Social Icons

Monday, 31 March 2014

Chadema ianzishe mageuzi ya ndani, vinginevyo ni vigumu kuiondoa CCM 2015


Kama kuna vitu vya kusikitisha na wakati mwingine kukatisha tamaa ni mgongano ambao umekuwa ukifukuta kwa muda ndani ya CHADEMA kiasi cha kuwa kama doa chafu ambalo halipaswi kuvumilika. Mambo ambayo yametokea Arusha, Mwanza, Mbeya na sasa BAVICHA yanaashiria kuwa kama CHADEMA haitaamua kujiangalia ndani na kuanzisha mabadiliko ya mfumo na muundo wake basi kuiangusha CCM na kuiondoa madarakani mwaka 2015 itakuwa ni ndoto ya kutamania tu lakini kamwe haitatokea.


Migongano hii ambayo imeishia katika watu kutimuana na kutuhumiana imesababisa watu kuzungumzia migogoro ndani ya chama kuliko maono yake kwa taifa. Wiki hizi chache zilizopita zimesababisha mazungumzo mengi ndani ya CHADEMA na nje yake yawe ni kuhusiana na kundi la vijana ambao walituhumiwa kuendesha uasi ndani ya chama kuliko kuzungumzia mipango ya CHADEMA kushika dola. Tumeshuhudia kwa masikitiko makubwa wale wanaoitwa wapiganaji wakitumia muda mwingi kupigana wenyewe kwa wenyewe na sisi ambao tuko kwenye mitandao ya kijamii tumeshuhudia siyo tu kurushiana risasi bali mishale, visu, misumari, mawe na ndoana! Inaudhi, inasikitisha na inaacha maswali mengi kweli.


Tushukuru Mungu CHADEMA haikushinda uchaguzi mkuu wa 2010?

Jinsi ambavyo migogoro na milumbano ya chini kwa chini kati ya viongozi wa CHADEMA ambayo yamefikia mahali pa kulipuana kumenifanya nibakie na swali ambalo limenikaa kichwani kwa wiki sasa; je wale waliounga mkono CHADEMA washukuru Mungu kuwa haikushinda uchaguzi mkuu? Swali hili linakuja kwa sababu najiuliza kama CHADEMA wangeshinda mwaka 2010 wangeunda serikali ya namna gani? Je wangeweza kuaminiana?

Je wangeweza kuunda serikali ya namna gani? Je siyo kwamba wao kwa wao wangeanza kuhujumiana na kurushiana vijembe? Kwa wale ambao tulikuwa tunafuatilia siasa za ndani ya CCM hasa baada ya kujiuzulu kwa Lowassa Februari 2008 tunakumbuka jinsi ndani ya CCM kulivyozuka malumbano ya wao kwa wao, kunyemeleana, kuchimbana na hata – tukiamini maneno ya Rais Kikwete Butiama – ilifika mahali wao kwa wao CCM wanaogopa kuachiana glasi za maji mezani kwa kuhofia kutiliana sumu. Je hili ndilo ambalo nalo lingetokea ndani ya CHADEMA? Leo hii tunaona kuwa CCM chama chenye mifumo ya zamani na ambacho kina nyenzo nyingi za kushughulikia uasi imeshindwa kufanya hivyo je CHADEMA ingeweza?


Tumeshuhudia pamoja na majigambo yote ya “kujivua gamba” CCM imeshindwa kujisafisha na badala yake wameamua kuvumiliana, kubebana na kulindana huku wale waliokuwa ni watuhumiwa vitendo vya ufisadi wakijipanga vizuri zaidi kuweza kuendesha kampeni ya kufa mtu kuugombea urais. Sasa kama CCM pamoja na watu wake wote mashuhuri ambao walijipambanua kuwa ni wapinga ufisadi leo si wameshindwa? Wameshindwa si kwa sababu hawakuwa na nia bali kwa sababu mgawanyo ulioko ndani yake ni zaidi ya maslahi; ni mgongano wa binafsi (personal conflict) na hauaisha na naweza kusema hautaisha hadi ama Lowassa awe Rais mwaka 2015 au akataliwe. Na akiwa Rais nina uhakika wa kutosha tu kuwa mpasuko wa CCM utakuwa ni kamili!


Sasa leo CHADEMA ambao wanatarajiwa kuwa ndio wenye kuleta nuru mpya ya uongozi inapofika mahali wanachubuana wenyewe, hakuna nidhamu na kushindana kila siku kama wangeweza kuuchukua Urais kweli nchi ingekuwa salama? Je, kama mgongano huu ukiendelea kuvumliwa na kudharauliwa huku viongozi wakuu wa chama wakifunika vichwa vyao kama mbuni wakidai ati hakuna ‘mgongano’ ni ‘demokrasia’ kweli CHADEMA itaweza kupambana na CCM na kushinda uchaguzi mkuu? Kama leo kina Maige wananukuliwa wakimchimba vijembe Katibu wao wa Uenezi Nape si tunaweza kukuta hayo hayo yanatokea ndani ya CHADEMA kama ingeunda serikali ambapo baadhi ya wabunge wake au viongozi wake wangeanza kuirushia vijembe serikali yao au viongozi wao?


Mfumo wa CHADEMA wa sasa unalea mno uzembe na viongozi wanaosumbua!


Wengi wetu tumekuwa tukilalamika sana jinsi serikali ya CCM chini ya Rais Kikwete ilivyojenga mfumo wa kubebana, kulindana na kuvumiliana kiasi kwamba hadi mtu afukuzwe kazi au aondolewe kwenye nafasi yake basi ni lazima awe amevurunda mno – awe ameboronga. Na hata akiboronga bado kuna muda mrefu sana wa mtu huyo kupewa nafasi nyingine sehemu fulani. Mfumo huu wa CCM ndio uliozaa ufisadi na matokeo yake kwa taifa ni maangamizi.


Sasa mfumo kama huo huo ukiangalia kwa karibu unaona ukifanya kazi ndani ya CHADEMA. Ni mfumo wa kuvumiliana, kusubiriana na kutegeana. Ni mfumo ambao kwenye serikali ya CCM utasikia wanasema “mwenye ushahidi alete” wakati kwa CHADEMA ni mfumo “kutafuta ushahidi zaidi”. Matokeo ya mifumo yote miwili ni kuwa serikali inalea viongozi wabovu, wabinafsi na hatari kwa taifa na CHADEMA inajikuta inavumilia viongozi wabovu, wabinafsi na hatari kwa maslahi ya chama. Matokeo yake ni kuwa CHADEMA itajikuta na yenyewe inazaa serikali dhaifu!


CHADEMA ibadilike sasa vinginevyo ijiandae kuwa msindikizaji


Sasa ninachokisema hapa ni kuwa uongozi wa CHADEMA usijifanye wao Mbuni; wanafichwa kichwa mchangani. Tatizo la CCM ambalo limechelewesha chama hicho kujisafisha na kuweza kubadilika ni imani kuwa kinapendwa. Na kweli wapo watu wanaoipenda CCM kama mtoto anavyompenda mzazi wake. Wapo ambao wameapa kabisa kuwa liwalo na liwe wao na CCM milele. Mapenzi ya namna hii hayajali ubovu, mapenzi ya namna hii hayajali CCM inatawalaje au inaongoza vipi. NI mapenzi ambayo ‘hayaoni wala hayasikii’. Ni sawa na mapenzi ya wapendanao wawili ambapo licha ya mausia ya watu kuwa mmoja wao ni jambazi au ni kahaba wapenzi hao hawataki kusikia maneno hayo kwani wanaona ni ya watu wenye wivu, ambao hawataki mapenzi yao yafane. Hadi siku moja mmoja auawe kwenye matendo yake machafu ndio watu wanaanza kushangaa ‘mbona sikujua’!


Mabadiliko ya msingi ya CHADEMA ni lazima yaanzie kwenye Katiba yake


Binafsi naamini kuwa moja wapo ya mambo yaliyochangia kwa kiasi kikubwa kwa CHADEMA kushindwa kwenda Ikulu mwaka 2010 ni Katiba yake ambayo imenakili kwa kiasi kikubwa mfumo ule ule wa CCM – yaani Chama kimejengwa kutoka makao makuu na kinaongozwa kutoka juu. Ni mfumo mbaya kwa sababu unategemea maamuzi ya juu kuweza kugusa uongozi wa chini kabisa na katika demokrasia mfumo huu ambao umetengenezwa kutoka juu kwenda chini ni mfumo mbaya. CHADEMA inajikuta inalazimika kujibu na kushughulikia mambo yanayotokea chini kutoka makao makuu.


Ipo mifano mingi ya kuweza kuonesha hili likifanyika lakini miwili inatosha kuitaja hapa. Baada ya baadhi ya viongozi wa CHADEMA Karatu kuangaza kugongana ilimlazimu Mwenyekiti wa Taifa Mbowe kwenda Karatu na kujaribu kupatanisha pande mbili na kujaribu kutafuta suluhisho. Na tumeambiwa suluhisho limepatikana. Jingine na suala la BAVICHA ambapo baadhi ya vijana wamejikuta wakitumuliwa toka BAVICHA na CHADEMA kutokana na lundo la tuhuma dhidi yao. Uamuzi huo umechukuliwa na BAVICHA Taifa. Sasa baadhi ya watu wanaweza kuona ni jambo zuri lakini kwangu linathibitisha tu ubovu wa mfumo huo – huwezi kutatua kila kitu toka makao makuu! Ni lazima Chama kiwe na mifumo inayoweza kushughulikia matatizo ya chini au ya ngazi fulani na yakaishia huko huko bila kulazimika kwenda makao makuu.


Ili kuweza kuleta mabadiliko ambayo yataisaidia CHADEMA kujipanga naamini mabadiliko ya harakaya Katiba ya CHADEMA yanahitajika. Kama nilivyowahi kuandika nyuma kuhusu CCM kuwa ilihitaji Mkutano Mkuu Maalum wa Chama ili kijisafisha – hawakufanya hivyo – naamini CHADEMA nayo inahitaji Mkutano wake Mkuu (Baraza Kuu) kuweza kukaa chini na kupitisha mabadiliko ya msingi ya Katiba ili kuweza kukipanga chama. Mabadiliko hayo ni lazima –kwa maoni yangu – iweke mambo yafuatayo (pamoja na mengine mengi).

  • a. Viongozi wa juu wa Chama wa Kitaifa wasiwe wabunge – Wabunge wawe wabunge wasishike nafasi za uongozi makao makuu ya chama – hili nimuhimu kwa ajili ya kuweza kusimamiana (checks and balances).
  • b. Viongozi wa kitaifa wanaotaka kugombea nafasi yoyote ya kuchaguliwa (ubunge, udiwani au Urais) ni lazima waachie madaraka (wajiuzulu) nafasi zao mara wanapotangaza nia ya kugombea nafasi hizo. Hii itazuia viongozi wa kitaifa kutumia raslimali za chama kusaidia kampeni zao au za watu wao wa karibu.
  • c. Mgawanyo wa fedha za ruzuku uongozwe na kanuni zilizowekwa kikatiba ambapo kiasi kikubwa cha fedha kinaenda mikoani na ngazi zachini kujenga chama badala ya kutumika makao makuu. Makao makuu ipewe uwezo wa kubuni na kuendesha miradi ya chama kukipatia kipato.
  • d. CHADEMA irudishe chama kwenye majimbo kuonesha kuwa kinaamini kweli sera ya majimbo. CHADEMA imekuwa ikiuza sera kuwa wakishika madaraka wataongoza nchi wa kuweka madaraka katika majimbo zaidi. Sasa kama hili kweli wanaamini ni jambo zuri basi waanze nalo kwenye chama. Kwanini chama kiko too centralized? Naamini CHADEMA kitoe madaraka makubwa kwa chama mikoani au kwa kuunganisha mikoa na hivyo kuwa na makao makuu ya chama ya Kanda ambayo yatashughulikia shughuli zote za chama katika ngazi hizo. Kama majimbo ni mazuri kwa uendeshaji wa serikali bila shaka ni mazuri kwa uendeshaji wa chama! Hii pia itasaidia kuondoa watu wanaotaka kwenda kufanya kazi makao makuu ya taifa! Wengine waende kwenye kanda huko!
  • e. Mfumo wa nidhamu ubadilishwe ili masuala ya nidhamu yashughulikiwe katika mfumo mmoja, unaoeleweka na ambao unafanya kazi kwa haraka, kwa uwazi, na kwa uhuru. Mfumo unaosubiri miaka au miezi kushughulikia migongano kwenye majimbo au ngazi fulani ni mfumo mbaya. Ni muhimu mfumo uwepo ambao mara tatizo linapojitokeza linashughulikiwa mara moja na kumalizwa siyo kuachwa kiporo wiki baada ya wiki miezi baada ya miezi na hata inakuwa miaka baada ya miaka. Huo ni mfumo mbaya.
  • f. Kurasimisha M4C kama taasisi ya chama. Sasa hivi M4C sijui ni kitu gani ndani ya chama. Niliandika hili wiki chache zilizopita kuwa mojawapo ya matatizo mengine ni hili la M4C kutokuwekwa katika utaratibu unaoleweka ambao utaondoa hisia ya kuwa M4C inaendesha na makao makuu tu na itaweka utaratibu wa wazi kwa wanachama na mashabiki wa michango inayopatikana na inavyotumika. M4C ni lazima iwekwe kama taasisi ya chama, uongozi wake utambulishwe rasmi ukiwa unajulikana majukumu yake na mipaka yake. Isije CHADEMA ikajikuta imetengeneza chama ndani ya chama.

CHADEMA ikiamua kujipanga vizuri na kufanya maamuzi ya haraka, thabiti na kuharakisha maamuzi hayo – yakiwemo ya mabadiliko ya Katiba inaweza kujipa nafasi ya kushinda uchaguzi mkuu ujao. Sasa hivi baada ya kuupoteza mwaka 2012 sioni ni jinsi gani bila mabadiliko ya ndani ya chama tena makini, ya makusudi na ya haraka CHADEMA itaweza kushinda uchaguzi mkuu ujao. Na hili ni la kwanza hatujagusa suala la mabadiliko ya sera na maono.

No comments:

 
 
Blogger Templates