Social Icons

Friday, 10 February 2017

Nani walimpigia simu IGP Mangu?

WATU wanaodaiwa kumpigia simu Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, kumshawishi alegeze kamba kwenye vita dhidi ya dawa za kulevya bado hawajafahamika kwa majina lakini Raia Mwema limeambiwa kazi ya kuzuia uingiaji wa dawa hizo hapa nchini imekolea.

Rais John Magufuli alifichua juzi Jumatatu kwamba anafahamu kuna watu walijaribu kumpigia simu IGP Mangu ili afanye ushawishi usio mzuri kuhusu watuhumiwa wa biashara hiyo lakini askari huyo alisimama kidete.

Katika mazungumzo yake na gazeti hili juzi jioni, Mangu hakutaka kuzungumzia suala hilo zaidi ya kucheka tu na kusema Jeshi la Polisi liko thabiti kwenye vita hiyo.

“ Waandishi wa habari mnapenda habari kweli. Ngoja nikwambie tu kwamba Jeshi la Polisi liko thabiti kwenye mapambano hayo na litazidi kusonga mbele. Hilo ndilo naweza kukwambia kwa sasa,” alisema Mangu huku akicheka.

Kauli hiyo ya Magufuli na majibu hayo ya Mangu yametokana na matukio yaliyotokea jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo mamia ya watu; wakiwamo watu maarufu katika tasnia ya burudani, walikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na biashara ya dawa za kulevya.

Operesheni ya kuwakamata watuhumiwa ilitangazwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kuongozwa na Kamanda wa Polisi kanda Maalumu ya Dar es Salaam (RPC), Simon Sirro.

Ni kazi kubwa

Katika uchunguzi wake dhidi ya biashara hii ya dawa za kulevya, Raia Mwema, limebaini mbinu mbalimbali zinazotumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kuingiza bidhaa hizo hapa nchini.

Kwa mujibu wa mojawapo ya ripoti za nyuma zilizowahi kuandaliwa na vikosi kazi vya kupambana na dawa za kulevya, njia kadhaa zimeelezwa kutumika kupitisha dawa hizo.

Njia hizo ni za kisasa na zimebuniwa kwa lengo la kuzuia mashine zinazowekwa kwenye viwanja vya ndege na mbwa maalumu wa kunusa kutojua lolote.

Kwa mfano, Raia Mwema sasa limebaini, baadhi ya wapitishaji wa dawa za kulevya huzungushia dawa zao karatasi maalumu zinazojulikana kwa jina la carbon paper ambazo miale ya mashine hushindwa kutambua.

Watanzania wengi wanazifahamu karatasi hizi ambazo ukiandikia kitu juu yake hujitokeza hadi kwenye karatasi zilizowekwa chini yake lakini waingizaji wa dawa hizo wanazitumia kivingine.

Kwenye kukwepa mbwa, waingizaji wa dawa hizi huweka dawa zao kwenye makopo ya kahawa au yaliyopuliziwa marashi (perfume) kwa wingi, ambayo huwapoteza mbwa maboya.

“ Mbwa wanaijua harufu ya dawa za kulevya. Lakini, kama ukiiweka kwenye boksi au kopo la kahawa mbwa atasikia harufu ya kahawa na hatabaini harufu ya dawa za kulevya.

“ Hivi ndivyo ambavyo watumiaji wa dawa hizi wamekuwa wakipita katika viwanja vingi vya ndege pasipo kutambuliwa. Mtenda maovu kila siku anabuni mbinu mpya za maovu yake,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.

Hati za kusafiria

Kwa muda mrefu, nchi za bara la Asia, hususani Afghanistan na Pakistan, zimekuwa zikitajwa kama mojawapo ya vyanzo vikuu vya uzalishaji wa dawa hizo.

Kwa sababu hiyo, vyombo vingi vya usalama vimekuwa makini na wasafiri wanaosafiri kutoka katika nchi hizo.

Kwa sababu wamejua kwamba wanafuatiliwa, waingizaji wa dawa hizo hapa nchini sasa wamebuni mbinu mpya ya kuingiza dawa hizo.

Mbinu hiyo ni kuwa na hati za kusafiria (passports) zaidi ya moja ambapo wanatoka Tanzania wakiwa na hati ya Tanzania lakini wakienda ugenini huchukua za huko na kuzitumia kwenda Pakistan.

“ Wanachokifanya sasa ni kuwa labda mtu anakwenda Afrika Kusini kabla ya kwenda Pakistan. Anakuwa na hati ya kusafiria ya Afrika Kusini na ya Tanzania.

“ Akifika Afrika Kusini, anaacha ya Tanzania na anachukua ya kule ambayo sasa anasafiria kuendea kuchukua mzigo. Akichukua anarudi nao hadi Afrika Kusini.

“ Akifika Kusini anaacha pasipoti hiyo pale na halafu anachukua ya Tanzania. Mkimkagua hapa Dar es Salaam au Kilimanjaro mnakuta ametoka Afrika Kusini tu. Mnapunguza wasiwasi ambao ungekuwepo kama angeonekana ametoka Pakistan, Raia Mwema limeambiwa kwenye uchunguzi wake.

Vikosi

Raia Mwema limeambiwa na vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi kwamba mmoja wa wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo aliyewahi kukamatwa hapa nchini, alikuja baadaye kubainika kuwa na kampuni yake ya ulinzi iliyokuwa ikimlinda.

Pamoja na mambo mengine, kampuni hiyo ilimpa uwezo wa kununua silaha kali ambazo angeweza kutumia kujilinda endapo angekutwa wakati wa kuingiza dawa hizo hapa nchini.

“ Yule jamaa (anamtaja jina) alikuwa ni kiboko. Alikuwa na walinzi wenye silaha nzito kama Shotgun. Wakati mwingine unakuta ana silaha nzito kuliko hata askari wanaofanya doria. Hali kwa kweli ni mbaya,” gazeti hili limeambiwa.

Ujauzito

Katika mojawapo ya matukio ya kushangaza katika historia ya mapambano dhidi ya biashara hiyo haramu, Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya hapa nchini kiliwahi kumkamata mama mmoja mjamzito raia wa Zambia akiwa na dawa hizo.

Raia Mwema limeambiwa kwamba mjamzito huyo alitumika kwa sababu ya hali yake hiyohiyo na kwamba haikuwa bahati kuwa alitumika.

Kwa mujibu wa sheria za kimataifa za masuala ya anga, mwanamke mjamzito hatakiwi kukaguliwa kwa kutumia miale ya kwenye mashine kwa sababu ya afya ya mtoto na hivyo ujauzito pia umetumika sana kusafirisha dawa hizo.

“ Kama mtu amemeza dawa za kulevya tumboni, huwezi kumuona bila ya kutumia mashine maalumu za ukaguzi. Lakini zile mashine zinatumia miale maalumu ambayo ni mibaya kwa wajawazito.

“ Hivyo ilifikia kipindi ikawa dili mtu kuwa mjamzito. Mtu ukiwa mjamzito tu unafuatwa na watu na wanakwambia utasafiri na watakulipia kila kitu,” mmoja wa maofisa wa ngazi za juu katika Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya aliliambia gazeti hili.

Katika miaka ya mwisho ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, Jeshi la Polisi nchini lilianza kukamata mizigo mikubwa ya wafanyabiashara wa dawa za kuevya.

Mzigo mkubwa kabisa wa dawa za kulevya kuwahi kukamatwa hapa nchini kwa wakati mmoja ulikuwa ni wa mfanyabiashara aliyefahamika kwa jina la Shikuba; uliokadiriwa kuwa na uzito wa kilo 212.

Wakati huo, Operesheni ya kukamata mzigo huo iliongozwa na aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa ambaye hivi sasa amestaafu kutoka serikalini.

Ukamataji huo ulifanyika mwaka 2014 lakini mzigo mkubwa wa kwanza mkubwa ulikamatwa mwaka 2010 ukiwa na kilo 95.

Pia, Polisi waliweza kukamata mizigo mingine mikubwa ya dawa za aina ya Cocaine, Heroin, Mandrax na mengineyo yaliyokuwa na uzito wa kilo 95, 97, 205 85.

Wakati huo, kwenye mikutano mbalimbali na waandishi wa habari, Nzowa alikuwa akisisitiza kwamba mafanikio yaliyopatikana yalisababishwa na ushirikiano mzuri na watoa siri.

Operesheni ya Dar

Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam juzi, Makonda alisema ameamua kupoteza marafiki na kuhatarisha uhai wake kwa sababu ya kuokoa maisha ya Watanzania walio wengi.

Katika mkutano huo, Makonda alitoa siku kumi kwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Wazazi na Watumiaji na Wafanyabiashara kutoa taarifa au kujisalimisha kwa vyombo vya dola.

“Natoa siku 10 kwa kila Mwenyekiti wa Mtaa kwenye mitaa yote ya Dar es Salaam kutoa taarifa za mtaa wake juu ya dawa za kulevya.

Natoa siku 10 kuanzia kesho kwa wazazi, kama wewe ni mzazi unaishi na mtoto anatumia dawa za kulevya na unaishi nae, njoo utoe taarifa.

“Tukikukamata baada ya siku 10 na mwanao anahusika tutaamini na wewe ulikuwa sehemu ya kumfanya mtoto wako atumie dawa za kulevya.

“Natoa siku 10 kwa wafanyabiashara na watumiaji wa dawa za kulevya, waje wenyewe Polisi kwa Kamishna, kama umekuwa ukifanya biashara ya dawa za kulevya na umeacha njoo Polisi, nguvu tunayo, uwezo tunao…. hakuna kiunga tutashindwa kufika, hizi kelele nyingine zinatusaidia kutupa hamasa zaidi za kufanya kazi,” alisema.

Miongoni mwa watu maarufu ambao walikamatwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi mkoa wa Dar es Salaam kuhusiana na tuhuma hizo ni wasanii Wema Sepetu, Chid Benz, Tid, Petit Man na Nyandu Tozz.

Chanzo. Raia mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates