Social Icons

Sunday, 2 March 2014

WAPIGANAJI SUDAN KUSINI WAWAUA WAGONJWA HOSPITALINI

Wapiganaji Sudan Kusini wawaua wagonjwa hospitalini

Shirika la madaktari wasio na mipaka -MSF-limesema wagonjwa Sudan Kusini waliolazwa hospitalini waliuawa kwa kupigwa risasi vitandani mwao na vituo vya kutoa huduma za matibabu vimeporwa au kuchomwa

Shirika hilo la Medecins sans Frontieres MSF limesema leo kuwa wapiganaji wa pande mbili zinazozozana nchini humo zimekosa kuonyesha heshima na utu kwa wafanyikazi katika sekta ya afya na kutokana na kuongezeka kwa ghasia zinazowalenga, imekuwa vigumu kufanya kazi nchini humo.

Wafanyakazi wa MSF waligundua kiasi ya miili 14 katika hospitali moja katika mji unaozozaniwa na pande hizo wa Malakal mwishoni mwa juma lililopita.Baadhi ya miili hiyo ilipatikana na majeraha ya risasi ikiwa imelala vitandani.

Waasi watiifu kwa aliyekuwa makamu wa Rais wa nchi hiyo Riek Machar wamekuwa wakipambana na jeshi la serikali kuudhibiti mji huo wa Malakal wenye utajiri mkubwa wa mafuta.

MSF yatafakari kusitisha huduma Sudan Kusini

Mkuu wa shirika hilo la kutoa misaada ya huduma za matibabu Raphael Gergou amesema vituo vyao katika miji ya Leer na Bentiu vimeporwa na kuharibiwa kabisa na kuongeza kuwa shirika hilo halingependa kuondoka Sudan Kusini lakini lazima izingatie usalama wa wafanyikazi wake.

Msafara wa magari ya shirika la madaktari wasio na mipaka MSF

Msafara wa magari ya shirika la madaktari wasio na mipaka MSF

Gergou amesema itakuwa vigumu kuendelea kuwepo hadi mzozo huo utakapofikia kikomo kwani hawana hakikisho kuwa wafanyikazi wao na wagonjwa wanaowahudumia hawatalengwa na wapiganaji wa pande zote mbili ambao wameonyesha bayana kuwa hawaheshimu mchango wa wahudumu wa afya.

Mwishoni mwa mwezi uliopita,maelfu ya raia waliutoroka mji wa Leer baada ya mapigano kuzuka katika mji huo ambao ndiko alikozaliwa Machar.MSF ambayo imekuwa ikihudumu katika mji huo kwa miaka 25 iliwaondoa wafanyikazi wake huku wahudumu wengine 240 wakijificha vichakani.

Wiki hii wafanyakazi hao walirejea katika mji huo wa Leer na kupata hospitali yao ambayo huwahudumia watu laki tatu ikiwa imeharibiwa.MSF imesema huenda wakalazimika kuwakata viungo baadhi ya wagonjwa wao kutokana na kutopata matibabu yanayohitajika baada ya kuporwa kwa vituo vyao na hivyo kusababisha vidonda kuoza.

Kenya yatuma wanajeshi 300 zaidi

Maelfu ya watu wameuawa katika mzozo huo wa Sudan Kusini uliozuka katikati ya mwezi Desemba na takriban raia laki tisa wameachwa bila makaazi kufuatia makabiliano makali kati ya majeshi ya Rais Salva Kiir na waasi.

Wanajeshi wa Sudan Kusini wakishika doria mjini Juba

Wanajeshi wa Sudan Kusini wakishika doria mjini Juba

Baraza la kitaifa la usalama nchini Kenya NSC ambalo linaongozwa na Rais Uhuru Kenyatta limezitaka pande zote mbili katika mzozo huo kurejea katika mchakato wa kutafuta amani na kuonya kuwa hali itazidi kuwa mbaya zaidi iwapo hawatafanya hivyo.

Baraza hilo la kiusalama limeonya kuongezeka kwa mzozo wa kibinadamu ikiwemo ongezeko la wakimbizi wanaotoroka mapigano Sudan Kusini na kutorokea Kenya.

Kenya imetangaza itatuma wanajeshi 300 zaidi kujiunga na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo na kufikisha idadi ya wanajeshi wa Kenya Sudan Kusini kuwa 1,000

Mwandishi:Caro Robi/Afp /ap

Chanzo: Dw.de


No comments:

 
 
Blogger Templates