Social Icons

Wednesday, 12 March 2014

Wakuu wa jeshi wa zamani Rwanda wahukumiwa kifungo

Jenerali Kayumba Nyamwasa

Jenerali Kayumba Nyamwasa

Mahakama kuu ya kijeshi nchini Rwanda imetoa hukumu ya kifungo cha miaka 24 jela dhidi ya mkuu wa zamani wa majeshi ya nchi hiyo Jenerali Faustin Kayumba Nyamwasa na kuvuliwa cheo chake.

Wakati huo huo washirika wake watatu wamepewa hukumu ya kifungo cha miaka kati ya 20 na 24 jela.

Mahakama hiyo imewakuta na hatia ya mashtaka sita yakiwemo uhaini, kuhatarisha usalama wa taifa na kuunda kundi la uhalifu.

Kesi ya washirika hao wa zamani wa Rais wa Rwanda Paul Kagame iliendeshwa wakiwa uhamishoni.

Wanapinga mashtaka hayo wakisema yamechochewa kisiasa.Kutoka Kigali mwandishi wetu Yves Bucyana ametuma taarifa ifuatayo."

Jaji wa mahakama hiyo amethibitisha hoja ya mwendesha mashtaka kuwa ushahidi wa mashtaka hayo unapatikana katika mazungumzo waliyofanya na vituo vya redio vya kimataifa pamoja na matangazo mbali mbali waliyotoa kupitia vyombo vya habari.

Alisema yote yalilenga kupotosha wananchi, kuwahamasisha kugoma dhidi ya utawala na kuchochea mgawanyiko miongoni mwa Wanyarwanda kwa misingi ya ukabila na pia kumkashifu Rais wa Jamuhuri.

Pia alisema waliamua kuunda kundi la uhalifu na kutangaza hadharani kuwa mstari wa mbele kupinga utawala wa Rwanda na kuwa tayari kushirikiana na yeyote atakayewaunga mkono katika vita vya kuung'oa utawala wa Rais Kagame.

Pamoja na hayo Jenerali Faustin Kayumba na Meja Theogene Rudasingwa wamekutwa na hatia ya kutoroka jeshi na kuhukumiwa kifungo cha miaka 24 jela pamoja na kuvuliwa vyeo vyao vya kijeshi.

Washtakiwa wengine Gerald Gahima na Patrick Karegeya wamepewa kifungo cha miaka 20 jela.

Awali mwendesha mashtaka alikuwa amependekeza hukumu ya kifungo cha miaka kati ya 30 na 35.

Kesi hii ilianza tarehe Januari 3 mwaka huu bila washtakiwa kuwepo mahakamani kwa kuwa wanaishi uhamishoni.

Hapo awali washirika hawa wa zamani wa Rais Kagame walianzisha vuguvugu la kisiasa la Rwanda National Congres, wakisema lengo lao ni kuleta demokrasia, haki na uhuru kwa wananchi wa Rwanda.

Pia wanapinga mashtaka hayo wakisema yamechochewa kisiasa.

Chanzo:- bbc

No comments:

 
 
Blogger Templates