“Niambie sweet, yuko wapi huyo mpumbavu?” Jimmy alimuuliza huku akizungusha kichwa chake kuwatazama watu waliokuwa hotelini hapo, kila mtu akiwa bize kwa shughuli zake.
ENDELEA...
“Wewe kaa kwanza utulie, hivi umeshakuja roho yangu ina amani,” Maria alimwambia Jimmy aliyekuwa akivuta kiti na kukaa, akiangalia upande ambao angeweza kuona vizuri mambo mengi. Jamaa akakubali kwa kutingisha kichwa.
Ndani ya ukumbi ule, askari kanzu wawili pia walikuwa wakiwatazama Stone na Maria kwa zamu. Waliamini kabisa kwamba ule ulikuwa ni wakati ambao kijana huyo alipania kufanya uhalifu. Walitaka kumkamata kijana huyo bila jambo hilo kujulikana kwa wateja wengine waliopo hotelini hapo.
Baada ya kuwa wameshafanya mawasiliano na askari wa Kawe kituoni waliokuwa wakija na difenda ya Polisi, askari mmoja aliifuata meza waliyokuwa wamekaa Jimmy na Maria.“Habari zenu, mimi ni askari, tupo wawili na mwenzangu humu ndani.
Wewe dada unafuatiliwa na jamaa mmoja pale anaitwa Stone, anataka kukudhuru. Lengo letu sisi ni kumkamata, hatutaki kufanya hivyo humu ndani, kwa hiyo tunakuomba usimame ufanye kama unatoka nje, wewe bro subiri hapahapa, yule jamaa atasimama na atakamatwa mara tu akifika getini,” alijieleza askari huyo na kuwafanya vijana wale kumkazia macho.
“Tutaamini vipi kama wewe ni askari na si mmoja wa watu wa Stone,” Jimmy alimuuliza huku akizungusha macho, Stone alikuwa akifuatilia meza yao kwa tahadhari kubwa.“Huna haja ya kuwa na hofu,” alisema huku akitoa kitambulisho chake mfukoni na kumsogezea kwa namna ambayo Stone hakuweza kuona. Jimmy alimwelewa, wakakubaliana na palepale akasimama na kuelekea chooni wakati askari akisimama kuondoka meza hiyo.
***
“Mko chini ya ulinzi,” mmoja wa watu wawili walioshuka kwenye gari lililofunga breki nyuma yao ndiye alitoa kauli hiyo na kumfanya mzee Linus na wenzake waliokuwa ndani ya gari kutahayari. Yule mtu aliyesema maneno hayo alilisogelea gari lao na kufungua milango.
Wakaamriwa kutoka nje. Katika jambo lililowashangaza zaidi mzee Linus na mkewe pamoja na mwanamke waliyekuwa naye, ni kitendo cha gari lingine la tatu kufika eneo hilo na askari wenye bunduki kushuka. Wote watatu wakaamriwa kuingia katika gari moja, ambalo liliwashwa na kuondoka eneo hilo likielekea kituo cha Polisi mjini Morogoro.
Baada ya kuhakikisha wale watu watatu wameanza safari ya kuelekea polisi, askari wale wenye silaha walielekea katika baa iliyokuwepo barabarani, ambayo Dayani alikuwa amekaa na vijana wake.
“Mbona tena simu zao hazipatikani?” Dayani aliwauliza vijana wake alipokuwa akijaribu bila mafanikio kupiga simu ya mzee Linus na wenzake.
“Hebu ngoja nijaribu kusogea nione kuna kitu gani, maana wakati tunaondoka pale kulikuwa na hali flani ya wasiwasi,” Tonsa alimwambia bosi wake huku akisimama. Lakini kabla hajafanya lolote, askari wawili waliovalia kiraia walitoa bastola zao.
“Wote mpo chini ya ulinzi, inueni mikono juu mara moja,” walisema kwa pamoja huku wakijiweka tayari kushambulia. Ni wakati huo ndipo gari lililokuwa na askari wengine waliokuwa na silaha, waliotoka kuwakamata akina mzee Linus ndipo walikuwa wanaingia na kulifanya eneo lile la baa kuwa tulivu.
Watu walikuwa wanashangaa kuona askari wakiingia huku wakiwa na bunduki. Hawakuelewa kitu gani hasa kimetokea. Askari wakawafuata akina Dayani waliokuwa wameinua mikono juu na kuwapekua. Watatu kati yao walikutwa na bastola hivyo kuzidi kuwachanganya wanywaji wengine waliokuwepo hapo.
Akilini mwake, Dayani alikuwa anajilaumu sana kwa kuruhusu kukamatwa kizembe namna ile. Hakuwa ametegemea kama wangeweza kumfikia kama walivyomfikia. Difenda ya Polisi ikaja na kuwaamuru kupanda garini. Ni baada ya msafara huo kuondoka katika baa hiyo, ndipo uhai ukaonekana kurejea upya.
Chanzo: globalpublishers
No comments:
Post a Comment