Dodoma. Kamati mbalimbali za Bunge Maalum la Katiba zimeendelea kuwasilisha taarifa zake leo huku suala la ukomo wa mbunge na suala la wananchi kumuwajibisha mbunge wao anaposhindwa kazi likizua mvutano.
Baadhi ya wajumbe hao katika kamati zao wameunga mkono pendekezo hilo katika Rasimu ya Katiba huku wengine hasa maoni ya wengi wakipinga kuwepo kwa ibara hiyo na kutaka iondolewe.
Akiwasilisha maoni ya Kamati namba mbili bungeni mjini Dodoma, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Shamsi Vuai Nahodha, alisema wajumbe walio wengi katika kamati yake wametaka kuondolewa pendekezo la kuwepo kwa ukomo wa mbunge kugombea nafasi hiyo, ili kutoa nafasi kwa wananchi kuamua.
“Kamati iliona pia bora ifute ibara ndogo ya 2(a) inayohusu ukomo wa kugombea ubunge baada ya kutumikia kwa vipindi vitatu, kamati inaona ni vyema suala hili liamuliwe na wananchi wenyewe,” alisema Vuai.
Hatahivyo, wajumbe walio wachache kupitia kamati hiyo hiyo ya namba mbili, wametaka Ibara hiyo iendelee kubaki kama ilivyopendekezwa na rasimu.
Akisoma maoni ya wachache, mjumbe wa kamati namba mbili, Elizabeth Minde alisema: “Wananchi lazima wapewe uwezo wa kumdhibiti mbunge wao iwapo amekiuka utaratibu kwani kusubiri hadi kipindi cha uchaguzi, tutakuwa tumechelewa kwa kuruhusu kiongozi mzembe kuingia madarakani.”
Wajumbe walio wengi katika Kamati namba tisa walisema iwapo ibara hiyo itaachwa kama ilivyopendekezwa, itatoa mwanya kwa wananchi kutumia nafasi hiyo vibaya kwa kuwawajibisha wabunge hata kama hakuna sababu za kufanya hivyo.
Kamati hiyo pia ilishauri badala ay wananchi kupewa mamlaka hayo, Bunge liunde sheria itakayotoa muongozo wa kumuwajibisha mbunge atakayeshindwa kazi na si suala hilo kuachwa mikononi mwa wananchi.
Wajimbe hao pia walitofautiana juu ya sifa za mgombea ubunge ambapo rasimu ya Katiba imependekeza mtu anayetaka kugombea nafasi hiyo awe na elimu ya kuanzia kidato cha nne huku wengine wakisema kusiwe na kiwango cha juu ya elimu.
Pamoja na mapendekezo hayo, baadhi ya kamati zimetaka kuundwa kwa mahakama ya juu, ili kutoa wigo mpana wa utoaji wa haki, badala maamuzi kuishia mahakama ya rufaa pekee.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment