Nairobi. Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya, Mutea Iringo ameingia matatani baada ya Mahakama Kuu nchini humo kuagiza akamatwe kwa kushindwa kumfidia Mtanzania, James Koroso Sh573.5 milioni.
Agizo hilo lilitolewa na Jaji George Odunga wa Mahakama Kuu baada ya Koroso kushinda kesi ya kuwekwa kizuizini na kuteswa kimakosa.
Mahakama iliamuru Koroso alipwe Sh31 milioni za Kenya (Sh 573.5 milioni za Tanzania) lakini hadi mwanzoni mwa wiki hii, Iringo alikuwa
hajatekeleza agizo hilo.
Kwa kushindwa kutekelezwa amri hiyo, Mahakama ilitoa agizo kwa kumtaka Mkuu wa Polisi Kenya, IGP David Kimaiyo kuhakikisha anamkamata Iringo na kumfikisha mahakamani ili aeleze ni kwa nini asishtakiwe kwa kukiuka amri ya Mahakama.
Kosoro aliieleza Mahakama kuwa maisha yake yako hatarini kutokana na vitisho vinavyotolewa kwake na maofisa wa Serikali kwamba atauawa kama akiendelea na madai yake mahakamani.
Hata hivyo, IGP Kimaiyo alisema wanatafuta utaratibu wa jinsi ya kumkamata Iringo kwa kuwa wanaepuka kumdhalilisha.
Msemaji wa Polisi, Masoud Mwinyi hakuelezea taratibu hizo lakini alisema hatua madhubuti zitachukuliwa kwa muda mwafaka.
“Hatutaki tuone Serikali inaidhalilisha Serikali. Tunataka kuhakikisha unafanyika utaratibu unaofaa,” alisema Mwinyi.
Kosoro alifungua kesi hiyo baada ya kuweka kizuizini na kuteswa Desemba 19, 1993 na Serikali ilitakiwa kumlipa fidia kutokana na kosa hilo lakini hadi sasa haijatekeleza amri hiyo.
“Pamoja na kutakiwa kulipwa fidia lakini Serikali imeendelea kukiuka amri ya Mahakama na badala yake nimekuwa nikipigiwa simu na maofisa wa Serikali ambao wananiambia hii ni Kenya na mimi ni mgeni hivyo naweza kupoteza maisha kama nikiendelea kufuatilia madai yangu,” alisema Kosoro.
Kosoro alisema maofisa wa polisi wa Kiambu walimkamata mwaka 1993 na alishikiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi wakati jeshi hilo likifanya uchunguzi dhidi yake kwa ujambazi. Alisema alizuiwa kuwasiliana na mtu yeyote na alikuwa akipigwa akiwa chini ya ulinzi.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment