Social Icons

Thursday, 6 February 2014

MBADALA WA CCM, CHADEMA SI TIBA YA VIRUSI VYA KIMFUMO

NIKIRI kwamba mimi ni miongoni mwa wafuatiliaji wazuri na makini wa makala za Dk. Kitilla Mkumbo ndani ya gazeti hili la Raia Mwema. Binafsi, naamini, Kitilla ni mwanadamu kama wanadamu wengine. Udhaifu upo na mazuri ya kuigwa kutoka kwake yapo. Katika hayo, kuna sifa moja kuu inayonifanya niwe mfuatiliaji wa karibu wa maoni yake. Sifa hiyo ni hii: Kitilla ni mkweli. Naam, ni mahiri katika kuwasilisha hisia zake mbele ya hadhira bila kujali ibuko la buhuti na kereheko mioyoni mwa hadhira. Naam, yuko tayari kuutetea msimamo wake kwa hoja bila kuangalia matokeo ya gharama ya kufanya hivyo. Hicho tu, ndicho kinachonisukuma kufuatilia maoni yake hata kama sikubaliani na baadhi ya misimamo yake kifikra. Kwa ujumla ningependa awe rafiki yangu!

Kutokana na upenzi huo, tukio la kufukuzwa na chama chake kwa madai ya usaliti lilinihuzunisha sana. Mtu huyu amefukuzwa wakati chama kina uhitaji mkubwa wa rasilimali watu wa sampuli yake. Kama ni suala la mabadiliko, kwa mtazamo wangu, Dk. Kitilla ndiye aliyepaswa kuwa Mwenyekiti wa chama hiki. Katika hili hata viongozi wa juu wa CHADEMA watakubaliana nami ya kwamba msomi huyu ametulia kiakili, kihisia na kimaono na ni mkweli asiyependa makuu. Chama hiki kimepoteza mtu muhimu sana katika medani ya siasa!

Nikiwa mmoja wa waumini ndani ya muktadha wa umuhimu wa mabadiliko ndani ya chama kikuu cha upinzani, sijavutiwa na mbinu za jopo la wasomi hawa kufanikisha mabadiliko hayo. Na wala sikubaliani na mtazamo wa hivi sasa wa Dk. Kitilla wa kushawishi umma wa Watanzania ya kwamba matatizo ya kimfumo yaweza kutatuliwa kwa kuasisi chama kipya cha siasa. Siamini pia kama Zitto Kabwe ni mtu anayestahili kuwa mwenyekiti wa chama hicho cha kufikirika mara baada ya kufanikisha mchakato wa mabadiliko hayo. Sababu kuu ni hii, mbinu waliochagua kuleta mabadiliko inakidhoofisha chama badala ya kukihuisha na Zitto wanayempigania, mwenye harufu ya usaliti usiotiliwa shaka.

Hilo ni doa kubwa kwa kiongozi yeyote yule. Hilo nililifafanua kwa kirefu kwenye baadhi ya makala zangu. Kutokana na harufu hiyo, wale wote walioandaa mikakati ya kumweka madarakani kiongozi asiyesomeka vizuri mbele ya wale wenye jicho la tatu, wamejikuta wakijinakshi kwa taswira fifi ya usaliti! Naomba sasa tujikite kwenye hoja yetu ya msingi.


Muktadha wa mfululizo wa makala za ndugu Kitilla, mara tu baada ya kufukuzwa uanachama ndani ya CHADEMA, una hoja muhimu inayotawala. Katikati ya moyo wa makala hizo kuna ladha ya ushawishi kwa umma wa Watanzania  kwamba mparaganyiko wa kimaono na kimaadili wa vyama viwili vikuu vya siasa, CCM na CHADEMA, unahitaji tiba ya haraka. Kisha ameweka bayana ya kuwa tiba stahiki ni kuwa na chama mbadala wa vyama hivyo, chenye nguvu na nidhamu ya hali ya juu. Ili kufikia malengo hayo, akaongezea,  kutakuwa na safari ndefu. Kwamba ili kuwa na chama kikuu cha upinzani mbadala wa vyama hivi viwili chenye hadhi ya CHADEMA yaweza kuchukua miongo miwili.

Huo ni ukweli mtukuka, lakini, wenye suluhisho lenye makengeza ya kimaono. Tutaona. Tuseme, kuna mshehenezo wa ukweli ndani ya makala za Kitilla kuhusu mwenendo wa chama hiki pinzani ambao udadavuzi wake waweza kuanza kwa gia hii: iwapo kuna mtu anasiyekubaliana na mchezo mchafu wa kuwekeza akili zake rehani ndani ya kapu la ushabiki wa kisiasa unaonajisi mtiririko wa fikra huru, basi mtu huyo hawezi kukubaliana kwa asilimia zote na mwenendo wa kiutendaji, kimaadili na kiuamuzi unaoendelea ndani ya viunga vya CHADEMA. Mchakato wa uamuzi wa kisiasa ndani ya chama hiki una ladha ileile inayokerehesha. Ladha ya upofu wa kutokubali kukosolewa. Ladha ya kutumia ubabe badala ya hekima na busara katika kufikia uamuzi. Ladha inayoambatana na mzio dhidi ya fikra zozote zile zinazokinzana za mwelekeo wa kundi la wateule wachache. Mwandishi, Robert A Heinein ameandika hivi; “A society that gets rid of all its trouble makers goes downhill.” Kwamba, jamii inayowafukuzia mbali wasumbufu wote inaelekea  kuvingirikia chini ya kilima!

Wakati huo huo ukakasi wa kuabudu fikra za wateule wachache pamoja na waasisi wa chama hata kama fikra hizo ni dhoofu, chovu na za hovyo, umeingia na kutamalaki ndani ya viunga vya chama hiki cha siasa na kusababisha umajeruhi wa wale wote wenye fikra huru na kiu ya kuleta mapinduzi ya kweli kifkra, kimaono na kimfumo. Tatizo ni hili: wakati wapo waumini wenye kiu ya kweli ya mabadiliko ndani ya CHADEMA, kama ilivyo ndani ya chama tawala CCM,  ndani ya msafara huo-huo wa kiu ya mabadiliko kuna kenge wa kutosha kuwafunika mamba halisi kwa kivuli fifi cha usaliti.

Tatizo linakuwa kubwa zaidi pale ambapo hata hao wenye kiu ya mabadiliko ya kweli wakiwa bado wana upungufu wa kinga dhidi ya virusi vya kimfumo wanavyodai kupambana navyo kwa udi na uvumba. Tatizo pacha ya hilo ni pale wapambanaji hao wanapoonekana kukosa misuli imara ya uthubutu, maono, mikakati yakinifu, na mtandao mpana kiintelijensia ili kubaini hila za chama tawala za kudhoofisha harakati hizo. Matokeo yake wameshindwa kujitengenezea mwonekano wenye kuwapambanua kama manabii wa kweli na kuwajengea imani ndani ya chama wanachodai kukipigania! Ni kizungumkuti ndani ya mtikisiko wa kimaono.

Wakati chadema kikijinasihi kuwa kina lengo la kupambana na ufisadi wa kimfumo unaolitafuna taifa, mimi binafsi bado sijaona dhamira ya dhati ya usimamizi na uendeshaji wa chama kwa uadilifu uliotukuka. Kwa mujibu wa barua ya Chacha Wangwe, aliyoiandika kabla tu ya kufariki kwake, zikiwamo tuhuma za hapa na pale kutoka kwa mahasimu wao kisiasa wenye joho la usaliti zenye kubeba ukweli usiotilia shaka, na kwa kuutathimini mwenendo wa chama hiki katika eneo hili la ufisadi, eneo ambalo ndiyo ajenda kuu ya chama hiki,  inahitajika akili mbadala wa akili pevu, kuamini kuwa CHADEMA ni chama chenye dhamiri ya dhati ya kupambana na ufisadi.

Ugonjwa wa mfumo wa chama kimoja, uliokuwa ukiabudu fikra za waasisi hata kama zina matobo, ndio unaoonekana kurithiwa na chama kikuu cha upinzani CHADEMA kiasi cha kufifisha taadhira ya njozi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya kuwa na chama mbadala, kwa maana ya kuwa na fikra mbadala na wala sio nakala (photocopy). Huu ni ukweli mchungu kwa wale wenye kiu ya mabadiliko. Chama kinaendeshwa kwa hisia badala ya kuendeshwa kwa hekima na busara, kinapaswa kutazamwa kwa jicho kali kwa mrengo wa tahadhari.

Tatizo kuu la mwenendo  usiotia matumaini ndani ya vyama hivi liko wapi hasa? Je, tiba itakayoleta ahueni kwa raia wa Tanzania ni ipi hasa?  Hapa ndipo inapoanzia njia panda baina ya shule ya mawazo yangu na ya Kitilla, pamoja na wengine wenye fikra kama zake. Tofauti yangu na Kitilla  haijajengwa juu ya tofauti ya kimtazamo juu ya  taswira tunayoiona ndani ya CHADEMA bali ni juu ya namna sahihi ya kushughulikia ugonjwa wenyewe. Tofauti ya shule zetu za mawazo baina yangu na Dk. Kitilla ni juu ya tiba stahiki. Dk. Kitila anatoa suluhisho la tatizo la kimfumo kwa kuunda aina nyingine ya chama kiteule ndani ya jamii ileile iliyolewa kwa mvinyo wa kimfumo.

Anatoa tiba ya kuwa na chama mbadala ndani ya mfumo unaorutubishwa na kurutubika kutokana na elimu isiyohandisi raia wavumilivu ndani ya mawimbi ya fikra kinzani. Mfumo wenye raia wepesi kustahimili dhoruba na mikikimikiki ya hoja mbadala. Naam, wanaofura kama vifutu pale maono yao yanapotupwa jalalani mithili ya takataka kwamba ni ya hovyo au yana mashiko. Katika hili, Kitilla anataka tuamini kuwa iwapo tutanunua kiriba kipya, kwa maana ya chama kipya, na kisha kutia mvinyo uleule wa zamani uliochacha, kiriba hicho kitaweza kujifanyia muujiza wa kugeuza mvinyo ulioharibika na kuwa divai mpya! Tiba hiyo ni ya kimuujiza zaidi. Tiba inayohitaji kiasi fulani cha uwendawazimu kuweza kuunga mkono kwa kuipigia makofi, vifijo na nderemo!

Wakati taswira ya kisiasa ndani ya CHADEMA inaakisi mfumo unaotamalaki kitaifa. Mfumo wa ubinafsi na kutovumilia mawazo mbadala, hali ambayo hata Dk. Kitilla amekiri wazi kwamba chimbuko lake ni mfumo wetu wa elimu butu, usiojali uwekevu wa maono mapevu, Kitilla anatoa suluhisho mbadala lenye ukweli na upogo kwa mbali; anapendekeza ianzishwe midahalo shuleni ili kusaidia uhandisi jamii ya Watanzania wenye kushindana kwa nguvu za hoja. Ni hoja. Hata hivyo naomba abatizwe ndani ya ukweli huu wa ziada ili kushibisha hoja yake. Tatizo kubwa la wapinzani wa fikra za mabadiliko chanya ni la kimaadili zaidi kwa maana ya kusukumwa na tabia ya ubinafsi.

Midahalo, kwa sehemu kubwa, inawapa wasomi uwezo wa kujenga na kupangua hoja. Midahalo  haiwezi kufanikisha zoezi la kufinyanga jamii ya watu waadilifu hata kama watapewa fursa ya kudahalika tangu asubuhi hadi jioni. Katika hili, Dk. Kitilla anapaswa kusimama kizimbani ili kujibu maswali yaliyostawishwa kwa mboji ya ushawishi wake wenye nakisi ya uhalisia wa mambo. Je, kwa vile gonjwa la CHADEMA chimbuko lake ni la kimaadili kwa maana ya kuhandisiwa kimfumo, ni mikakati gani itatumika,  ili kupata ‘krimu’ ya wanachama wa sampuli isiyo na virusi vya mfumo uliowahandisi? Je, chama hicho cha kufikirika kitaanzisha viwanda vya kuhandisi sampuli hiyo wapi?  Je, ni mwezini kusikofikiwa na virusi hivi vya kimfumo? Bahati mbaya huko hakuna wanadamu! Je, ni kinga gani itakizuia kisikabiliwe na mkwamo wa kiburi cha mafanikio kama ilivyo kwa vyama hivi viwili? Tuseme, na hata kama kingefanikisha mpango huo, bado chama hicho kitapaswa kufanya kazi ndani ya jamii ile ile, iliyonajisika kimfumo.

Kwa vile tatizo ni la kimfumo, je, ipi njia ndefu na yenye gharama kubwa kuliko nyingine kati ya hizi mbili. Njia ya kwanza; kuendelea na mapambano dhidi ya virusi vya kimfumo ndani ya CHADEMA na pembezoni mwake. Njia ya pili; kuanzisha chama kipya ndani ya jamii ile ile yenye mfumo butu. Wakati tathimini ya haraka ya Kitilla ni kwamba ili kulifikia lengo kusudiwa njia ya pili inaweza kutumia miaka ishirini, je, haoni kuwa iwapo Watanzania watapewa elimu stahiki, njia ya pili inaweza kuchukua muda mfupi zaidi?

Kwa maoni yangu, naliona tatizo la itifaki ya hoja za Dk. Kitilla juu ya tiba ya tatizo la vyama hivi viwili vya siasa. Akiwa kama mjenzi wa hoja za kisomi, katika makala zake ameibua wazo linalokinzana na muktadha wa kile anachokijengea ulinzi kwa wigo wa dhahabu. Tiba ya matatizo ya kimfumo yapaswa kufanyika ndani ya mfumo huo huo na sio nje. Chumvi bora yapaswa kuwekwa ndani ya chakula na wala sio pembezoni. Dk. Kitilla usiishiwe pumzi. Endelea kuuelimisha umma wa Watanzania ili wajue kufanya uamuzi stahiki na wala si kuwashawishi kuanzisha utitiri wa vyama. Tafakari.


Chanzo:- Raia Mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates