Rais wa Urusi Vladimir Putin na rais wa Marekani Barack Obama wamefanya mazungumzo kwa njia ya simu .
Masuala mbali mbali kuhusu mzozo wa Ukraine, hususan upinzani wa wanaharakati wa kusini mashariki mwa taifa
hilo dhidi ya sera za serikali ya sasa ya Kiev yamejadiliwa baina ya viongozi hao.
Afisa wa ngazi ya juu wa ikulu ya White house amesema mazungumzo hayo yamefanyika kwa ombi la Urusi na yalikuwa ya kirafiki na ya moja kwa moja .
Ikulu ya White House inasema Rais Obama amesema wazi kuwa Marekani ingetaka mzozo kati ya Urusi na Ukraine usuluhishwe kwa njia ya kidiplomasia.
Hatahivyo amesikitika kuwa vitendo vya Urusi katika siku za hivi karibuni havionekani kuzingatia hilo.
Katika mazungumzo hayo Rais wa Urusi Vladmir Putin amesisitiza kuwa maandamano yanayofanyika kusini mashariki mwa Ukraine ni kutokana na nchi hiyo kutojali maslahi ya Urusi na raia wanaozungumza Kirusi.
Amemuomba Rais Obama kutumia raslimali za Marekani kuzuia umwagikaji damu.
Marekani na Urusi zimelaumiana kwa kuingilia kati maswala ya Ukraine huku Urusi ikilalamika kuhusu ziara ya mkuu wa idara ya ujasusi ya Marekani mjini Kiev.
Mazungumzo hayo yameonyesha wazi jinsi misimamo ya Marekani na Urusi kuhusu hali ya baadaye ya Ukraine ilivyotofautiana
Wakati huohuo, Umoja wa Ulaya na Marekani zinapangia kuiongzezea vikwazo Urusi .
Mawaziri wa maswala ya kigeni wa Ulaya jana waliafikiana kuongeza idadi ya watu watakao wekewa vikwazo vya kiuchumi na usafiri .
Mawaziri hao waliokutana huko Luxembourg walikubaliana kuipa Ukraine msaada ya dola bilioni moja nukta nne mbali na kuiondolea taifa hilo vikwazo vya kodi kwa muda katika muungano huo.
Kauli hiyo inawadia huku taharuki ikitanda katika miji ya mashariki mwa Ukraine ambapo makundi ya waandamanaji wanaunga mkono Urusi wakivamia makao makuu ya serikali ya Kiev na kuziteketeza moto.
Marekani ilisema kuwa ndege ya kivita ya Urusi ilipaa karibu sana na manuari ya kivita ya Marekani katika bahari ya Black sea.
Huko Washington, mkutano baina ya waziri wa maswala ya kiuchumi wa Marekani Jacob Lew na mwenzake kutoka Ukraine , Oleksandr Shlapak uliafiki na kutia sahihi mkopo wa dola bilioni moja .
Awali Kaimu rais wa Ukraine Olexander Turchynov aliwaonya waasi kuwa watakabiliwa na vikosi vya jeshi kutoka Kiev huku akiiomba Umoja wa mataifa kuingilia kati katika operesheni hiyo.
Chanzo:- bbc
No comments:
Post a Comment