Ukraine imedai kuwa Urusi imeanzisha kile ilichookita ''vita vikubwa, ambavyo Ulaya haijawahi kuvishuhudia tangu kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.''
Matamshi hayo yametolewa wakati ambapo waasi wa Ukraine, wamechukua udhibiti wa uwanja wa ndege muhimu na kuwalazimisha wanajeshi wa serikali ya Ukraine kukimbia. Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Valeriy Geletey, ameishutumu Urusi kwa kuanzisha vita hivyo, ambavyo vinaweza kusababisha mauaji ya maelfu ya watu. Akizungumza kabla ya mkutano na waasi baadaye wiki hii, Geletey amesema Urusi iko nyuma ya mashambulizi yanayofanywa na waasi wanaoiunga mkono Urusi kwenye miji ya mashariki ya Donetsk na Luhansk.
Mazungumzo ya awali kati ya maafisa wa Ukraine na waasi yameanza jana Jumatatu. Katika ujumbe wake alioutuma kwenye mtandao wa mawasiliano ya kijamii wa Facebook, Geletey ameapa kuwa nchi yake itajibu mashambulizi dhidi ya Urusi, ambayo inajaribu siyo tu kunyakua maeneo yanayodhibitiwa na waasi, lakini pia inazidi kusonga mbele kuingia kwenye maeneo mengine ya Ukraine.
Waasi hao wameudhibiti uwanja wa ndege wa Luhansk kutoka kwa wanajeshi wa serikali hapo jana. Hata hivyo, Rais wa Urusi, Vladmir Putin amepuuzia madai kwamba wanajeshi wake wanawasaidia waasi na amewalaumu viongozi wa Ukraine kwa kuhusika na mzozo huo. Amesema, ''operesheni za waasi zilisababishwa na ukweli kwamba wanajeshi wa Ukraine walifanikiwa kuizingira miji yote na kushambulia moja kwa moja kwenye makaazi ya watu. Kwa bahati mbaya suala hili linapuuzwa na mataifa wa Ulaya.''
Putin aulaumu Umoja wa Ulaya
Rais Putin pia ameulaumu Umoja wa Ulaya ambao unafikiria kuweka vikwazo vipya dhidi ya Urusi, kwa kupuuzia suala la vikosi vya Ukraine kuwalenga moja kwa moja raia katika mzozo uliosababisha mauaji ya zaidi ya watu 2,600 tangu ulipozuka katikati ya mwezi Aprili mwaka huu.
Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Federica Mogherin, leo ameliambia Bunge la Ulaya kuwa serikali za Umoja wa Ulaya zitachukua maamuzi ya kuweka vikwazo vipya dhidi ya Urusi, ifikapo siku ya Ijumaa.
Jana, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Anders Fogh Rasmussen alisema kuwa jumuiya hiyo inazingatia kuongeza majeshi yake katika eneo la Ulaya ya Mashariki, ili kuyasaidia mataifa wanachama. Ingawa Ukraine siyo mwanachama wa NATO, mataifa jirani ya Estonia, Latvia na Lithuania ni wanachama.
Ama kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov amesema leo kuwa hatua ya Ukraine kutaka kujiunga na NATO, ina lengo la kudhoofisha juhudi za kumaliza vita vya mashariki mwa Ukraine.
Rais wa Marekani, Barack Obama na viongozi wa NATO watahudhuria mkutano utakaofanyika siku ya Alhamisi kwa lengo la kuujadili mzozo wa Ukraine.
Chanzo Dw.de
No comments:
Post a Comment