Dodoma. Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Seif Idd ametangaza vita kwa mtu yeyote anayepanga njama za kuvuruga mchakato wa Rasimu ya Pili ya Katiba.
Hata hivyo amebeza kauli ya makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad aliyoitoa juzi kwenye viwanja vya Kibandamaiti Zanzibar akisema kuwa kiongozi huyo hana uwezo wa kufanya chochote kisiwani humo.
Juzi katika hotuba yake Hamad alisema chama chake hakiko tayari kuunga mkono suala la Serikali mbili na wala suala la hotuba ya Rais Jakaya Kikwete bali wako katika misingi ya hotuba ya Jaji Warioba.
“Mheshimiwa Hamad hana uwezo wa kufanya jambo lolote visiwani Zanzibar. Zaidi ya yote ataishia kusema tu bila ya mafanikio na ndiyo maana Wazanzibari wameshatambua kuwa mzee yule ni mwongo,” alisema Balozi Idd.
Alisema hali ikiendelea hivyo na Serikali ya Mapinduzi haitasita kuwashughulikia watu wote wa aina hiyo.
Kuhusu nafasi ya Makamu wa Kwanza alisema kuwa alitoa kauli ile kwa nafasi yake ya katibu wa chama cha CUF, lakini hakuwa amesimama kama makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Makamu huyo alipinga kauli kwamba Wazanzibari hawataki serikali mbili kwa kuwa hakuna aliyeulizwa juu ya jambo hilo.
“Kule Zanzibar tuko karibu watu 1.3 milioni, sasa nani aliulizwa kama si uongo wa kutaka kuwagombanishwa watu. Wanafanya ubaguzi usio na maana na hiyo ni choyo tu,” alisema.
Aliwataka wananchi wa Serikali ya Zanzibar kupuuza kauli za makamu wa kwanza wa Serikali ya Zanzibar kwa madai kuwa kauli zake ni kwa masilahi yake na chama chake.
Alisema kwa sasa inaonekana kuwapo na baadhi ya wanasiasa ambao wana mpango wa kukwamisha mjadala wa kujadili Rasimu ya Katiba, ikiwamo kikundi cha Ukawa.
Huku akionekana kuunga mkono hotuba ya mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ina mashiko na ni nzuri lakini akaponda suala la serikali tatu.
Aliwatupia lawama wanasiasa kuwa wamekosa uvumilivu na utashi wa kweli katika kupata Katiba ya nchi.
Chanzo:- Mwananchi
No comments:
Post a Comment