Social Icons

Friday 12 September 2014

Kashmiri: Ilikuwa tumpige Idd Amin mwaka 1972

WIKI iliyopita, Kanali Ameen Kashmiri, Mkuu wa Kwanza wa Idara inayofahamika kama Lojistiki na Uhandisi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) alieleza mambo mbalimbali kuhusu yeye na historia yake ndani ya Jeshi. Leo hii anaelezea matukio ya kukumbukwa kwake. EndeleaKanali Kashmiri

KATIKA ofisi zake za sasa zilizopo Upanga, jirani na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Kanali Kashmiri, anawaza anieleze nini kuhusu matukio ya kukumbukwa zaidi kwake ndani ya JWTZ.

Kuna mengine, kwa sababu za kiusalama, hataweza kuniambia. Tunakubaliana katika hilo. Halafu kuna mengine mengi anayoweza kuniambia. Lakini si makubwa sana.

Nampa fursa ya yeye kukumbusha. Natumia fursa hiyo kumtazama zaidi na kudadisi ofisi yake. Kiatu chake cha ngozi kimepigwa rangi vizuri kama ambavyo ungetaraji kuona kiatu cha askari.

Shati lake ni jeupe lisilo doa. Suruali yake ya rangi ya kaki imepigwa pasi katika staili ambayo vijana wa siku hizi wanaita ‘panga’. Namtania kuhusu suruali yake ilivyonyooka na ananiambia siku hizi hainyooki sana kama zamani wakati walipokuwa wakivaa kaptura kuanzia Jeshi la Mkoloni (KAR) na lile la Tanganyika huru yaani TR.

Ananieleza kwamba wakati huo wapo askari waliokuwa wakimwagia unga katika suruali zao ili zinyooke ipasavyo. Hata hivyo, namuhakikishia kwamba kwa siku ile niliyozungumza naye, sikuona mtu ambaye amenyoosha suruari yake na ikanyooka kama ya Kashmiri.

Tunacheka kwa pamoja. Sasa yu tayari kunieleza anayokumbuka.

“La kwanza ni tukio lililotokea baada ya Dikteta Iddi Amin kupindua serikali ya Rais Milton Obote wa Uganda. Unajua Obote na Mwalimu walikuwa marafiki sana na Nyerere alikuwa tayari kupeleka askari ili kusaidia kumrejesha Obote madarakani.

“Nikapewa maelekezo kwamba natakiwa niliandae Jeshi kwa ajili ya vita. Kimsingi, nilitakiwa kuwa ndiyo Kamanda wa Jeshi wakati wa vita hiyo kama ingetokea.

“Mara moja nikaanza kuandaa mazingira ya vita kwa kuchagua askari na vikosi. Mara moja nikaanza kupeleka magari ya kivita kwenye mpaka wa Tanzania na Uganda.

“Kwenye dunia hii, vita si jambo la siri sana. Ukianza tu kupeleka silaha mipakani, watu watajua tu lipo tatizo. Nadhani taarifa zilianza kuenea kwamba Tanzania inapeleka silaha kwenye mpaka wake na Uganda.

“Tukapewa taarifa ya baadhi ya nchi kwamba hawatakubaliana na vita hiyo. Kwa mfano, Uingereza walileta taarifa kabisa kwamba tusiishambulie Uganda. Kwamba kama tungeishambulia, basi wao wangeingia kusaidia Uganda.

“Sasa Uingereza ni Taifa kubwa na kama wangeingia kwenye ile vita, kazi ingekuwa kubwa sana. Hata hivyo, mimi niliendelea na mipango yangu kama kawaida maana sikuwa nimeelezwa vinginevyo.

“Tayari nilishaandaa mpango wa vita. Kimsingi, nilipanga kutumia mbinu ambazo alitumia Field Marshal Rommel kwenye Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Unaingia vitani kwa kasi na spidi ya kutisha ukitumia zaidi vifaa na askari wanafuata nyuma.

“Nilikuwa na imani kubwa kwamba kwa kutumia mbinu hiyo, ile vita tungeshinda. Lakini baadaye Amiri Jeshi Mkuu (Mwalimu) akaagiza kwamba tuache vita. Hatukuwa tumeungwa mkono na nchi nyingi na tungeifanya vita iwe ngumu kwetu.

“Nina matumaini kuwa kama vita ile ya mwaka 1972 ingepiganwa, tungeepusha kwenda vitani mwaka 1978 wakati wa Vita ya Kagera. Lakini ndiyo hivyo tena,” anasema Kashmiri.

Rommel anayezungumzwa na Kashmiri ni Erwin Johannes Rommel, Jenerali wa Jeshi la Ujerumani aliyekuwa akifahamika sana kwa jina la Mbweha wa Jangwani (Desert Fox) kutokana na umahiri wake wa kivita wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia alipoongoza majeshi ya Taifa lake Kaskazini mwa Afrika.

Staili yake iliyokuwa maarufu ilikuwa ni kutumia vifaa vya mwendo kama magari ya deraya na vifaru vinavyotumia kasi kubwa katika kufanya mashambulizi mazito na ya ghafla yanayofuatiwa baadaye na mashambulizi ya askari.

Ni staili hiyo ambayo Kashmiri alipanga kuitumia kwa ajili ya majeshi ya Iddi Amin Dada. Kwa bahati nzuri, ni vita ambayo Kashmiri hakuwahi kuipigana.

Kimsingi, katika utumishi wake wote wa jeshini, Kashmiri hajawahi kupigana vita ingawa alitumia sehemu kubwa kufanya mafunzo ya kivita.

Kuna tukio jingine la kihistoria katika JWTZ ambalo Kashmiri analikumbuka vizuri.

Mara baada ya mauaji ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Abeid Karume, Aprili 7, 1972, serikali iliamuru kukamatwa kwa baadhi ya maofisa wa JWTZ waliodaiwa kuhusika na tukio.

Mmoja wa waliotakiwa kukamatwa alikuwa ni Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa JWTZ, Kanali Ali Mahfoudh, ambaye wakati huo alikuwa akifahamika kwa ustadi wake kijeshi.

“Siku chache baada ya mauaji ya Mzee Karume, nilipewa kazi na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi, Mirisho Sarakikya, ya kumkamata Kanali Mahfoudh.

“Wakati huo, Ofisi za Makao Makuu ya JWTZ zilikuwa ziko pale Magogoni karibu na Ikulu. Siku ya kumkamata Mahfoudh nilikuwa ofisini kwangu na nikaambiwa yuko jirani na ofisi ya Makamu wa Rais (wakati huo Rashidi Kawawa) na nikatakiwa kuandaa mpango wa kumkamata.

“Agizo hilo nilipewa na Sarakikya mwenyewe ambaye wakati huo alikuwa ofisini kwa Kawawa. Hivyo, Mahfoudh akaambiwa aje ofisini kwangu amsubiri Sarakikya. Lengo ni kwamba nimkamate wakati huo.

“Wakati nikitafakari namna ya kumkamata pasipo kuwa na matatizo yoyote, ghafla nikaona mlango wangu wa kuingia ofisini ukifunguliwa na kisha mmoja wa wajumbe wa Baraza la Mapinduzi, Kanali Seif Bakari, akachungulia na kunisalimia; ‘Oh, Kashmiri, hujambo’?”. Baada ya kusema hayo akaondoka.

“Wakati huo, tayari nikawa nimepanga mipango ya kumkamata tayari. Ofisi ambayo ingefaa kwa tukio hilo ilikuwa ni ile ya Sarakikya kutokana na ukubwa wake. Nilipanga viti katika mfumo ambao Mahfoudh alikuwa akae katikati.

“Sasa wakati Seif Bakari alipokuja kuchungulia na kuona askari wako na mimi mule ofisini, walidhani kwamba niko kwenye kikao. Kumbe mambo yote yalikuwa yamepangwa. Hakukuwa na kikao wala nini isipokuwa askari waliokuwa wanasubiri tukio.

“Alipoingia Mahfoudh ofisini kwangu, akiwa na Bakari, alikuwa na bastola mbili kiunoni. Visu viwili pamoja na mkanda wa risasi kiunoni. Na unajua alikuwa pande la baba aliyepata mafunzo ya kijeshi Cuba ya wakati wa Fidel Castro wakati huo.

“Tulikaa ofisini kwa Sarakikya pale kwa zaidi ya nusu saa wakinieleza nini kinaendelea Zanzibar na tuhuma za mauaji anazozushiwa Mahfoudh. Nikawa namsikiliza kwa makini.

“Lakini wakati huo, Sarakikya akawa anapiga simu na kuuliza, vipi umeshamkamata? Nami namjibu bado. Najibu hivyo wakati Mahfoudh mwenyewe akiwa mbele yangu ila hakujua nilikuwa namjibu nani na kwa sababu gani.

“Mara walipomaliza wakaondoka. Askari niliowachagua wakawa hawajafanya kazi yao. Kwa bahati nzuri wakawa hawajaondoka kwenye maeneo ya Makao Makuu ya Jeshi.

“Walikuwa wametoka kwangu na wakaenda kwa aliyekuwa Kamisaa wa Siasa wa JWTZ, Kanali Simba nafikiri pia kwa ajili ya kumueleza nini kinaendelea Zanzibar.

“Nikawa mkali kwa wale askari nikawauliza, kwanini hamjamkamata  Mahfoudh? Mmoja wao akanijibu, afande, una Arrest Warrant (Hati ya Kumkamata Mtu)? Nikasema nyie vipi? Jeshini kuna arrest warrant? Hebu nendeni mkamkamate.

“Naona walikuwa wanamuogopa. Sifa zake kama komandoo na mwanajeshi mahiri zilikuwa zimewatisha. Kumbuka pia kwamba alikuwa na silaha pale alipo.

“Kwa bahati nzuri, akatokea askari mmoja miongoni mwao, nakumbuka jina lake lilikuwa Luteni Kyungu, akaamua kwenda kufanya kazi hiyo peke yake.

“Akaingia ofisini kwa Kanali Simba na kumwambia Mahfoudh; Kanali, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua ukamatwe kutokana na mauaji ya Karume. Uko chini ya ulinzi kuanzia sasa.

“Pasipo kutaraji, Mahfoudh akakubali bila ubishi. Yule Kyungu akaja naye ofisini kwangu. Nikamwambia Kanali, naomba uweke silaha zako chini na ujisalimishe. Akavua mkanda wake wa kiunoni, akatoa bastola zote, visu na risasi na kuziweka mezani.

“Nikamwambia, je, una ujumbe wowote ambao ungependa kumwandikia mkeo au familia yako. Kitu kama maelekezo hivi au maagizo. Kusema ukweli, sikujua nini ambacho kingemkuta na sikutaka askari mwenzangu apotee pasipo kuacha maelekezo kwa familia yake.

“Akasema ndiyo. Akaandika barua yake kwa mkewe kama alivyotaka. Alipomaliza akanikabidhi na nikamuahidi kwamba nitahakikisha familia yake inapata ile barua.

“Baadaye, nimekuja kubaini kwamba Seif Bakari alikuja naye huku kwa sababu alitaka akamatiwe huku. Walihofu kwamba kama angekamatwa angali Zanzibar, wangemuua. Hivyo kukamatiwa huku Bara ilikuwa ni nusura kwake. Na pengine ndiyo maana hakutaka kufanya fujo ya aina yoyote

“Alisubiri hadi alipokuja kuchukuliwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Polisi wakati huo akiitwa Sawaya. Hapo sasa ndipo nikamuarifu Sarakikya kwamba kazi imemalizika na sasa Mahfoudh yu mikononi mwa serikali.

“Nashukuru kwamba miaka michache baadaye, nilikuja kukutana na Mahfoudh mjini Maputo, Msumbiji kwenye mojawapo ya matukio ya kuwakutanisha Watanzania.

“Yeye alichukuliwa na aliyekuwa Rais wa Msumbiji, Samora Machel na akaja kuwa mshauri wake wa masuala ya kijeshi. Tulipokutana, tulichangamkiana kama kawaida na tulipata chakula cha jioni pamoja.

“Akaniambia kwamba hana kinyongo na mimi hata kidogo. Watu walikuwa wakimwambia maneno kwamba mbaya wake ni mimi kwa sababu ndiye niliyemkamata lakini yeye, kama askari, alikuwa akifahamu kwamba nilichofanya kilikuwa ni kutekeleza amri halali ya Jeshi. Hata angekuwa yeye, asingefanya tofauti na nilivyofanya mimi,” anasema.

Pamoja na ukubwa wa umri wake, Kashmiri anaonekana yuko fiti. Kwa watu wanaopenda kwenda kutazama michezo mbalimbali katika Viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam, mstaafu huyu ni miongoni mwa wanachama wa kudumu.

Mchezo aupendao ni Skwash aliojifunza wakati akiwa Uingereza. Unafanana na mchezo wa Tennis lakini tofauti kubwa ni kwamba wachezaji wa Skwash hushindana kwa kupiga mipira ukutani na kurudi.

“Kila wiki nacheza mchezo huu walau mara tatu. Kuna wenzangu hapa ambao tunapenda huu mchezo na huwa tunashindana. Nacheza muda mrefu na kwa kweli unanisaidia sana kiafya.

“Ukitaka kuishi maisha marefu hapa duniani na kuinjoi pia, ni muhimu ukajiwekea utaratibu wa kufanya mazoezi. Kama hufanyi mazoezi ni lazima tu utaumwa haswa ukifikia umri kama wangu,” anasema.

Mwishoni mwa mwaka huu, Kashmiri amepanga kwenda kupanda Mlima Kilimanjaro lakini kwa sehemu tu na kujipima, kwani mwakani, amedhamiria kupanda mlima huo hadi kileleni ikiwa sehemu ya kuadhimisha kutimiza miaka 80 tangu kuzaliwa kwake.

Miongoni mwa matukio ambayo hayafahamiki vizuri, ni namna ambavyo Sarakikya na Kashmiri waliondoka jeshini na kupewa majukumu ya kiraia.

Mwaka 1974, Mwalimu aliamua kumteua Sarakikya kuwa Waziri wa Vijana na Utamaduni katika mabadiliko ambayo pia yalimgusa Kashmiri ambaye alipewa jukumu jipya la kuanzisha Shirika la Maendeleo ya Sukari.

“Mimi mwenyewe nilikuwa nataka kustaafu kutoka jeshini kwa sababu zangu binafsi. Lakini Mwalimu alinizuia na kuniambia huwezi kuondoka jeshini namna hiyo. Utasababisha maswali mengi.

“Hivyo akanipa kazi ya kuanzisha Shirika la Taifa la Sukari. Mimi nilitaka kupumzika tu moja kwa moja ili nianze kufanya shughuli zangu binafsi. Ukitaka kufanya biashara ni muhimu ukaanza mapema kabla hujazeeka.

“Lakini baada ya Mwalimu kuniomba nikawa sina ujanja. Nikakubali na kubeba jukumu hilo. Nikaanza kutafuta wafanyakazi na ofisi. Nikafanya kazi kwa miaka miwili na kisha nikaruhusiwa sasa kufanya shughuli zangu binafsi.

“Ni wakati wangu ndipo tulipoanza mkakati wa kuwa na viwanda kule Kagera na Kilombero mkoani Morogoro. Mimi ndiye nilileta hili suala la out growers scheme (wakulima wanalima kwenye mashamba yao na kuja kuuza miwa kwa kampuni ya sukari).

“Wakati nilipostaafu, walikuja watu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kukagua kuhusu utendaji wa mashirika ya serikali na katika ripoti yao walikuja na taarifa moja muhimu sana.

“Walisema katika mashirika yote ya serikali yaliyokuwa chini ya Wizara ya Chakula na Kilimo, Shirika la Sukari ndilo lililoongoza kwa kuendeshwa vizuri kuliko mengine yote. Nakumbuka nafasi yangu alichukua Joseph Mungai na ni yeye ndiye aliyenipa taarifa.

 “Mungai aliniambia kwamba ingawa shirika analoliongoza ndilo limeshinda na sifa zinaenda kwake, yeye anaamini sifa zile zilitakiwa kuwa za kwangu maana ndiye niliyekuwa kiongozi kabla yake.

“Siku moja, nilikutana na aliyekuwa Mkuu wa Usalama wa Taifa, Dk. Hassy Kitine, mkoani Morogoro na akanieleza kwamba mafanikio ya Shirika la Sukari yalikuwa yanamfanya Mwalimu atake kuniteua kuwa Waziri. Tatizo langu lilikuwa kwamba mimi sikutaka tena kulipwa mshahara. Nilitaka tu kufanya mambo yangu,” anasema.

Wakati tukimaliza mazungumzo yetu, Kashmiri aliniuliza kama ningehitaji kunywa kinywaji chochote; chai, kahawa, soda au juisi… Nikamjibu kwamba kinywaji pekee ninachotaka kukionja ni Shandi, lakini hicho tutakunywa tukikutana tena Gymkhana kwenye Skwash.

Chanzo Raia Mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates