Mahakama ya Misri imewahukumu kifo wafuasi 528 wa rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Mursi. Wafuasi hao walikutwa na hatia ya kuanzisha ghasia na kuvamia majengo ya polisi katika mji wa Kusini mwa Minya.
Wote waliohukumiwa kifo katika kesi hii ambayo ni kubwa kabisa katika historia ya Misri, wana haki ya kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Kati ya hao waliohukumiwa 153 wako kizuizini huku wengine wakiwa bado wanaendelea kutafutwa.
Kesi hiyo ilianza siku ya Jumamosi na washtakiwa 1200 kutoka chama kilichopigwa marufuku cha Udugu wa Kiislamu walisimamishwa kizimbani.
Hata hivyo jaji aliyotoa hukumu hiyo Saeed Youssef aliwaachia huru washtakiwa wengine 17.
Mahakama hiyo aidha iliwagawanya washtakiwa katika makundi mawili, hukumu ya kundi la pili la washtakiwa 700 inatarajiwa kutolewa hapo kesho.
Kulingana na gazeti linalomilikiwa na serikali la Al- Ahram watu hao 528 waliohukumiwa kifo walipatikana na hatia ya mauaji dhidi ya polisi, na kuvamia kituo cha polisi pamoja na kudhibiti silaha za polisi nchini humo.
Baada ya polisi kuvunja makambi mawili ya upinzani Agosti 14, mwaka uliopita watu hao pia walishtakiwa kwa kuvamia watu na mali ya umma kusini mwa mji wa Minya.
Rais wa zamani Misri anakabiliwa na mashtaka
Morsi, rais wa kwanza wa Misri aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia alipinduliwa madarakani na jeshi la nchi hiyo mwezi Julai baada ya maandamano makubwa dhidi ya utawala wake wa takriban mwaka mmoja.
Maelfu ya wafuasi wake waliuwawa na wengine kukamatwa wakati wa operesheni kali iliofanywa na serikali dhidi ya upinzani.
Mwezi Desemba mwaka jana serikali inayoungwa mkono na jeshi ililiweka kundi la Udugu wa Kiislamu katika orodha ya makundi ya kigaidi.
Kwengineko shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limesema takriban watu 1400 waliuwawa katika ghasia za Misri huku wengine zaidi ya 1000 wakitiwa nguvuni.
Rais wa zamani Mohammed Mursi kwa sasa anakabiliwa na mashtaka katika kesi tatu tofauti, ikiwemo kuchochea mauaji ya waandamanaji nje ya ikulu ya rais wakati alipokuwa madarakani.
Mursi aliondolewa madarakani baada ya madai ya kuchukua madaraka kwanguvu na kuyumbisha uchumi dhaifu wa nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment