Social Icons

Tuesday, 15 April 2014

Hali inatisha Ukraine: Muda wa kuweka chini Silaha umemalizika

Kitisho cha kuripuka vita vya wenyewe kwa wenyewe kinazidi kukua nchini Ukraine.Urusi inatuhumiwa na nchi za magharibi kuwakusanya maelfu ya wanajeshi karibu na mpaka wa mashariki wa nchi hiyo

Machafuko katika mkoa wa Sloviansk-mashariki ya Ukraine-waasi wanaoelemea upande wa Urusi wamevamia kituo cha polisi

Muda waliopewa wanaharakati wanaoelemea upande wa Urusi na serikali ya mjini Kiev waweke chini silaha umeshamalizika."Hakuna atakaesalim amri" anasema Alexei Chmulenko,ambae ni msemaji wa wanaharakati hao katika mkoa wa Luhansk.Akizungumza na shirika la habari la Urusi-Interfax,Chmulenko amesema idadi ya wanaharakati inazidi kuongezeka na majengo zaidi kuvamiwa katika eneo hilo la mashariki.Rais wa mpito wa Ukraine Oleksandr Turchynov aliwaonya wanaharakati hao ,jeshi litaingilia kati ikiwa hawatoweka chini silaha zao hadi saa nne za asubuhi .

Hali imezidi kuwa mbaya tangu mwishoni mwa wiki pale watu waliokuwa na silaha walipovivamia vituo kadhaa vya polisi na majengo ya serikali.Bendera za Urusi zinapepea .Shule na ofisi za serikali zimefungwa.Rais wa mpito Oleksandr Turchynov amesema opereshini dhidi ya magaidi zitaanza wakati wowote kutoka sasa.

Jana nchi za magharibi katika baraza la usalama la Umoja wa mataifa zimeilaumu Urusi kukusanya wanajeshi kati ya 35 elfu na 40 000 karibu na mpaka wa Ukraine kwa lengo la kulivamia eneo la mashariki,kama ilioyolivamia eneo la Crimea..

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Serguei Lavrov amekanusha dhana hizo na kukosoa kile alichokiita "unafiki wa nchi za magharibi" kuelekea matukio ya Ukraine.

Ujerumani yaisihi Urusi isiyape kisogo mazungumzo ya Geneva

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na mwenzake wa China Wang Yi PK mjini Beijing

Akiwa ziarani mjini Beijing waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameitolea wito Urusi isiupe kisogo mkutano wa pande nne uliopangwa kuitishwa alkhamisi hii mjini Geneva:

"Bado nnaamini pande zote zi medhamiria kuona mkutano huo unafanyika;Sio tu kwasababu ya juhudi zilizohitajika kuandaa mkutano huo,bali zaidi ni kwasababu ya hali namna ilivyo.Pande zote zinazohusika zinabidi kukutana ili kuepusha balaa.Na nnataraji Moscow pia ina maoni sawa na haya."Amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier.

Ukraine haipingi Kura ya maoni

Rais wa mpito wa Ukraine Oleksandr Turchynov

Hofu kama hizo zimeelezewa pia na mwakilishi mkuu wa siasa ya nje wa Umoja wa Ulaya bibi Catherine Ashton aliyeitolea wito Urusi iunge mkono juhudi za Umoja wa Ulaya kuiona Ukraine ikisailia nchi moja.Na hivi punde rais wa mpito Oleksandr Turchynov ameliambia bunge mjini Kiev Ukraine haipingi fikra ya kuitishwa kura ya maoni kuhusu mustakbal wa nchi hiyo,wakati mmoja na uchaguzi wa raids utakapoitishwa May 25 ijayo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/dpa/Reuters/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Chanzo:- Dw.de

No comments:

 
 
Blogger Templates