:

Mpaju said...

Nimevutiwa na Uchambuzi wa swala hili. Lakini,haitakuwa vema mimi kubaki na dukuduku la machache niliyonayo juu ya uchambuzi huu.

Sikubaliani sana NA KUFANYA kazi kama mashine. Lakini sipendi zaidi, tabia ya kutofuatilia sheria kwa sababu za kisiasa za wakati HUO bila kujali sababu za KITAALAMU za MUDA MREFU. Hii inadhorotesha sana maendeleo ya JAMII. Hakuna MAENDELEO yasiyomdhulu mwananchi, kilicho muhimu ni kupunguza tu kiwango cha madhara,MAGUFULI AACHWE AFUATE SHERIA, kama HATUTAKI, bunge libadili hizo SHERIA. Na sidhani kama MAGUFULI anidhuru SERIKALI NA CCM,kwa upande wangu, anaijenga TANZANIA, ambayo kimsingi ndio lengo la CCM, LABDA kama ni tofauti na niwazavyo mimi!

 
 
Blogger Templates