Social Icons

Saturday, 26 November 2016

'Sekta ya mafuta na gesi si mkombozi kwa Watanzanzania' - Wataalamu




WATANZANIA wanapaswa kufahamu kwamba sekta ya mafuta na gesi ambayo kwa muda sasa inapigiwa upatu kuwa itakuwa mkombozi wa uchumi wa taifa, huenda isilete matarajio ya wengi.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba sekta hii ni nyeti, yenye vishawishi na udanganyifu mkubwa na inahitaji usimamizi wa hali ya juu, kwani asilimia kubwa ya uendeshaji wake unasimamiwa na kampuni za nje, na baadhi zenye hila.

Kwa sasa, Tanzania inakadiriwa kuwa na akiba ya mita za mraba trilioni 57 ya gesi asilia, kwenye maeneo ya ukanda wa Bahari ya Hindi, pamoja na maeneo mbalimbali ya nchi kavu.

Mbali na akiba hiyo, Tanzania pia imeanza mchakato wa kujenga kiwanda cha kuchakata gesi asilia, hatua ambayo itaifanya nchi kuanza kuuza gesi za majumbani, viwandani na nje ya nchi.

Kutokana na kuwa na akiba hiyo ya gesi asilia, Tanzania ni nchi ya pili  kwa sasa baada ya Msumbiji ambayo inaongoza kwa kuwa na akiba ya zaidi ya mita za mraba trilioni 150.

Watafiti wa masuala ya uchumi wameonya kwamba itakuwa hatari kwa nchi kuendelea kutegemea gesi huku wananchi wakiaminishwa kwamba sekta hiyo itakuwa mkombozi wa uchumi.

Wakati wawekezaji mbalimbali wakiweka mitaji yao kwenye utafiti na uchimbaji wa gesi kwa sasa, utaratibu umeandaliwa kwa kutumia sera na sheria ili kuhakikisha kwamba faida itakayopatikana itagawanywa baina ya mwekezaji na serikali.

Hata hivyo, kutokana na kampuni kubwa zinazojishughulisha na sekta ya mafuta na gesi kuendelea kuendeshwa na wageni, itakuwa vigumu kwa nchi kuepuka udanganyifu wa kimapato, kama ilivyofanywa kwenye sekta ya madini, hasa ya dhahabu.

Hadi hivi sasa, sekta ya madini imekuwa ikilalamikiwa kuwa inawanufaisha wawekezaji kutoka nje ya nchi na kwa takribani miaka 20 sasa ni kampuni chache tu ndizo zinalipa kodi ya mapato inayostahili.

Baadhi ya kampuni kubwa za madini ziliingia nchini zaidi ya miaka ishirini iliyopita na hadi sasa hazijaanza kulipa kodi kwa kisingizio kwamba bado wanarudisha fedha zao walizotumia katika uwekezaji.

Wawekezaji wengi kwenye sekta ya mafuta na gesi wamekuwa wakilalamika kitendo cha serikali kutaka kujipatia faida bila kushiriki kwa namna yoyote katika uwekezaji wa awali.

Mkurugenzi wa Utafiti wa Kimkakati wa REPOA, taasisi ya utafiti wa masuala ya uchumi na umasikini, Dk Abel Kinyondo, bado ana wasiwasi kwamba sekta ya mafuta na gesi haijitoshelezi kuitwa mkombozi wa uchumi wa nchi kwani mchango wake utakuwa mdogo kwenye pato la taifa.

Mkurugenzi huyo amebainisha kwamba sekta ya mafuta na gesi itachangia asilimia sita tu ya pato la taifa, kiwango ambacho huenda kisilete matumaini kwa Watanzania ambao tayari wanaamini rasilimali hiyo italeta neema kwa maisha yao.

Hii itakuwa mchango kidogo ikilinganishwa na sekta ya kilimo ambayo inachangia asilimia 25 kwa sasa, zikifuatia sekta za viwanda na ujenzi ambazo kwa pamoja zinachangia asilimia zaidi ya 17.

Imeelezwa kwamba hadi kufikia mwaka 2020 ambapo sekta ya mafuta na gesi itakapoanza kazi kikamilifu, mchango wa sekta hizo tatu za kilimo, viwanda na ujenzi utaendelea kuwa mkubwa zaidi.

 “Kama suala hili halitawekwa mapema na kuelezwa wazi, utegemezi wa sekta ya mafuta na gesi huenda ukasababisha kudorora kwa shughuli nyingine za kiuchumi,” alisema.

Pia imebainika kwamba, kwa kuwa mafuta na gesi ni rasilimali zinazoisha, itachukua miaka si zaidi ya 35 kwa Tanzania kunufaika, kwani baada ya hapo huenda kusiwe tena na rasilimali hiyo hapo baadaye.

Baadhi ya tafiti zimeonyesha kwamba hata ajira kwenye sekta hiyo zitakuwa ni kidogo na Tanzania haitaweza kunufaika zaidi iwapo haitakuwa na miundombinu ya kuongeza thamani ya rasilimali hiyo.

Dk Kinyondo ameyataja maeneo matatu ya hatari ya sekta ya mafuta na gesi kuwa ni kuzuka kwa ugonjwa wa waholanzi (Dutch disease), wanasiasa kuitumia kama mtaji wa kuendelea kutawala pamoja na ushindani wa kimaslahi ambao utasababisha watu kuacha kazi zao za msingi na kuelekeza nguvu zao kutafuta pesa za mafuta na gesi.

Ugonjwa wa Dutch ni hali ya uvivu iliyowakumba Waholanzi baada ya ugunduzi wa gesi na kubweteka kabisa na kutofanyakazi kutokana na kuamini kwamba sekta ya mafuta na gesi itamaliza matatizo yao ya kiuchumi.

Kutokana na hali hiyo, wananchi wengi wa Uholanzi waliacha kufanyakazi na kutegemea kulipwa pesa za mafuta na gesi na matokeo yake sekta nyingine ambazo zilikuwa ni nguzo ya uchumi wa Uholanzi kudorora.

“Watu wengi wameshaaminishwa kwamba, iwapo mambo mazuri yatapatikana kwenye mafuta na gesi ikiwemo mapato, yatagawanywa kwa wananchi na kumaliza shida zote za kiuchumi,” alisema Dk Kinyondo.

Alisema kwa kuwa sekta ya gesi inahusisha fedha na kodi itakuwa ni hatari iwapo viongozi wa kisiasa wataitumia kama fimbo ya kupata ama kubakia madarakani, hali ambayo itadhoofisha demokrasia.

Kwa mfano, kwa kuwa nchi zikiwemo Nigeria, Angola, Libya na Guinea ya Ikweta zilifanikiwa kupata mafuta na gesi, watawala wake walitumia rasilimali hii na mapato yaliyopatikana kuendelea kutawala kwa miaka mingi ama machafuko.

Kwa upande wa Nigeria, upatikanaji wa mafuta umesabaisha machafuko kwenye Jimbo la Delta. Pamoja na utajiri huo, ukosefu wa ajira ni mkubwa sana nchini humo na asilimia 93 ya kaya hazina umeme.

Pia, baada tu ya gesi itakapoanza kuzalishwa kibiashara, Watanzania wengi wenye taaluma mbalimbali huenda wakakimbilia huko kwa ajili ya kupata fedha za haraka na kusababisha mgawanyo mbaya wa rasilimali watu, hasa wataalamu.

Kwa mfano, daktari anaweza kuacha kazi yake ya msingi na kukimbilia kuvizia zabuni kwenye sekta hiyo, na kufanya kuwepo na nakisi ya wataalamu kwenye sekta mbalimbali.

Dk Kinyondo amesema kuwa suala la kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye sekta ya gesi bado linajadiliwa ngazi ya juu tu hasa serikalini na wafanyabiashara wakubwa, na Watanzania wa kawaida wamewekwa pembeni.

“Suala la ushiriki wa Watanzania kwenye sekta ya mafuta na gesi haliko sawa kwani limejielekeza zaidi kwenye masuala ya mrabaha na kodi na mambo mengine ya msingi yameachwa,” alisema.

Anaamini kwamba, ushiriki wa Watanzania kwenye sekta ya mafuta na gesi utaongezeka iwapo kutakuwa na wataalamu wa ndani watakaohusika na uendeshaji wa uchimbaji wa mafuta katika nyanja mbalimbali.

Chanzo. Raia mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates