Social Icons

Wednesday, 12 August 2015

Watu wa "Maamuzi" magumu


MPAMBANO wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utahusisha wagombea wawili ambao wana sifa moja kubwa; ya kuwa na uwezo wa kufanya kile kinachoitwa “maamuzi magumu”, lakini wakitofautiana katika mambo mengine.

Mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli amechukua fomu ya kuwania urais jana na mgombea wa Chadema ambaye pia ndiye atawakilisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, anatarajiwa kufanya hivyo wakati wowote wiki hii.

Wagombea hawa wamepishana umri kwa miaka sita, Lowassa sasa akiwa na umri wa miaka 62 huku Magufuli akiwa na umri wa miaka 56. Lowassa aliingia kwenye Baraza la Mawaziri la Rais Ali Hassan Mwinyi kwa mara ya kwanza mwaka 1993 huku Dk. Magufuli akiteuliwa kwa mara ya kwanza na Rais Benjamin Mkapa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi mwaka 1995.

Uamuzi
Lowassa alisifiwa kutokana na uamuzi wa kuvunja mkataba na kampuni ya City Water iliyokuwa ikitoa huduma ya maji kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kwenye miaka ya 1990. Ingawa ulikuwa uamuzi wa Baraza la Mawaziri, lakini aliusimamia bila kuyumba.

Kampuni hiyo ilizorotesha huduma hizo na serikali, wakati huo Lowassa akiwa Waziri wa Maji, iliamua kusitisha mkataba huo ambao awali ilidaiwa ungeisababishia serikali hasara ya mabilioni endapo ungevunjwa.

Alipokuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2008 alipojiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond, Lowassa alikuwa akifahamika kutokana na staili yake ya mchakamchaka iliyofanya viongozi wa maeneo aliyotembelea kuwa “matumbo joto.”

Lowassa pia alijijengea umaarufu kwa kuwa na tabia ya kufika haraka katika maeneo yote ambako matatizo yalikuwa yakitokea na hivyo kujiweka katika nafasi ya kutoa uamuzi wa papo kwa papo kwa watu walioonyesha dalili za kuzembea.

Ni tabia zake hizi ndizo zilizosimika jina hilo la Mzee wa “Maamuzi” Magumu. Wafuatiliaji wa siasa za Tanzania wanaamini kuwa ni uamuzi wake wa haraka ndiyo pengine ulisababisha aingie kwenye suala la Richmond au kwenye lile suala la kutaka kuagiza mvua za kutengeneza kutoka nchini Thailand wakati alipokuwa Waziri Mkuu.

Magufuli amejijengea jina kama Waziri wa Ujenzi asiye na simile kwenye shughuli zake. Kwenye wadhifa wake huo aliweza kuamuru kufanyika kwa bomoa bomoa kwa watu na kampuni zilizokuwa zimejenga kwenye maeneo ya hifadhi za barabara.

Uamuzi huo haukupokewa vizuri na baadhi ya watu na suala hilo lilionekana kama lingeweza kukipunguzia kura chama chake katika chaguzi zilizofuata. Lakini Magufuli aliendelea na mchakato huo pasipo kujali kelele hizo.

Akiwa Waziri wa Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Magufuli aliendesha operesheni kali dhidi ya wavuvi haramu iliyosababisha alaumiwe kwa kuharibu maisha ya wavuvi wadogo waliokuwa wakitegemea uvuvi haramu kuendesha maisha yao.

Lipo pia suala la meli ya kuvua samaki iliyokamatwa ikifanya hivyo katika Bahari Kuu ya Tanzania aliyoikamata akiwa waziri na kuamuru izuiwe na samaki waliokuwepo kugawiwa. Ni uamuzi ambao sasa umeisababishia serikali hasara lakini haiondoi ukweli kuwa meli ile ilikuwa ikifanya uvuvi haramu.

Mmoja wa wasaidizi wa Magufuli aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina alisema tatizo alilokuwa akikabiliana nalo Magufuli wakati akiwa Waziri ni kwamba imefikia wakati mtu anayefuata taratibu anaonekana ndiyo tatizo kwa vile utaratibu sasa ni kuvunja utaratibu.

“Magufuli ni mtu anayependa watu wafuate sheria, kanuni na taratibu. Sasa tatizo la Watanzania ni kwamba wengi wao hawataki kufuata taratibu. Hii tabia mbaya ni lazima ikomeshwe na itakuwa hivyo tu wakati Magufuli atakapokuwa kiongozi mkuu,” alisema.
Ufuasi
Wanasiasa wote wawili wanaonekana kuwa na ufuasi mkubwa. Tangu wakati CCM ikifanya vikao vyake vya uteuzi mjini Dodoma, ilikuwa ikisemwa chini chini kwamba mtu pekee ndani ya chama hicho anayeweza kushindana na wapinzani kwenye uchaguzi ni Magufuli – iwe anashindana na Lowassa au Dk. Wilbrod Slaa aliyekuwa akitarajiwa kupitishwa na umoja wa vyama vinne vya upinzani, maarufu kwa jina la Ukawa.

Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, Magufuli amejipambanua kama waziri mchapakazi zaidi katika serikali za Mkapa na Jakaya Kikwete. Lowassa alitanguliwa na Magufuli kwenye baraza la Mkapa lakini naye alijijengea sifa kutokana na vitendo vyake vya ufuatiliaji.

Hata hivyo, Lowassa alianza harakati za kutafuta urais tangu mwaka 1995, wakati Magufuli akiwa hajulikani kabisa katika siasa za Tanzania na hivyo ana faida ya kujulikana zaidi kuliko mwenzake huyo.
Lowassa pia ana uhusiano wa muda mrefu na waandishi wengi wa habari na vyombo vya habari; hali inayompa nafasi ya habari zake kuandikwa zaidi kuliko Magufuli ambaye ana marafiki wachache kwenye vyombo vya habari. Hata hivyo, taaluma ya uandishi wa habari huzingatia zaidi misingi yake na si urafiki pekee.

Tofauti
Ukiondoa miaka ya karibuni ambapo kumekuwa na maswali kuhusu hali ya kiafya ya Lowassa, mwanasiasa huyo alikuwa akiishi aina ya maisha ambayo vijana wengi wanayapenda. Ndiyo maana, kwenye miaka ya 1990, yeye na aliyekuwa swahiba wake wakati huo, Kikwete, walipachikwa jina la Boyz two Men; wakifananishwa na jina la kundi moja la muziki nchini Marekani.

Katika ujana wake huo, Lowassa alikuwa akifahamika kama mtu anayejipenda kimavazi, mwenye ukwasi mkubwa, anayependa kinywaji na mchapakazi. Hizi hazikuwa sifa za kawaida kwa mwanasiasa aliyelelewa katika misingi ya TANU na CCM.

Hata hivyo, mmoja wa wanasiasa wanaofahamika kama wafuasi kindakindaki wa Lowassa, Peter Serukamba, aliwahi kuliambia gazeti hili kwamba tuhuma za ufisadi zinazoelekezwa kwa mwanasiasa huyo hazina ukweli bali ni majungu tu.

“Ukweli ni kwamba Edward aliamua kuwa responsible na maisha yake tangu angali kijana. Alikuwa anatunza fedha na hakuwa kama wanasiasa wengine tunaowafahamu ambao fedha zao ziliishia kwenye pombe na wanawake. Hiyo ndiyo tofauti na haya mambo ya ufisadi sijui nini yanaletwa tu,” alisema mbunge huyo wa Kigoma Mjini.

Si mengi yanayofahamika kuhusu ujana wa Magufuli. Wakati Mkapa alipomteua kwenye baraza la mawaziri, mbunge huyu wa Chato alikuwa na umri wa miaka 35 tu. Kwa lafudhi yake ya Kisukuma na upya wake huo, Magufuli hajawahi kuonekana kama “mtoto wa mjini” kama ilivyokuwa kwa wenzake wa Boys Two Men.

Magufuli anafahamika kama mmoja wa wanasiasa wachache nchini ambao hawajawahi kuvuta sigara wala kunywa pombe. Ana asili ya Kanisa Katoliki ingawa kuna wakati alikuwa akisali katika makanisa yenye asili ya Kipentekoste.

Lowassa ana shahada mbili alizosomea katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na cha Bath nchini Uingereza. Shahada ya kwanza ilihusu Sanaa za Maonyesho na ya pili ikijikita kwenye Maendeleo ya Uchumi. Kwa ufupi, Lowassa ni mwanasanaa.

Magufuli ana shahada tatu ambazo zote amezipata UDSM. Yeye ni mwanasayansi na amebobea katika masuala ya hisabati na kemia. Ameandika machapisho na vitabu kuhusu usomi wake huo. Kwa ufupi, Magufuli ni msomi mbobezi na anayeandika mawazo yake tofauti na mwenzake huyo.

Magufuli anatoka katika mkoa mpya wa Geita ulioko Kanda ya Ziwa. Lowassa anatoka katika Mkoa wa Arusha ulioko katika Kanda ya Kaskazini. Wote wawili wanatarajiwa kufanya vizuri katika maeneo walikotoka.

Soka
Magufuli na Lowassa hawafahamiki kuwa na mapenzi ya kinazi na mchezo wowote ule ingawa Lowassa amekuwa akihusishwa na klabu ya Simba. Magufuli anahusishwa na klabu ya Yanga ingawa hakuna ushahidi kuwa naye amewahi kuhudhuria mechi yoyote ya klabu hiyo popote hapa nchini.

Uchaguzi
Inatarajiwa kuwa mchuano kati ya Lowassa na Magufuli unaweza kuwa mkali katika historia ya chaguzi za urais hapa nchini. Kuna uwezekano kuwa CCM na Ukawa vikakosa kuwa na wingi wa kutosha bungeni kutengeneza kambi.

Ndiyo maana, wapo wanaoamini kuwa chama kipya cha ACT-Wazalendo, kinaweza kuja kuamua ni chama kipi kitakuwa na wingi wa kutosha bungeni.

Kama chama hicho kipya kitapata walau asilimia kumi ya kura za wabunge, kinaweza kuungana na mojawapo ya CCM au Ukawa kwenye kutengeneza kambi kuu katika Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. -

Chanzo: raiamwema.

No comments:

 
 
Blogger Templates