Akilini mwake, Dayani anajilaumu sana kwa kuruhusu kukamatwa kizembe namna ile. Hakuwa ametegemea kama wangeweza kumfikia kama walivyomfikia. Difenda ya polisi ikaja na kuwaamuru kupanda garini. Ni baada ya msafara huo kuondoka katika baa hiyo ndipo uhai ukaonekana kurejea upya.
ENDELEA...
Aliwahi kukamatwa mara nyingi, lakini mara hizo zote ilikuwa ni baada ya polisi kuhangaika sana na kila alipokamatwa, aliachiwa muda mchache baadaye baada ya kukosekana ushahidi, ingawa pia kwa Dar es Salaam, alikuwa na watu wake ndani ya jeshi la polisi waliokuwa wakimlinda.
Kati ya watu waliokutwa na bastola, na yeye ni miongoni mwao. Licha ya silaha hiyo, pia alichukuliwa simu yake ya mkononi na karatasi zingine zilizokutwa mfukoni mwake. Ingawa alijua angeachiwa baada ya muda mfupi, lakini alifahamu wazi kuwa alikabiliwa na wingu kubwa mbele yake.
Mawazo yake yakarejea familia yake na kwa namna ya kushangaza kabisa, akajikuta akimlaumu rafiki yake mzee Linus, kwa kitendo chake cha kumrejesha katika harakati za kihalifu kwani kwa kiwango cha maisha alichokuwa anaishi, hakutakiwa tena kujihusisha na uhalifu.
Njia nzima hakuna mtu aliyesema jambo lolote hadi gari hilo lilipoegesha nje ya Kituo cha Polisi Morogoro na askari kutangulia kushuka na kuwaamuru wahalifu nao kufuata. Katika usiku ambao lolote lingeweza kutokea, askari waliwaamuru kuweka mikono vichwani mwao.
Wakapita kaunta, wakaingizwa katika chumba kimoja kilichoonekana kuwa ni ofisi. Kulikuwa na viti, wakaamriwa kukaa. Waliachwa humo kwa dakika kadhaa kabla ya Dayani kuchukuliwa na kuondolewa.
Dayani, rekodi zinakutaja kama mhalifu mzoefu na tunao ushahidi wa kutosha katika hili. Huyu Linus bado tunatafuta vitu vya kumuunganisha japo hatuna shaka na urafiki wenu. Hapa Morogoro hamna kesi, isipokuwa usiku huu mtasafirishwa kwenda Dar es Salaam mnakokabiliwa na kesi ya mauaji. Hawa vijana wenu watashtakiwa hapa kwa makosa mengine ya uhalifu ambayo tunaendelea kukusanya ushahidi dhidi yao, askari aliyevalia kiraia, aliyewakalisha katika chumba kingine aliwaambia Dayani na rafiki yake mzee Linus, ambao muda wote walikuwa kimya.
***
Yule askari kanzu baada ya kuondoka katika meza aliyokuwa amekaa Maria na mpenzi wake Jimmy, aliondoka na kuelekea nje, pasipo kuangalia katika meza aliyokuwa amekaa Stone. Jimmy hakukaa sana chooni, alirejea, lakini badala ya kwenda alipokuwa amekaa mpenzi wake, alipitiliza hadi katika eneo lingine la baa ambalo lilikuwa ndani ya hoteli hiyo.
Macho ya Stone yalikuwa yanazunguka kama ya Tai angani, alitazama nyendo za watu wote waliohusiana na Maria na akashindwa kuelewa ni kitu gani kilikuwa kinaendelea. Lakini pale alipokaa, aliamini kabisa msichana huyo jirani yao alikuwa hajamuona. Jua lilianza kuzama na hilo lilimfurahisha zaidi.
Hakukaa muda mrefu kabla ya kusimama na kuanza kuondoka kuelekea nje, jambo ambalo Stone alilifurahia sana. Alipogusa geti la kutokea, Stone aliinua chupa yake ya soda na kumalizia kinywaji chake kilichobaki ndani, kisha akainuka na kuanza kuondoka kuelekea mlangoni.
Wakati akiinuka, Jimmy alimuona, lakini hakufanya papara yoyote. Alipofika nje, alimuona Maria akitembea kwa kuelekea upande ambao haukuwa barabara, kitu kilichomshangaza kidogo Stone. Alimtegemea aelekee barabarani, kwani kule chini alikokuwa akienda, kulikuwa na nyumba za kuelekea baharini, ambako hakudhani kama kunamhusu binti huyo.
Baada ya kupingana na mawazo yake kwa sekunde kadhaa, akaamua kumfuata huko huko anakoelekea, kwa mwendo wa taratibu huku akisoma ramani kama anaweza kutimiza dhamira yake eneo lile.
Mbele kidogo Maria alisimama. Stone hakutegemea, akageuka nyuma, akawaona watu wawili nao wanakuja upande ule, lakini wakionekana kila mmoja akiwa na safari yake. Akachepuka pembeni na kujifanya anajisaidia haja ndogo. Wale watu wawili walimpita. Lakini mtu mwingine akaonekana anakuja upande ule, akaendelea kujifanya anajisaidia huku Maria akiwa bado amesimama.
Akili yake ilikuwa kwa Maria tu. Akamaliza kujisaidia na kuanza kumfuata. Akamsogelea alipokuwa amesimama na alipomfikia, hakumpa nafasi ya kuzungumza. Akamrukia na kumkaba shingo. Lakini pasipo kutarajia, akasikia kitu kizito kikipiga kichwa chake .akapoteza fahamu!!!
Chanzo: globalpublishers
No comments:
Post a Comment