Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewakumbuka wayahudi walioangamizwa katika mauaji ya Holocaust na mashambulizi ya kigaidi, katika siku ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu ya mashariki ya Kati.
Papa Francis alitoka kwenye ratiba yake aliyopangiwa, na kukitembelea kituo cha kumbukumbu ya wahanga wa ugaidi nchini Israel, akiipa nchi hiyo usikivu kamili, siku moja baada ya kueleza kuwa anashikamana kikamilifu na Wapalestina katika harakati zao za kupata taifa lao huru.
Katika kituo cha kumbukumbu ya mauaji ya Wayahudi cha Yad Vashem, Francis alifanya sala mbele ya chumba yalikohifadhiwa majivu ya wahanga, na kuweka shada la maua ya rangi nyeupe na njano katika ukumbi wa kumbukumbu.
'Kamwe isitokee tena'
Na baadae alivibusu viganja vya manusura sita mmoja baada ya mwingine, huku akisikiliza simulizi zao na za wapendwa wao waliouawa na wanazi wakati wa vita vikuu vy apili vya dunia.
"Kamwe isitokee tena, eeh Mungu, kamwe isitokee tena," alisema Papa Francis na kuongeza kuwa wako pale wakijiskia aibu kutokana na mwanadamu alichoweza kuwafanyia wanaadamu wenzake.
Mapema, Papa Francis alifanyia maombi katika ukuta wa magharibi mwa Jerusalem, ambao ni eneo takatifu zaidi wanakoweza kusalia wayahudi, na kuacha kikaratasi chenye sala ya "baba yetu" ilioandikwa katika lugha yake ya asili ya kihispania, katika moja ya nyufa zilizopo kati ya mawe ya ukuta huo.
Baadaye alimkumbatia rafiki yake Abraham Skorka, Padri wa Kiyahudi wa Argentina, na kiongozi wa jumuiya ya Waislamu wa Argentina Omar Abboud, ambao wote walikuwa katika ujumbe wake rasmi wa ziara hiyo kama ishara ya urafiki baina ya dini zote.
Marais Israel, Palestina kuombea amani Vatican
Ziara ya Papa Francis imeainishwa na mwaliko wa ghafla kwa marais wa Palestina na Israel kwenda mjini Vatican mwezi ujao kwa lengo la kuombea amani. Viongozi hao wote waliukubali mwaliko, na papa Francis alitarajiwa kukutana na rais wa Israel anaemaliza muda wake Shimon Perez baadae leo.
Papa Francis alianza siku ya leo kwa kuvua viatu vyake na kuingia katika msikiti wa al Aqsa, ambao ndiyo eneo la tatu kwa utakatifu katika Uislamu, inakoaminika kuwa Mtume Muhammad alipandia kwenda mbinguni.
Akizungumza na Mufti mkuu wa jiji la Jerusalemu na viongozi wengine wa Waislamu, papa Francis aliwataja Waislamu si tu kama marafiki wapendwa, bali kama ndugu wapendwa. Papa Francis anatajiwa kurejea mjini Rome kabla ya saa sita za usiku.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,afpe,dpae
Mhariri: Saum Yusuf
No comments:
Post a Comment