Rais wa Marekani Donald Trump ameikosoa China kufuatia taarifa kuwa meli za China zimetumika kuhamishia mafuta katika meli za Korea Kaskazini na hivyo kukiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya nchi hiyo.
Rais Trump ameandika katika ukurasa wake wa twitter kuwa China imeshuhudiwa ikiruhusu mafuta kusafirishwa kwenda Korea Kaskazini na kusema amekatishwa tamaa na hatua hiyo na kuongeza kuwa hakutakuwa na suluhisho la kirafiki kuhusiana na Korea Kaskazini iwapo vitendo hivyo vya China vitaendelea.
Trump ambaye mara kadhaa amekuwa akisifu juhudi za China katika kuweka mbinyo dhidi ya Korea Kaskazini hakugusia hatua za kijeshi kutatua mzozo huo wa Korea Kaskazini lakini hivi karibuni alitishia kuisambaratisha Korea Kaskazini iwapo vita itatokea.
China ambayo ni mshirika muhimu wa kibiashara na Korea Kaskazini wiki mbili zilizopita ilisifiwa na rais Donald Trump kwa msaada wake katika juhudi zinazooongozwa na Marekani dhidi ya Korea Kaskazini ikiwa ni pamoja na kuunga mkono vikwazo vya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya taifa hilo lililotengwa.
Hata hivyo Jumanne wiki hii gazeti moja la Korea Kusini likiwanukuu maafisa kadhaa wa Korea Kusini liliripoti kuwa satelaite za Marekani zilishuhudia meli za China zikihamishia mafuta katika meli za Korea Kaskazini karibu mara 30 mwezi Oktoba katika eneo la bahari upande wa China taarifa ambazo pia ziliandikwa na vyombo vya habari vya Marekani ikiwa ni pamoja na shirika la habari la Fox.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema Marekani inataarifa kuwa baadhi ya meli zimekuwa zikihusika na shughuli zilizopigwa marufuku na Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa shehena ya mafuta yaliyosafishwa pamoja na kusafirisha makaa ya mawe kutoka Korea Kaskazini.
Afisa mmoja wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani alisema wanaushahidi kuwa baadhi ya meli zinazohusika na usafirishaji mafuta zina milikiwa na makampuni ya nchi kadhaa yakiwemo kutoka China.
Marekani imesema inalaani kitendo hicho na kuwa ina tumaini nchi yeyote mwanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ikiwemo China itatoa ushirikiano wa karibu kuzuia usafirishaji wa aina hiyo.
China yakanusha taarifa hizo
Wizara ya mambo ya nje ya China kupitia kwa msemaji wake imesema inatekeleza ipasavyo vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini na kuongeza kuwa hana taarifa za hivi karibuni nyingine tofauti na hivyo.
Usafirishaji wa bidha kwa njia ya meli unaoihusisha Korea Kaskazini ni suala lililozuiwa kupitia vikwazo vilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa Septemba 11 pamoja na vikwazo vilivyotangazwa hivi karibuni kufuatia Korea Kaskazini kufanya jaribio la kombora lenye uwezo wa kutoka bara moja kwenda jingine.
Mwezi uliopita idara ya fedha ya Marekani ilitangaza vikwazo dhidi ya makampuni sita ya Korea Kaskazini pamoja na meli 20 na Oktoba 19 kuchapisha picha ilizodai ni meli za Korea Kaskazini ambazo huenda zilikuwa zikihamisha mafuta ili kukwepa vikwazo dhidi yake.
Hata hivyo taarifa hiyo haikufafanua iwapo meli za China zilihusika katika kuhamisha mafuta hayo.
Azimio la Umoja wa Mataifa lililoandaliwa na Marekani linapiga marufuku usafirishaji wa bidhaa zitokanazo na mafuta yaliyosafishwa kwenda Korea Kaskazini kwa kiwango cha asilimia 75 , kuweka kikomo kuhusiana na biashara ya makaa ya mawe pamoja na kuagiza raia wa Korea Kasakzini wanaofanya kazi nje ya nchi hiyo warejeshwe ifikapo mwishoni mwa mwaka 2019.
Mwandishi: Isaac Gamba/afpe/ape
Mhariri :Gakuba, Daniel
Chanzo BBC
No comments:
Post a Comment