MIEZI michache ikiwa imebaki kabla ya mbio za kumrithi Rais Jakaya Kikwete kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanza rasmi, majina manne ya wanachama wa chama hicho yametajwa kuwa ndiyo yanayopendekezwa na vyombo vya Maadili pamoja na Ulinzi, Raia Mwema limeambiwa.
Gazeti hili limeambiwa kwamba kuna kikundi cha maveterani wa CCM ndani ya chama na Idara za Usalama wanaoandaa ripoti itakayopendekeza majina hayo kwa chama.
Majina yote manne ni ya mawaziri walio katika serikali ya Kikwete hivi sasa; na ukiondoa mmoja, wote wanatoka katika maeneo ambayo hayajawahi kutoa Rais wa Tanzania.
Mawaziri hao wametajwa kuwa ni Benard Membe (Mambo ya Nje), Samuel Sitta (Ushirikiano wa Afrika Mashariki), John Magufuli (Ujenzi) na Dk. Harrison Mwakyembe (Uchukuzi).
Raia Mwema limeambiwa kwamba Ikulu itapelekewa ripoti maalumu iliyotayarishwa kuhusu watu wote wanaotajwa kutaka kuwania nafasi hiyo na itaelezwa kwamba ili CCM ishinde kirahisi mmoja wa mawaziri hao wanne inabidi apewe nafasi.
“Ngoja nikwambie, mgombea mzuri kwa CCM katika uchaguzi ujao ni lazima awe anafahamika na wananchi na inatakiwa rekodi yake iwe inajulikana. Hatuwezi kupeleka mtu asiyejulikana.
“Hatuwezi pia kupeleka jina la mtu ambaye mnaanza kujitetea from day one. Hatuwezi kwenda kwenda kwenye uchaguzi with a defensive mentality ( tukiwa tumejiandaa kupokea mashambulizi). Tunatakiwa kushambulia kuanzia siku ya kwanza,” kilisema chanzo cha gazeti hili ambacho kiliwahi kutumikia TANU katika miaka ya 1970 na baadaye CCM na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Chanzo hicho kililiambia gazeti hili kwamba hata Kikwete mwenyewe anaunga mkono mgombea kutoka miongoni mwa mawaziri hao wanne.
“Hivi, kama CCM ikiamua kumchagua Magufuli kuwania urais unadhani wananchi watapata picha gani? Picha itakuwa kwamba chama sasa kimeamua kuwapa mtu ambaye anaweza kupambana na matatizo yanayowakabili,” kilisema chanzo hicho.
Raia Mwema limeelezwa kwamba Mwakyembe, Sitta na Magufuli wanatoka katika jamii zenye idadi kubwa ya watu ambao hawajahi kupata fursa ya kutoa rais na kugombea kwao kutahakikisha kura nyingi kutoka katika jamii zao.
Ingawa CCM kimekuwa, kwa muda mrefu, kikihubiri kuhusu siasa zisizo za dini, ukabila au ubaguzi wa aina yoyote, chaguzi za karibuni zimeonyesha kwamba vigezo hivyo vimekuwa vikianza kuchukua nafasi.
Gazeti hili limeambiwa kwamba ripoti hiyo kutoka katika vyombo vya kimaadili na dola itapelekwa moja kwa moja Ikulu au itapitia kwanza katika Kamati Ndogo ya Maadili ya chama inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula.
Duru za kisiasa ndani ya CCM na Ikulu zimedai kwamba hatua ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, kutangaza nia yake ya kuwania urais haikushtua vyombo kwa vile inaaminika hana dhamira ya dhati ya kuwania urais mwaka 2015.
“Anachofanya Makamba ni kujiandaa kwa ajili ya urais wa 2015. Atakuwa na umri wa miaka 50 wakati huo na kwa Tanzania labda huo ndiyo umri wa ujana unaosemwa.
“Vyovyote vile, atakayeshinda urais kwa CCM mwakani ni lazima atamchukulia Makamba serious. Pengine atampa nafasi nyeti ya uwaziri. Anachotaka ni kuwa King Maker ili yeye aje kuwa King baadaye,” gazeti hili limeambiwa.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu majina hayo ya wagombea, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema hashangazwi na majina hayo na akasema yanabebwa na uzoefu zaidi kuliko uwezo wa kutenda kazi.
Alisema yeyote kati ya hao wanne anaweza kutoa upinzani mkali kwa wapinzani; ingawa akasema inategemea na nini kitatokea katika kipindi cha kati ya sasa hadi mwakani.
“Mwaka mmoja ni muda mrefu sana kwenye siasa. Huwezi kujua nini kitatokea. Hata hivyo, Edward Lowassa pia ni mgombea mzuri tu kwa CCM.
“Inaonekana amejiandaa sana kuwania urais na inawezakana ameshajua udhaifu katika kambi ya upinzani na anaweza kutumia mbinu kuhakikisha anaua nguvu ya upinzani.
“Mwisho wa siku, ukakuta badala ya wapinzani kuzungumza namna ya kushinda uchaguzi, ukasikia wakawa wanatimuana timuana wenyewe kwa wenyewe,” alisema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage, alisema anaamini mawaziri hao wanne wote wanaweza kupeperusha vema bendera ya chama hicho.
Sitta kwa mfano, tumeona nguvu yake katika Bunge la Katiba. Yeye alichaguliwa kwa kishindo na alikubalika na wabunge wa pande zote; wale wa CCM na wa upinzani.
Imani hii kwa Sitta ambayo walionyesha wabunge wa upinzani na wale wa chama tawala ndiyo hiyo hiyo ambayo nadhani iko kwa wananchi. Wananchi wanamheshimu sana.
Magufuli na Mwakyembe wanafahamika kwa uchapakazi wao. Kila Mtanzania anafahamu nini wamefanya katika wizara ambazo waliwekwa. Membe naye anafanya vizuri katika wizara yake.
“Kwenye uwaziri wake tumetembelewa na marais wa nchi kubwa zote duniani na kwa kweli diplomasia yetu inaonekana kuanza kurejea mahali pake,” alisema.
Mbunge mwingine kijana kutoka CCM ambaye hata hivyo hakutaka kutaja jina lake, alisema Bunge la Katiba lina nafasi kubwa katika kuamua mgombea urais wa CCM ajaye.
Kama hili Bunge likifa na mwafaka ukashindikana, nafasi ya Sitta kuwa mgombea itakuwa finyu. Lakini, kama Katiba Mpya itapitishwa, na Sitta akiwa Spika wa Bunge la Katiba, itakuwa vigumu sana kumzuia akitaka urais. Tungoje tuone Bunge litaishaje, alisema Mbunge huyo kutoka mojawapo ya mikoa iliyo katikati ya Tanzania.
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/ni-membe-magufuli-mwakyembe-na-sitta#sthash.d2YRjWYb.dpuf
No comments:
Post a Comment