Social Icons

Saturday, 21 December 2013

MBUNGE ALIA NA RAFU KATIKA MKUFU

MBUNGE wa Viti Maalumu (CCM), Mary Mwanjelwa (48), amelalamika kuhusu madai yanayoelekezwa kwake kwa kumhusisha na tukio la kuiba mkufu wakati wa ziara yake ya kibunge nchini Ubelgiji, Septemba mwaka huu.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, ukweli wa tuhuma hizo umejikita katika malengo ya kisiasa kutoka kwa washindani wake, na hususan siasa za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Jumanne wiki hii, gazeti dada na hili, Raia Tanzania liliripoti kuhusu kuwapo kwa madai kwamba mbunge huyo ambaye anatumikia kipindi chake cha kwanza cha ubunge, aligundulika kuchukua mkufu huo na mmoja wa watu waliomuona wakati akifanya tukio hilo jijini Brussels.

“Mheshimiwa Mwanjelwa alikuja hapa Ubelgiji kuhudhuria mkutano wa masuala ya Mazingira wa wabunge wa nchi za bara za Afrika, Karibeani na Pasifiki (ACP) uliofanyika hapa Ubelgiji.

“Sasa siku moja akataka kwenda kufanya manunuzi mjini na ubalozi wa Tanzania uliopo hapa Brussels ukampa gari kwa ajili hiyo. Akaingia katika mojawapo ya maduka kwa ajili ya shopping hiyo.

“Akajaribu mkufu wa kwanza, akauvua. Akajaribu mkufu wa pili, akauvua. Akajaribu mkufu wa tatu, akauvua. Baadaye, akachukua ule mkufu wa pili na akauvaa lakini hakuuvua.

“Sasa kuna mtu alikuwa amemuona. Kwa sababu ya hofu ya kujulikana kwa tukio hilo, akatoa taarifa kwa ubalozi ambao nao haukuchelewa kutoa taarifa kwa Ofisi za Bunge na sijui kama wamechukua hatua yoyote,” kilisema chanzo cha habari cha gazeti dada na hili, Raia Tanzania linalochapishwa siku za wiki, isipokuwa Jumatano na Jumapili.

Mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo wa Ubelgiji, Mwanjelwa ambaye ni miongoni mwa wabunge wanawake wenye uwezo mkubwa wa kujieleza, alikwenda katika mojawapo ya nchi za Mashariki ya Mbali kwenye ziara nyingine ya kibunge.

Ni siasa za maji taka, wivu

Lakini katika mazungumzo yake na gazeti hili la Raia Mwema, Mwanjelwa alisema kinachoendelea ni siasa za majitaka na hakuna ukweli wowote kuhusu yeye kuhusika katika tukio hilo.

Mwanjelwa ambaye anatajwa kuwa kati ya wanasiasa wanawake wenye nafasi ya kufanya vizuri zaidi katika Uchaguzi Mkuu ujao, anasema amekuwa akiandamwa kwa muda mrefu na wabaya wake kisiasa na kati ya mamnbo yanayowakera maadui zake hao ni ufanisi wake kisiasa ndani ya Bunge na namna anavyowakilisha nchi kupitia Bunge, katika vikao mbalimbali vya kimataifa.

Mwanjelwa amepata kuwamo katika Kamati Maalumu ya Bunge iliyofuatilia urejeshaji wa chenji ya rada, fedha zilizopaswa kurudishwa nchini baada ya ununuzi wa kilanguzi wa iliyokuwa rada ya kijeshi nchini Uingereza.

Pamoja naye, wengine waliokuwamo katika kamati hiyo ni Job Ndugai, Musa Azzan Zungu na John Cheyo.

Kabla ya kuwa Mbunge, Mwanjelwa aliwahi kuwa Mkurugenzi wa miongoni mwa mashirika makubwa ya masuala ya afya za akina mama la PSI hapa na ni miongoni mwa akina mama wenye uwezo mzuri kifedha.


Chanzo;- Raia Mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates