Social Icons

Thursday, 10 October 2013

WENYE MALORI WAMBANA MAGUFULI.


WAKATI Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli akisema atahakikisha anasimamia sheria ili jitihada za serikali za kudhibiti uharibifu wa barabara zisidhoofishwe, wamiliki wa malori wamemtunishia misuli wakidai kuwa hawajagoma bali wameegesha malori yao wasiendelee kuharibu barabara.

Wamiliki hao walieleza kuwa waziri huyo amerudisha tozo ya asilimia tano kwa maslahi yake na amekuwa mtu ambaye haambiliki, hashirikiani na wadau pamoja na kujichukulia sheria mkononi.

Wakizungumza jijini Dar es Salaam jana, wamiliki hao walieleza kuwa sheria hiyo ilitangazwa na Magufuli kuanza kutumika Oktoba Mosi, na wao walipatiwa barua Oktoba 2 ya kueleza kuwa tozo hiyo imeondolewa hali iliyosababisha msongamano.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Consolidated Ltd, Karim Radha alisema kuwa wanaomba sheria hiyo ifuate utaratibu wa kwenda bungeni na kupitishwa.

“Kwamba wasafirishaji tunataka faida kubwa! Huo ni uongo na sheria ya tozo ipo nchi nyingi, hata kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na hata zile za SADC, aseme kuwa anaogopa barabara zake hazina viwango, hivyo zitaharibika,” alisema.

Davis Mosha kutoka Delina Group, alisema kuwa wao hawabishani na kiongozi ila waziri hana dhamana ya kuvunja sheria iliyopo miaka 40 iliyopita.

“Hatutaki kukurupuka kwenda mahakamani kama ambavyo waziri alisema, tunasubiri majibu, pia sisi hatupo kisiasa wala hatutumiki, hatujagoma ila tumepaki vyombo vyetu,” alisema.

Naye Ibrahim Ismail alisema kuwa tozo hiyo ilikuwepo kutokana na mizani zote kutokuwa na viwango sawa.

Naye Waziri Magufuli kupitia kwa msemaji wa Wizara, Martin Ntemo alisema kuwa nia ya serikali sio kuwatoza faini wasafirishaji hao bali kuwaona wakiwa wazalendo katika kulinda barabara nchini.

Alisema hivi karibuni kumejitokeza wasafirishaji wasio waaminifu waliokuwa na mawasiliano ya karibu na watendaji wa zamani waliokuwa wakishirikiana nao kupitisha mizigo kinyume cha taratibu.

“Mianya hiyo kwa sasa imezidi kudhibitiwa na hali kwa sasa ni nzuri tofauti na awali kabla ya kuwabadilisha wafanyakazi takriban 400 ambao ni sawa na asilimia 85 ya watumishi wote katika vituo vya mizani na kuajiriwa wapya,” alisema.

Ntemo alizipongeza baadhi ya kampuni za usafirishaji kuwa mfano wa kuigwa, akizitaja Dar Express, Cargo Star, Hood Bus, Coca Cola, BM Coach, Bakharesa (AZAM Transport), TBL, Golden Coach, Kanji Lanji Bus, Taqwa, Consolidated Logistic, Lamada na Puma.

“Kumbukumbu zilizofanyiwa uchambuzi kwa kipindi cha miaka kumi zimebainisha kuwa yapo makampuni ambayo hayana rekodi ya kuzidisha mizigo wakati wote yanapopimwa katika vituo vya mizani ya barabarani,” alisema.

Chanzo:- Tanzania Daima

No comments:

 
 
Blogger Templates