Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania TBC, Tido Mhando Ijumaa amefikishwa mahakamani jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.
Tido Mhando, hivi sasa ni Mkurugenzi wa Azam Media.
Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) Leonard Swai ameiambia mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Mhando anatuhumiwa kwa mashtaka matano.
Anadaiwa kutenda makosa hayo mwaka 2008 alipokuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC. Anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka na kusababisha hasara ya shilingi 897 milioni za Tanzania.
Mhando hata hivyo amekana mashtaka yote na kuachiwa kwa dhamana. Kesi imeahirishwa hadi Februari 23, 2018 kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.
Mhando aliwahi kutumikia Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC) kama Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili kabla ya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC.
Hali kadhalika aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanspoti na The Citizen.
Pia aliwahi kuajiriwa na Sauti ya Ujerumani (Deutsche Welle), Sauti ya Amerika (VOA), na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) lilipokuwa linafahamika kama Sauti ya Kenya (VoK).
Chanzo. VOA
No comments:
Post a Comment