Bukombe. Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Bukombe mkoani Geita kimevamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za kivita pamoja na mabomu, na kuwaua askari polisi wawili na wengine wawili kujeruhiwa.
Habari zilizopatikana na kuthibishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo zinaeleza kuwa tukio hilo limetokea jana usiku kwenye kituo hicho kilichopo mjini Ushirombo.
“Ni kweli kituo hicho kimevamiwa na baadhi ya askari wameshambuliwa na kupata majeraha huku wawili wakipoteza maisha, lakini kwa sasa tunaendelea na uchunguzi wetu, tutatoa taarifa rasmi baadaye,”alisema Konyo.
Mbali na taarifa za Kamanda Konyo, baadhi ya taarifa ambazo hazijathibitishwa na polisi zinadai kuwa majambazi hao walivamia kituo hicho na kuiba bunduki 10 na mabomu ya machozi ambayo hayajajulikana idadi yake.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Bukombe, Dk Honoratha Rutatinisibwa alithibitisha kupokea miili ya watu wawili ya askari wa kituo hicho, huku wengine wawili wakiwa wamejeruhiwa vibaya na mabomu na risasi sehemu mbalimbali za miili yao.
Dk Rutatinisibwa aliwataja askari waliopoteza maisha kwa kupigwa na bomu ni Uria Mwandiga mwenye namba WP 7106 mwingine ni Dustan Kimati mwenye namba G 615 PC.
Aliwataja waliojeruhiwa ni David Ngupama Mwalugelwa (44) namba E 5831 APL na Mohamed Hassan Kilomo (25) namba H 627 PC.
Dk Rutatinisibwa alisema kati ya majeruhi hao, David Ngupama amekutwa na vipande vya bomu kichwani, huku akiwa amepasuliwa kichwa kwa bomu na maeneo mbalimbali ya mwili wake yakiwa na majeraha makubwa.
Alisema Mohamed Hassan amejeruhiwa kwa kupigwa risasi moja kifuani na mikononi. Majeruhi hao na miili ya askari waliofariki dunia ilifikishwa hospitali hapo saa kumi alfajiri.
Wakati huohuo mwandishi Ibrahim Yamola anaripoti kuwa Kamishina wa Polisi Operesheni na Mafunzo, Paulo Chagonja akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana alisema majambaza yanayodhaniwa kuwa zaidi ya kumi walitumia uhalifu huo kwa vifaa vya kivita.
“Waliwashambulia askari waliokuwapo kituoni hapo saa 6 usiku kwa kuwarushia bomu la kutupwa kwa mkono ambalo liliweza kuwaua askari Polisi wawili na wengine wawili kujeruhiwa,” alisema Chagonja na kuongeza: “Katika tukio hilo, majambazi hayo yalifanikiwa kuchukua baadhi ya silaha zilizokuwepo kituoni hapo, ambazo idadi yake bado tunaifuatilia kwani hii ni taarifa ya awali tu.”
Kamishna Changonja alisema ,”Tunatoa wito kwa wananchi kutulia na kuondoa hofu badala yake wananchi wenye taarifa muhimu zitakazosaidia kuwakamata wahalifu hao kwa gharama na nguvu zozote watupatie ili tuweze kuzifanyia kazi haraka.
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment