Uganda imewashitaki Wanyarwanda 45 kwa madai ya ugaidi kufuatia kukamatwa kwao katika mpaka wake na Tanzania mapema mwezi huu.
Uganda imewashitaki Wanyarwanda 45 kwa madai ya ugaidi kufuatia kukamatwa kwao katika mpaka wake na Tanzania mapema mwezi huu. Msemaji wa polisi Emilian Kayima ameliambia shirika la habari la AFP kuwa washukiwa 43 wa Rwanda, walikamatwa Disemba 11 na wengine wawili walikamatwa wakati wa uchunguzi uliofuatia.
Wote wameshitakiwa kwa kubeba nyaraka za kughushi, vitambulisho vya uongo, na mashitaka ya ugaidi kwa kuwa madhumuni yao yalionyesha hivyo, amesema Kayima bila ya kutoa maelezo ya kina.
Washukiwa hao wanashikiliwa katika gereza la Nalufenya, mashariki mwa mji wa Kampala, ambako kwa kawaida wanafungwa wanaotuhumiwa kwa ugaidi au kujihusisha na makundi ya waasi.
Lakini Rwanda imesema watuhumiwa hao ni wanachama wa chama cha upinzani cha Rwanda National Congress, kilichoko uhamishoni na kinachoongozwa na mshirika wa zamani wa rais Paul Kagame, ambacho Kigali imekiorodhesha kama kundi la kigaidi.
Nchi hizo jirani za Rwanda na Uganda zimekuwa na uhusiano wa ugomvi, mnamo wakati viongozi wake wakishindania ushawishi katika ukanda huo.
Chanzo Dw.de
No comments:
Post a Comment