Social Icons

Monday 6 January 2014

MWAKA 2014, NI MWAKA WA WATANZANIA KUAMUA MAKUBWA NA MUHIMU


WATANZANIA wanakabiliwa na mwaka muhimu sana katika historia yao kama jamii ya watu. Ni Mwaka ambao wanaitwa na historia hiyo kuchukua uamuzi mbalimbali ambao utaamua wao na watoto wao pamoja na watoto wa watoto wao wataishi vipi kwa miaka mia ijayo. Lakini pia wanaitwa kuchukua uamuzi ambao wao wenyewe na watoto wao wataishi vipi katika miaka mitano ijayo. Ni mwaka ambao kila Mtanzania anaitwa kufikiria vizuri, kuchunguza kwa umakini na hatimaye kufanya uamuzi ambao hatajutua.

Juu ya kura ya maoni ya Katiba Mpya

uamuzi mkubwa zaidi ambao naamini utagusa maisha ya kila Mtanzania ni kuhusiana na ujio wa Katiba Mpya. Mwaka huu mpya wa 2014 wananchi wataitwa kuamua kama rasimu ya Katiba Mpya inayopendekezwa ipite na kuwa Katiba Mpya au la. Ni vizuri kufikiria Katiba Mpya kama msahafu wa taifa. Vitabu vyetu vya dini vinavyoongoza maisha yetu ya kiroho hatukuwa na uchaguzi wa nini kiwemo ndani yake. Hatukuulizwa kama tunakubaliana na amri kumi za Mungu au kama tunakubaliana na nguzo tano za imani katika Uislamu. Hatukuulizwa kama tunakubaliana na yale ambayo yamo ndani ya vitabu hivyo lakini tulipokubali imani hizo tulikubali kujiweka chini ya uongozi wa maandiko hayo matakatifu.

Watu wanachukulia misahafu hii kwa uzito mkubwa sana kiasi kwamba wapo watu wamekufa kutetea mafundisho yake  - na wengine wanaendelea kufa. Watu wanajifunza misahafu hiyo na wanafundisha watoto wao na watoto wa watoto wao. Kila uchao kuna watoto wanaenda “mafundisho” na wengine wanaenda madrasa kujifunza imani hii chini ya walimu waliokubuhu. Na kila wiki mamilioni ya watu pote duniani wanafunga ndoa, wengine wanabatizwa, wengine wanasilimishwa na wengine wanazikwa katika imani hizi. Lakini ukweli ni kuwa tumekubali kama imani japo hatukuwa na kauli yoyote juu ya ukweli, utakatifu na hata uzito wa mafundisho yaliyomo ndani yake. Tumekubali kama imani kwa sababu tumekubali ujumbe wa wale walioleta mafundisho ya vitabu hivi.

Katiba ya nchi ni msahafu wa nchi kama nilivyosema; ni msahafu unaoamua maongozi na mwelekeo wa maisha ya kila mtu katika taifa. Hoja inaweza kujengwa kuwa Katiba yaweza kuwa na nguvu zaidi kuliko misahafu hiyo ya kidini. Misahafu ya kidini na mafundisho wake yanawafunga wale waliokubali mafundisho na imani hizo. Biblia inawafunga Wakristu kama Qurani inavyowafunga Waislamu; mtu aliyeamini katika imani hizo hana uchaguzi (hata kama hapendi). Anaweza kuamua kuasi au kutofuata imani hizo kwa uzito wake lakini mtu wa imani nyingine hana ulazima wa kufuata mafundisho ya dini nyingine. Katiba ya nchi; inawafunga watu wote sawasawa; haijalishi Ukristo au Uislamu wa Mtu; haijalishi elimu au umri wa mtu; haijalishi kabila, rangi, jinsi au hali na mahali pa mtu. Katiba Mpya ni kitabu chenye kuwafunga wote sawa.

Na uzito wake ni kuwa sisi kama wananchi ndio tunaamua kuwa nini kiwemo ndani yake na kiwe vipi. Japo mimi sijaamini kama mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya ni sahihi ukweli ni kuwa wapo watu wanaamini hivyo na hata mimi nitajikuta ninafungwa na Katiba  hiyo hiyo – hata kama sikubali mchakato wake – kwa sababu watu wengi watakuwa wameikubali. Mikutano na vikao vyote vilivyofanyika mwaka uliopita, mijadala na midhara yote iliyofanyika yote inahitimishwa kwa wananchi kuulizwa swali jepesi na la moja kwa moja – je unakubali rasimu hii ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano (au swali linalofanana na hilo). Wananchi watatakiwa kujibu jibu jepesi tena la “ndio” au “hapana”. Hii ina maana kabla mtu hajakubali au hajakataa ni lazima achukue muda kujifunza kilichomo ndani ya Katiba hiyo na akipime kama kinaendana na matamanio yake, njozi zake na kiu yake ya kuona utawala bora nchini.

Kimsingi itakuwa ni kura ya dhamira ya mtu mmoja mmoja. Hapa hakuna kura ya makundi; kila mtu kama mtu huru aliyezaliwa huru na mwenye utu wake ataitwa kupima yaliyomo ndani ya rasimu hiyo ambayo imekabidhiwa kwa Rais Kikwete, Jumatatu hii iliyopita na kuamua kama dhamira yake inakubali au la. Katika hili ni muhimu kuhakikisha kuwa mijadala itakayofanyika sasa ni lazima iwe huru kabisa.

Mojawapo ya mambo ambayo itapaswa kuyaangalia kwa makini zaidi ni kama watu wanaopinga Katiba Mpya watapewa uhuru wa kufanya hivyo. Hakuna kitu kibaya ambacho kitaharibu mchakato huu kama watu watajiona wanalazimishwa kukubali kwa sababu watu wengine wanasema ni “Katiba nzuri”. Ni lazima watu wenye hoja tofauti waachwe wapinge kwa hoja bila kutishiwa na kama watu wengine wanafanya kampeni ya kuunga mkono rasimu ni vizuri wale wenye kupinga nao wapewe haki hiyo hiyo ili wananchi waweze kuamua kwa haki zaidi baada ya kupima pande zote mbili.

Wale wanaopinga au kuunga mkono hawahitaji kukubaliana au kupingana na yote yaliyomo ndani ya rasimu ili wachukue upande. Ni vizuri kila mtu ajipime yeye mwenyewe na kuona ni mambo gani “angalau” yakiwemo basi ataunga mkono na mambo gani yasipokuwamo hawezi kuunga mkono. Ni muhimu hata hivyo kuchukua msimamo wa kuhakikisha kuwa yale mambo ya msingi kabisa yasipokuwepo basi usiunge mkono na kama mambo unayoaamini ya msingi yamo basi uunge mkono. Kwa mfano mimi binafsi bila kuwepo na sehemu mbili za Bunge, Tume Huru ya Uchaguzi kwa Taifa na kwa Mikoa, serikali moja ya Muungano, kutenganisha dini na serikali, na kurudisha madaraka mikoani siwezi kuunga mkono rasimu. Wengine wanaweza kuona vitu hivyo si vya msingi kwani wao wakiona  kama serikali tatu tu zipo basi wataunga mkono.

Huu ni uamuzi muhimu sana kwa Watanzania ni lazima tufikirie kwa makini kwani tutaamua ni aina gani ya utawala tunaotaka. Tutaamua yatakayokuwemo kwenye msahafu wetu kama taifa; na mambo ambayo kimsingi tunawatengenezea wale wanaokuja baada yetu (watoto wetu na watoto wa watoto wao!).

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Mwaka huu vile vile ni mwaka wa uchaguzi wa serikali za mitaa. Sehemu ya kwanza kabisa ya serikali ambayo wananchi wa kawaida wanakutana nayo kila siku ni serikali za mitaa. Ni hapa ndipo ambapo wananchi wanajifunza utendaji wa serikali ni huku wanakoona serikali kazini na karibu na wananchi kuliko sehemu nyingine yoyote. Hivyo, Watanzania ni lazima waangalia maisha wanayoishi mitaani kwao, waone jinsi ambavyo serikali imetenda kazi kwa miaka yote iliyopita na kama wanajiona wameridhika basi wanajua warudishe serikali ya namna gani mitaani kwao. Ni uchaguzi wa zaidi ya sura za watu; ni uchaguzi wa mwelekeo wa serikali yao. Kinyume na watu wengi wanavyofikiria mfumo wa uchaguzi wote unalenga kuchagua chama zaidi kuliko mtu, kabila, rangi au dini yake.

Uamuzi huu wa serikali za mitaa utakuwa ni utangulizi wa uchaguzi wa rais na wabunge mwakani. Kuanzia sasa hadi wakati huo tutashuhudia watu na makundi ya watu yakijaribu kujijenga mbele ya Watanzania; Wananchi wanaitwa kuwafuatilia watu hawa na kuamua kama wanafaa kuwa viongozi wao. Tutafanya makosa kama tutaangalia majina ya watu au ukwasi wao badala ya kuangalia historia yao na misimamo yao. Kuanzia mitaani hadi Ikulu ni lazima tuangalie ni nani anafaa kutuongoza kwa uadilifu kwa miaka mitano ijayo. Tayari tumeshaona viongozi wanaopita sasa hivi; tusisubiri viongozi ambao wanaanza sasa kupita na kutulamba miguu huku wakijichekesha chekesha wakati miaka yote iliyopita walijifanya wamesahau wametoka wapi.

Kiongozi yeyote anayejitembeza na kujibembelezesha mbele za wananchi bila kuonesha rekodi ya utendaji wake ni viongozi wakufikiriwa mara mbili. Iweje mtu miaka karibu mitatu awe hana rekodi yoyote ya maana ya kuonesha? Leo aanze kuleta mabati na madawati na wapo watu wanaweza kudanganyika kirahisi? Ndio maana nasema ni mwaka wa uamuzi mzito na muhimu!

Katika mambo yote Watanzania ni lazima tujihakikishie uhuru wetu kufikiri na kuamua bila kujali vitisho, ahadi au vitu vingine. Tufuatilia hoja za Katiba Mpya na tuwafuatilie watoa hoja wanaotaka uongozi. Tusiogope au kukubali kuogopeshwa; tukichagua vibaya au kwa sababu ya kuona aibu, kupendelea watu au woga tujue tunalazimika kukubali matokeo ya uongozi huo. Tayari tumeona watu wengine walianza kujuta baada ya uchaguzi wa 2010 lakini ni hao hao walikuwa kimberembere kupigia debe viongozi ambao watu walishajua hawafai.

Tusikubali kuburuzwa tena na wanasiasa uchwara wa zama hizi. Iwe kwenye Katiba Mpya, Serikali za Mitaa au Uchaguzi Mkuu; Watanzania tuamue kuwa huru kusimamia uchaguzi wetu na utu wetu. Mwisho wa siku hatuna kitu kingine cha kupoteza zaidi ya utu na uhuru wetu.

Heri ya Mwaka Mpya 2014 Wenye Fanaka na Baraka Tele


Chanzo:- Raia Mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates