Social Icons

Friday, 10 February 2017

Mwanzo wa mwisho wa UKAWA?

MWAKA mmoja uliopita, wakati wa Mkutano wa Bunge la Katiba, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alitoka katika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma na kutaja hadharani kwa mara ya kwanza neno Ukawa.

Ukawa ulikuwa ni umoja wa wajumbe wa Bunge hilo ulioundwa na watu kutoka vyama tofauti vya siasa nchini. Ukapachikwa jina la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Profesa Lipumba na wabunge wenzake wa Upinzani walikuwa wakipinga hatua ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba (BMK) Samuel Sitta (Mungu amrehemu), kukubali kujadiliwa na kuingizwa kwa mambo ambayo hayakuwamo katika mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Profesa Lipumba alikuwa kiongozi wa Ukawa iliyotaka Rasimu ya Tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba ndiyo ijadiliwe kwenye BMK na si mapendekezo mengine ya wabunge kutoka chama tawala na washirika wao.

Pembeni yake, Lipumba alikuwa amefuatana na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freema Mbowe na Mwenyekiti wa Chama cha NLD, Dk. Emmanuel Makaidi (Mungu amrehemu).

Hao ndio wakawa vinara wa Ukawa ambayo baadaye ilisusia mchakato mzima wa BMK. Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Ukawa ikawa imejibadili kutoka kuwa umoja wa kutaka Katiba mpya na badala yake kuwa muungano wa vyama vya Upinzani wenye lengo la kuing’oa CCM.

Umoja huo wa vyama uliweka historia ya pekee mwaka 2015 baada ya kufanikiwa kusimamisha mgombea mmoja wa urais; jambo ambalo halikuwahi kutokea –ingawa kilikuwa kilio cha wengi, tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini.

Ukawa ukampata Edward Lowassakama mgombea wake wa urais baada ya kuwa amehama CCM na akakipa chama hicho tawala wakati mgumu kuliko katika uchaguzi mwingine wowote chini ya mfumo wa vyama vingi.

Lakini sasa, takribani miezi 15 baada ya Uchaguzi Mkuu huo, hali ya kisiasana uelewano ndani ya Ukawa ni tete.

Na sababu nyingi. Profesa Lipumba anaongoza CUF lakini hakubaliki kwa baadhi ya wanachama na viongozi wenzake. Makaidi amekwishakufariki dunia na kukiacha chama chake kikiwa taabani. Mbatia bado ni Mwenyekiti NCCR-Mageuzi, lakini wakati anaingia Ukawa alikuwa na wabunge watano, sasa chama kina mbunge mmoja tu, ambaye ni yeye.

Mmoja wa waliokuwa wanachama maarufu na mbunge wa NCCR, David Kafulila, tayari amekihama chama hicho kwenda Chadema; huku baadhi ya viongozi wa chama hicho wakinukuliwa na vyombo vya habari wakisema kwamba Mbatia anakiua chama chao taratibu.

Ndani ya Chadema nako hali si shwari. Dk. Wilbrod Slaa, aliyekuwa Katibu Mkuu wake na mwanasiasa aliyeungwa mkono zaidi ndani na nje ya chama hicho, alijiondoa kwenye chama hicho akipinga kukaribishwa kwa Lowassa na kufanywa mgombea urais.

Nini kimeikumba Ukawa?

Tatizo la kwanza la Ukawa lililetwa nakuingia kwa Lowassa kutoka CCM. Tangu awali, wapo viongozi wa juu wa Ukawa; hasahasa Chadema, walioonyesha kutokubaliana na ujio wa mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Monduli na waziri mkuu aliyejiuzulu wakati wa awamu ya kwanza ya utawala wa Jakaya Kikwete.

Chadema, naUpinzani kwa ujumla, vilikuwa vimejijengea uhalali kama vyama mbadala dhidi ya CCM na ajenda yao kuu kuelekea mwaka 2015 ilikuwa ni kupinga ufisadi. Wakati akiwa CCM, Lowassa alikuwa mlengwa mkuu wa mashambulizi ya upinzani dhidi ya ufisadi.

Ni kuingia huko kwaLowassa ndiyo kulikosababisha kujiengua kwa Dk. Slaa aliyepinga hatua ya kukubali mwanasiasa huyo awe mgombea urais kupitia Ukawa.

Wote wawili; Dk. Slaa naProfesa Lipumba, wamenukuliwa mara kadhaa na vyombo vya habari wakidai kuwa kabla ya kuingia kwa Lowassa, kulikuwa na makubaliano kuwa Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Chadema ndiye angekuwa mgombea urais.

Katika mazungumzo yake na Raia Mwema wiki hii, Profesa Lipumba alisema ingawa yeye alishiriki kwenye kumtaka Lowassa ajiunge na Upinzani, lengo halikuwa kumfanya awe mgombea urais.

“ Ni kweli kwamba tulimtaka Lowassa aje Upinzani. Lakini lengo halikuwa kumfanya awe mgombea urais kwani hilo lingeleta mkanganyiko kwa wafuasi wetu.

“ Iweje mtu ambaye tulitumia muda mrefu kumsema kwamba ni fisadi leo tumkubalie awe mgombea urais wetu. Ndiyo nikasema hata kama mimi ni Mnyamwezi, mzigo wa Lowassa ni mzito.

“ Watu wanasema mimi na Dk. Slaa ni vigeugeu.Hapana. Sisi tulitaka Lowassa aje kutuongezea nguvu kwa sababu alikuwa na mtaji mkubwa wa wafuasi na ushawishi. Lakini si kwa kugombea urais. Hapo tulikuwa tumekwenda mbali sana,” alisema Lipumba.

Katika kipindi cha mwezi mmoja tangu Lowassa kutangazwa kuwa mgombea, Dk. Slaa naProfesa Lipumba; ambao kwa miaka 15 iliyotangulia walikuwa mojawapo ya chachu za mawazo mapya na hoja zenye utafiti miongoni mwa vyama vya Upinzani, walijiondoa kwenye umoja huo.

Gazeti hili limeambiwa kwamba kilichookoa umoja huo wakati wa kuelekea uchaguzi ilikuwa ni haja ya kupambana na adui mmoja ambaye ni CCM; ingawa baadhi ya matatizo yalianza kujitokeza wakati wa uchaguzi wenyewe.

Mojawapo ya matatizo hayo ni ukweli kwamba kuna baadhi ya majimbo ya uchaguzi, hususan, Tanzania Bara, washirika wa Ukawa walishindwa kuachiana kama yalivyokuwa makubaliano.

Kama hatimaye Ukawa ingeshinda uchaguzi wa mwaka jana, pengine changamoto za Ukawa zilizopo sasa zisingeweza kuonekana au zingepungua.

Lakini, kushindwa kwake kwenye uchaguzi huo kumefumua mambo ambayo yanaweka rehani ukuaji wa Ukawa na Upinzani kwa ujumla kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 na kuendelea.

Kwa mfano, Rais John Magufuli, tofauti na Kikwete, amekuwa akionekana kutekeleza mambo ambayo kwa muda mrefu yalikuwa ajenda ya Upinzani.

Magufuli anaonekana kupambana na rushwa na matumizi mabaya ya fedha za umma, anawajibisha viongozi wanaoonekana wabovu, anatatua kero za wananchi na kushughulika na mambo ya muhimu.

Mwelekeo huu wa Magufuli ulikuwa unahitaji Upinzani uibuke na mipango mbadala ya kuufanya uendelee kubaki wa maana katika maisha ya Watanzania.

Kwa bahati mbaya; kwa sababu za kisiasa na zilizo nje ya uwezo wa wanadamu, wanasiasa ambao wangeweza kuwa vinara wa Ukawa sasa wote wapo nje ya siasa za umoja huo.

Profesa Lipumba naDk. Slaa wameondoka rasmi kwenye umoja huo. Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe pamoja na aliyekuwa mshauri wa kisiasa wa Chadema, Profesa Kitila Mkumbo, wote wako nje ya Ukawa na wangeweza kuwa chemchem ya mawazo mapya kwenye umoja huo.

Wakati huohuo, Mabere Marando, mwanamageuzi mbobezi wa Chadema pamoja na Mbatia; wote wajenzi wazuri wa hoja fikirishi za kisiasa; kwa sasa ni wagonjwa na wamepumzika kwa muda kufanya harakati za kisiasa.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema, ni kama amebaki peke yake lakini naye anasongwa kwenye biashara zake binafsi ambako mwishoni mwa mwaka jana ukumbi wake maarufu wa burudani jijini Dar es Salaam –Club Bilicanas ulivunjwa.

Ombwe hili la wafanya siasa limezibwa na watu kama Tundu Lissu na Godbless Lema; ambao mmoja wa viongozi wa juu wa Chadema amepata kusema kwamba ni “wanaharakati zaidi kuliko wanasiasa”.

Tatizo la wanasiasa-wanaharakati ni kwamba wanafanya siasa katika serikali ya Magufuli ambayo ni wazi haina uvumilivu wa siasa za namna hiyo.

Wakati haya yakiandikwa Lema yuko gerezani kwa takribani miezi mitatu kwa madai ya kukashifu mamlaka.

Kuelekea 2020

Katika maoni yake binafsi, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la CUF kwa sasa, Julius Mtatiro, anaamini kuna njia mpya ya kufuata endapo Ukawa na Upinzani kwa ujumla unaweza kupita katika kipindi hiki kigumu.

Tafakuri ya Mtatiro imetokana na matokeo ya uchaguzi mdogo wa ubunge na madiwani uliofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita. Katika uchaguzi huo, CCM ilitetea viti vyake vyote naUpinzani haukupata viti vipya.

“Hali halisi inaonyesha kuwa kama vyama mbadala vingeshirikiana vingelishinda kata si zaidi ya saba hivi. Bahati mbaya ushirikiano huo ulikosekana tangu mwanzo baada ya upande wa "CUF ya Msajili na Bwana Yule (Lipumba) " kusisitiza kuwa wataweka wagombea nchi nzima na hakuna Ukawa.

“Lakini pia, hata shajihisho la ushirikiano mkubwa zaidi lililokuja kuzuliwa na kaka yangu Kitila Mkumbo lilifanywa likiwa limechelewa. Niliwahi kusema, kiuzoefu, vyama haviwezi kuachiana maeneo wiki moja kabla ya siku ya uchaguzi na kushauri hivyo si kwa nia njema.

“Mkakati wa dola na CCM kuvitumia baadhi ya vyama au baadhi ya viongozi kwenye vyama (mamluki) unaelekea kufanikiwa sana. Lakini, sera za "Self Protectionism" ndani ya vyama mbadala hata kwenye mambo yanayohitaji ushirikiano wa kitaifa zitaendelea kuvigharimu vyama vyetu.

“ Habari njema kwa ACT Wazalendo ni kwamba huenda ndicho chama kilichofanikiwa kwenye uchaguzi huu kuliko vyama vyote (CCM inclusive) kwani pamoja na uchanga wake kimevishinda baadhi ya vyama vikongwe kwenye kata chache (kwa idadi ya kura na si ushindi wa jumla).

“ Hii inatakiwa kutuamsha kwamba ACT inahitajika ndani ya kapu la Ukawa. Kwa sababu hii, ACT inatakiwa sasa ienende kama chama cha kweli cha kisiasa wakati Ukawa ikijiandaa kisaikolojia kwa hilo.

“Sijaona uhusiano wowote kati ya matokeo haya na siasa za 2020. Vyama vyote vinayo fursa ya kuendelea kujipanga na kama tutafanikiwa kuuvunja mfumo dola unaoathiri vyombo vya uchaguzi na uhuru wake, unaoondoa mazingira sawa kwa vyama kufanya siasa, mabadiliko ya kikatiba kwenye NEC na sheria za uchaguzi na mengine mengi, siasa za 2020 zitakuwa mbichi sana,” anasema katika maandishi yake.

Katika mazungumzo aliyoyafanya na gazeti hili katikati ya mwaka jana, Profesa Mkumbo alionya kwamba kama Upinzani hautabadilika na kuibua hoja zenye mashiko kwa wananchi katika kipindi cha Magufuli, kuna hatari ya hakika kuhusu uhalali wake wa kuwapo.

Miaka hii mitatu ya mwisho kuelekea mwaka 2020, itakuwa ya kipekee katika mustakabali wa Ukawa na siasa za Upinzani kwa ujumla.

Jambo moja halina shaka kwa sasa, kwamba Ukawa inapita katika wakati mgumu kuliko mwingine wowote tangu kuanzishwa kwake takribani miaka miwili iliyopita.

Chanzo. Raia mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates