Social Icons

Monday, 10 March 2014

HOFU YATANDA BUNGE LA KATIBA KUVUNJIKA

Dodoma. Mjadala wa namna ya kuamua Rasimu ya Katiba umezua hofu ya Bunge Maalumu la Katiba kuvunjika.

Bunge hilo limeangia siku ya 21 kati ya 70 likiwa katika mjadala wa kupitisha kanuni, huku kukiwa na mabishano kuhusu namna ya kupitisha ibara.  Hadi sasa Bunge hilo limeshapitisha kanuni 85 za uendeshaji wa chombo hicho, ispokuwa mbili tu, ikiwamo ya upigaji wa kura katika kupitisha vipengele mbalimbali katika rasimu, ambayo inaonekana kusababisha mgawanyiko mkubwa.

Hali ya kutokubaliana katika masuala kadhaa ilisababisha baadhi ya wajumbe kumtaka Mwenyekiti wa Muda, Pandu Ameir Kificho aeleze iwapo Bunge hilo lingeendelea au la kutokana na utata wa kisheria na kikanuni kuhusu ibara na sura zitakazokataliwa na wajumbe kwa kura.

Akichangia mjadala wa kanuni mjumbe, Dk. Francis Michael aliitaka Kamati ya Mashauriano kuhusu vipengele vyenye ushindani ikae chini na kutoa ufumbuzi kuhusu utata huo.

“Inabidi tuwe na uamuzi, hapa tunataka Katiba Mpya au hapana. Hapa tunatumia fedha za walipa kodi. Kuna hoja ambazo zinaonyesha kabisa kuwa zikifika hapa zitagonga ukuta,” alisisitiza.

Dk. Michael alipendekeza wanasheria na wakuu wa Serikali wa pande zote za Muungano kutafuta suluhisho mapema.

 “Ni afadhali tuamue kabla hatujaendelea mbele kwa sababu hakuna mantiki ya kuendelea kukaa hapa wakati tunajua kuna hoja ambazo zinaweza zisifikie ufumbuzi,” alisisitiza Dk. Michael.

“Kwa hiyo mheshimiwa mwenyekiti kama kichwa hakikupata solution (suluhisho) huko mbeleni sijui tunakwenda kujadili vipi hii rasimu… hapa ni mahali pa kuangalia sana,” alisisitiza Hassan.

Naye Christopher Ole Sendeka alisema suala hilo la kupitisha ibara kwa kuzingatia wingi wa theluthi mbili za kura halihitaji ushabiki wowote ndani ya Bunge. Kanuni inataka iwapo ibara haikupitishwa kwa theluthi mbili ya wajumbe, ipelekwe katika Kamati ya Mashauriano ili kukarabatiwa na kurudishwa na baadaye kupigiwa kura kwa mara ya pili.

Iwapo wajumbe watapiga kura kwa mara ya pili na bado ikashindwa kupita, ibara hiyo itaondolewa kabisa. “Mnajadiliana iwapo Tanzania ni Shirikisho ama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inapigwa kura mnakosa theluthi mbili Zanzibar na Tanzania Bara, mtatakoje hapo?” Alihoji.

Kutokana na mkanganyiko huo, Sendeka alipendekeza wanasheria waliobobea wakae na Serikali na kukubaliana ikitokea hali hiyo, njia ipi itatumika kulinusuru Bunge lisivunjike. Pauline Gekul alisema kanuni inayozungumzia wingi wa kura katika upitishaji wa ibara imewaacha hewani kuhusu nini kitatokea kama ibara zitashindikana kupitishwa. Gekul alipendekeza kuwa badala ya ibara au sura ambayo haikupitishwa kuondolewa, alishauri suala hilo lipelekwe kwa wananchi kuamuliwa kwa wingi wa kura badala ya kuziondoa.

Naye Ummy Mwalimu alipendekeza wakati wa kupitisha ibara katika hatua ya kamati, suala hilo lipitishwe kwa kuzingatia uwiano wa zaidi ya asilimia 50 kutoka pande zote za Muungano badala ya theluthi mbili.

Chanzo:- Mwananchi

No comments:

 
 
Blogger Templates