NILIOLEWA NA JINI BILA YA KUTARAJIA 4:
Nikaenda kufungua milango ili nitoke nje niende huko ufukweni.
Nilikazana kufungua mlango wa nje bila ya kujari chochote na nikafanikiwa kutoka nje kumbe mama alisikia wakati nafungua milango, akatoka chumbani kuja kuangalia akaniona nikikazana kuongoza njia.
Mama hakujali kama alitoka na khanga moja ila alinikimbilia na kunishika mkono huku akianza kunirudisha nyumbani kwa nguvu ambapo nilikuwa nagoma.
"Jamani Sabrina mwanangu unaenda wapi?"
"Niache mama, naenda beach."
"Beach usiku huu mwanangu!! Nakuomba turudi nyumbani"
Nilikuwa nagoma kurudi, mama aliendelea kunivuta na dada Penina akaja kumsaidia mama ila kwavile nilipofika hapakuwa mbali sana na nyumba yetu, mama na dada walifanikiwa kunivuta na kunirudisha tena ndani kisha dada akafunga milango halafu mama akanipeleka sebleni na kunikalisha kwenye kochi.
"Mwanangu Sabrina jamani umechanganyikiwa?"
Nikawa namuangalia tu mama tena kwa macho ya hasira, dada naye akadakia.
"Hiyo beach ya usiku huu ukakutane na nani jamani mdogo wangu?"
"Hapo sasa, usiku huu akutane na nani? Mbona unataka kutuletea majini wee mtoto, hujui kuwa ndio mida yao hii? Tena huko baharini ndio nyumbani kwao"
Wakati mama akisema hayo mimi nilijiinamia na kuanza kulia bila sababu tena nililia sana.
"Nadhani fahamu bado hazijamrudia huyu"
"Hivi kwani ilikuwaje mama?"
"Nadhani kaamshwa na zile ndoto za usiku za kutembeza watu, si unazijua zile ndoto. Mtu anaamka na kwenda asipopajua na wengi hupotelea huko, jamani mwanangu kidonda cha babako hapa bado hakijapona halafu wewe unataka kunipatia kidonda kingine. Nitakuwa mgeni wa nani mimi jamani!!"
Mama aliongea kwa uchungu hadi nikaacha kulia na kumtazama usoni.
Mama alikuwa ananiangalia kwa sura ya huruma na upole sana.
Kisha akainuka na kwenda kuchukua maji na kuninawisha uso, kisha akaniinua na kunipeleka dirishani, akafunua pazia na kuniambia.
"Angalia giza la nje mwanangu, ni giza totoro na je unajua ni muda gani saizi?"
Nikatikisa kichwa kwa kukataa kuwa sijui.
"Ni saa nane usiku mwanangu, mbona unataka kuniletea makubwa wewe!"
Tulirudi na kukaa tena kwenye kochi huku akili yangu ikianza kama kuwa sawa hivi.
"Itabidi niwe nalala na funguo siku hizi naona mwanangu Sabrina ameanza kupatwa na vitu vya ajabu, maana mchana ameshindwa kula na usiku huu anataka kutoka bila taarifa mmh sijui ni mambo gani haya?"
Dada akashauri kuwa turudi kulala na mengine tuyazungumze kesho.
Basi mama akanipeleka chumbani kwangu na kuhakikisha nimepanda kitandani ndio akatoka na kwenda chumbani kwake.
Sikuweza kulala kabisa wala kujielewa, nilikuwa najishangaa tu. Kila nikiwaza nakosa jibu kabisa, yule mkaka mtanashati alishaichanganya akili yangu na sikujua kwanini alipenda kunifata kwenye ndoto zangu.
Kulipokucha, mama alikuwa wa kwanza kuja chumbani kwangu kuniangalia na kuniuliza kuwa nimeamkaje, ila nilikuwa mzima wa afya na nilikuwa Sabrina wa kawaida na siku zote.
Nilitoka na kuanza kufanya usafi ili mama atambue kwamba ninajielewa na wala hakuna tatizo tena kwangu.
Baada ya zile kazi mama akaanza kuzungumza na mimi kuhusu ndoto.
"Sikia nikwambie mwanangu, ndoto ni muunganiko wa mambo yote uliyoyafanya siku nzima, usiku ndio yanageuka na kuwa ndoto. Au mara nyingine ni mawazo unayoyawaza ndio hugeuka na kuwa ndoto"
Nikajifikiria inamaana mimi naota vitu ninavyoviwaza au.
Nikaamua kumuuliza mama,
"Inamaana mtu akiota ndoto ya kitu ambacho hajawahi fanya wala kuwaza inakuwa ni ndoto ya aina gani?"
"Mwanangu ndoto zingine hazitabiriki kabisa ila unachotakiwa kufanya ni kumuomba Mungu sana. Lakini mara nyingi ndoto huwa katika mtindo huo niliokueleza, kama vile wewe ulivyoamka usiku na kutaka kwenda beach inaonyesha hicho ni kitu ambacho ulikiongelea kabla"
Nikawa kimya kutafakari kauli ya mama kama ina ukweli wowote ndani yake.
Siku hii sikujishughulisha na simu kabisa nilikaa na kutafakari maisha yangu tu.
Ila ilipofika jioni nilichukua simu yangu kuangalia kama kuna mtu yeyote aliyenitafuta, nikaona hakuna ujumbe wala simu ambayo haikupokelewa.
Nikajiuliza kuwa inamaana Sam amechukia kiasi kwamba ameshindwa kunitumia hata ujumbe! Nikaamua kumtumia mimi mjumbe mfupi wa kumsalimia na ilionyesha kuwa umepokelewa ila hakukuwa na majibu kabisa, nikashangaa sana kwani tabia ya Sam imebadilika.
Kwa kawaida Sam hata nimkosee vipi hawezi kukaa kimya kunijibu hata salamu tu, nikaona lazima kuna tatizo hapa.
Muda huo nilikuwa chumbani na nikamsikia mama kapata ugeni wa rafiki yake pale sebleni, baada ya muda kidogo mama akaniita.
"Sabrina mwanangu, hebu njoo na huku uchangamshe akili"
Ikabidi nitoke nikakae pale sebleni na kumkuta mama Salome ambaye ni rafiki sana wa mama, nikamsalimia na kukaa. Yule mama akaendelea kuzungumza mazungumzo ambayo alikuwa anaongea na mama, ila mimi ndio nikawa mfano katika mazungumzo yake.
"Basi mtu mwenyewe yupo kama Sabrina, yani mwili wake hivyo hivyo. Akapandisha yale majini na kuanza kuropoka mambo ya pale"
Nikajikuta nikichukizwa na zile stori kwani sikupenda kusikiliza stori za majini karibia na usiku sababu zilinitisha wakati wa kulala, nikajaribu kuingizia mambo mengine kama vile kuwaulizia wakina Salome ila yule mama hakuacha kuelezea ile habari yake.
"Yani hali ilikuwa mbaya, kwakweli majini si ya kuchezea mama Penina"
"Sasa mkafanyeje?"
"Mwenzangu, si akataka tumtafutie marashi...."
Sikutaka hata kusikiliza zaidi, nikainuka na kurudi chumbani hadi pale niliposikia kuwa yule mama kaondoka.
Dada Penina aliporudi alikuja moja kwa moja chumbani kwangu.
"Kwani una tatizo gani mdogo wangu?"
Nilitamani kumueleza kuhusu zile ndoto ila nikasita.
"Sina tatizo dada"
"Basi njoo nikuonyeshe kitu"
Nikafatana na dada hadi chumbani kwake.
Akafungua mkoba wake na kunitolea maua mazuri sana na mdori mdogo mzuri,
"Umeona huyu mdori mdogo wangu na haya maua?"
Nikaitikia kwa kichwa.
"Kuna mtu kazini amenipa kama zawadi ila mimi nimeamua kukuletea wewe mdogo wangu, usiwe na mawazo sana. Unaweza kuweka hivi vitu mezani kwako na ukavifurahia"
Kisha nikaenda nae hadi chumbani kwangu, akanipangia yale maua na yule mdori kwenye meza ya pale chumbani kwangu.
"Umeona ilivyopendeza?"
Nikaitikia kwa tabasamu na kumshukuru dada kisha nikamkumbatia.
"Usijari mdogo wangu, sipendi kukuona na mawazo muda wote. Wewe bado mdogo, usijikomaze kwa mawazo. Ukiwa na tatizo lolote niambie hata kama litamuhusu Sam, mi kama dada yako nitakupa ushauri mzuri"
Nikafurahi ila wazo la kuwa Sam hajajibu ujumbe wangu likanijia kichwani na kujikuta nikinyong'onyea kiasi na kumuuliza dada.
"Hivi kwa mfano umemtumia message mtu unayempenda halafu hajakujibu utajielewaje?"
"Kwa haraka haraka unaweza kuhisi amekudharau au kuna kitu bora anafanya kuliko wewe ila ukweli ni kwamba simu haina vocha au imeharibika au ujumbe hajauona, usipende kumfikiria mtu kinyume. Sawa?"
Niliitikia kwa kichwa ila maneno yake yalinipa faraja kiasi.
Usiku wa leo baada ya kula, dada aliweka picha ya ngumi na kunitaka tuangalie wote. Tuliangalia hadi saa tano usiku kisha kuamua kwenda kulala.
Nikiwa kitandani, niliyatafakari sana yale maneno ya dada kuhusu kutokujibiwa ujumbe wangu hadi muda ule. Nikamtumia ujumbe tena na tena Sam ila bado sikujibiwa.
Niliendelea kuhisi kuwa Sam amenifanyia kusudi kwa kutokunijibu nikajisemea kuwa lazima kesho yake niende kwa Sam ili nikamuhoji.
Niliwaza na kupitiwa na usingizi pale kitandani.
Leo katika ndoto, nilimuona dada yangu akiwa kazini kwake kisha akatokea yule mkaka mtanashati wa kwenye ndoto zangu na kumkabidhi zawadi, dada alitabasamu na kuifungua yalikuwa maua na mdori kisha yule mkaka akanitazama mimi kwenye ndoto na kutabasamu.
Nikashtuka pale kitandani na jambo la kwanza lilikuwa ni kuangalia vile vitu alivyonipa dada, ile kupiga jicho kwa mdori nikamuona akitabasamu.
Niliogopa sana, nikajifunika shuka gubigubi ila bado nilimuona mdori yule akitabasamu.
Niliogopa hata kunyanyuka pale kitandani na kupiga makelele pia nilishindwa, nilijikuta nikiwa vile hadi kunakucha na palipokucha jambo la kwanza nilikimbilia chumbani kwa mama. Mama naye akashtuka na kuniuliza.
"Kwani kuna nini mwanangu?"
"Hata sijui"
"Na mbona umekimbia sasa? Si bure umeshaanza kuwehuka wewe."
"Hapana mama"
Sikutoka chumbani kwake hadi na yeye alipotoka, dada Penina alikuwa ameshaenda kazini.
Niliporudi tena chumbani kwangu hali ilikuwa shwari na yule mdoli alikuwa kawaida kabisa ila nikaamua kukusanya yale maua na yule mdoli na kuvirudisha chumbani kwa dada, kisha nikarudi na kukipanga chumba changu upya.
Mchana wa siku hiyo nikamuaga mama kuwa naenda kumtembelea Lucy, mama hakupinga akaniruhusu kwani alimuona Lucy nae aliponitembelea.
Safari yangu ilikuwa moja kwa moja hadi nyumbani kwa Sam, sikumkuta ila nikaamua kumngoja na hakukawia sana akawa amerudi kwenye mida ya jioni hivi.
Tukaingia ndani na kuanza mazungumzo, nilimlalamikia kwanini hajibu meseji zangu akadai kuwa hajapata ujumbe wangu hata mmoja na kusema kila alipojaribu kunipigia alikuwa hanipati hewani.
"Yani hapa nilikuwa nafikiria Sabrina kuwa nimekukosea nini hadi kufikia hatua ya kunizimia simu? Wakati kama safari ya beach ulikataa mwenyewe"
Kwakweli sikumuamini Sam kama kweli alikuwa hanipati hewani wakati simu yangu ipo hewani muda wote na sikumuamini kama kweli meseji zangu hazikufika kwake wakati kwangu zilionyesha kuwa zimefika.
Nikamnyang'anya simu yake ili kuhakikisha kama kweli na moja kwa moja nikaenda kwenye ujumbe unaotumwa kwake (inbox), kuangalia kama kweli ujumbe wangu hata mmoja haukufika.
Kwakweli wakati naangalia nikapatwa na presha kabisa kuona ujumbe uliotumwa na Lucy ukiwa umeongozana kwenye simu ya Sam, tena kila ujumbe niliosoma ulikuwa ni mzito sana.
Nilimuangalia Sam kwa jicho kali sana.
"Ndio nini hiki Sam?"
"Kwani nini?"
Nikampa ile simu yake aangalie mwenyewe.
"Angalia upuuzi unaochat na Lucy"
"Jamani! Lucy si rafiki yako na umenitambulisha mwenyewe?"
"Sasa kama rafiki yangu ndio uchat nae message za namna hiyo?"
"Kwanza unanipa lawama za bure Sabrina na unapandisha jazba bure tu. Tulia kwanza nikueleze"
"Hakuna cha kunieleza Sam, ujumbe wa humo umeshajitosheleza. Sam wewe una tamaa sana yani hadi kwa rafiki zangu loh!"
Nikainuka na sikutaka maelezo yoyote ya ziada na kuanza kuondoka kwani nilipandwa na hasira za ajabu.
Sam akawa ananirudisha ila sikutaka kumsikiliza wala nini ndio kwanza niliongeza mwendo.
Sam alinifatilia hadi alichoka na giza lilikuwa limeshatanda, akaomba kunisindikiza nyumbani nikamkatalia sikutaka tena kumsikiliza Sam ikabidi aniage kwa lazima huku natembea haraka haraka akasema kuwa kesho atakuja nyumbani ili tuweze kuzungumza vizuri.
Sikumsikiliza chochote na niliendelea na safari, nilifika kwenye njia flani na haikuwa na mtu yeyote, nikasikia nyuma yangu mtu akiita Sabrina.
Nikapatwa uoga hadi nikashindwa kugeuka kwani sauti ilikuwa ya kiume ila sio ya Sam.
Wakati natembea haraka haraka nikahisi kama huyo mtu ananikimbilia kwa nyuma, nami nikaanza kukimbia. Nikasikia tena sauti,
"Usinikimbie Sabrina, usiogope."
Nikazidi kupatwa na uoga kwani yule mtu alishafika nyuma yangu.
Mara akanishika bega, uoga ukazidi kunijaa kwani mikono yake ilikuwa na ubaridi uliopenya mwilini mwangu.
Itaendelea kesho.....!!!
Asanteni kwa maoni wadau, maoni yenu ni muhimu sana kwangu.
Kama tuko pamoja
![]()
By, Atuganile Mwakalile.

No comments:
Post a Comment