Waziri mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu ameapa kuendeleza kampeni ya kijeshi dhidi ya wapiganaji wa Hamas katika ukanda wa Gaza, ambayo tayari imeshagharimu maisha wa Wapalestina 43 na kuwajeruhi zaidi ya 370.
Ofisi ya waziri mkuu Netanyahu ilimnukuu akisema kuwa wameamua kuimarisha mashambulizi dhidi ya Hamas na makundi mengine ya kigaidi mjini Gaza, na kuongeza kuwa jeshi lake limejiandaa kwa hali yoyote itakayojitokeza. Waziri mkuu huyo anasema usalama wa raia wa Israel ndiyo kitu cha kwanza, na kwa hivyo Hamas italipa gharama kubwa kwa kuwafyetulia maroketi raia hao.
Roketi zaenda umbali mrefu
Siku ya Jumatano ndiyo ya pili ya mashambulizi hayo yaliyopewa jina la "Operesheni kinga", ambapo ndege za kivita za Israel zimeyashambulia maeneo 550 mjini Gaza, huku Hamas akijibu mashambulizi kwa kufyatua maroketi 165, baadhi yake yakianguka katika miji ya Jerumani na Tel Aviv, na mengine hadi mji wa Hadera, uliyoko umbali wa kilomita 116 kaskzini mwa Tel Aviv.
Maroketi mawili ya masafa marefu yaliufikia mji wa Haifa, ulioko umbali wa kilomita 165 kaskzini mwa Gaza, ambao ndiyo umbali mkubwa zaidi kufikiwa na kombora lililofyetuliwa kutoka Gaza. Msemaji wa jeshi la polisi nchini Israel Mickey Rosenfeld alithibitisha kuanguka kwa makombora kadhaa katika miji mbalimbali nchini Israel lakini ameongeza kuwa hayajafanya madhara yoyote bado, lakini akaongeza kuwa walikuwa wanajiandaa kwa lolote linaloweza kutokea.
Misri ilizitolea wito pande mbili kusitisha uhasama na kuacha kuupandisha mgogoro huo, lakini haikuonyesha utayarifu wa kulushisha mgogoro huo. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Misri Badr Abdelatty, alisema kwa sasa hakuna upatanishi wowote unaofanywa, lakini akaongeza kuwa juhudi la kidiplomasia za Misri zinalenga kusitisha mara moja mashambulizi ya Israel na kuacha vurugu za pande zote.
Hamas yaapa kuendeleza mapambano
Afisa wa juu wa Hamas aliahidi kuwa wapiganaji hawatasalimu kufuatia mashambulizi ya Jumatano. Osman Hamdan alieko mjini Beirut, alisema hakuna mazunguzo ya kusitisha mapigano, na wala hakuna mawasiliano yoyote kwa sasa. Alisema Waisrael hawataki upatanishi bali wanataka Hamas isalimu amri.
Israel inasema mashambulizi yake ni ya kujibu mashambulizi ya roketi zaidi ya 100 yaliyofyetuliwa ndani ya nchi hiyo na Hamas na makundi mengine yaliyopo katika ukanda huo. Mapigano hayo ndiyo mabaya zaidi kati ya maadui hao wawili, tangu vita vya siku nane walivyopigana Novemba 2012.
Chanzo: dw.de
No comments:
Post a Comment