Rais Donald Trump amewasili Alhamisi kwenye mkutano wa Baraza la Uchumi Duniani unaofanyika kwenye mji wa mapumziko huko Davos, na mara moja kuanza mazungumzo na viongozi wa nchi mbili ambazo ni washirika wa karibu sana wa Marekani—Uingereza na Israel.
Wachambuzi wanasema wajumbe wengi wanaohudhuria mkutano huo huenda wakawa na ukinzani wa mitazamo yenye kushindana juu ya uchumi wa dunia.
Wakati huo huo Trump anategemewa kusukuma ajenda yake ya “Marekani Kwanza”, ambayo imepelekea Marekani kutoza ushuru katika baadhi ya bidhaa zinazoingizwa nchini humo na akitaka kufanya marekebisho ya makubaliano ya uchumi wa dunia.
Lakini wakati wa mkutano wake na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May, Trump amesisitiza kuwa Marekani na Uingereza wanakubaliana na wanashirikiana vizuri kabisa;
Trump amesema: Sisi kwa hivi sasa tunaunganishwa na suala la ulinzi wa majeshi yetu. Tunafikra zinazofanana, maadili sawa, na hakuna kitu kinachoweza kutokea kwako ambapo hatutokuwepo kupigana kwa ajili yenu, unajua hilo. Na nataka kuwashukuru sana, ni heshima kubwa kuwa hapa na wewe leo.”
Muda mfupi baadae, Trump alikutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. Rais na Netanyahu kila moja kwa upande wake alikanusha fikra ya kuwa uamuzi wa Trump kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel—ikiwa ni suala lenye utata kati ya Israel na Palestina—utaathiri juhudi ya kupata suluhisho la amani la kudumu Mashariki ya Kati.
Trump alisema ukweli ni kuwa hatua ya kuitambua Jerusalem itasaidia kurahisisha mazungumzo baina ya pande hizo mbili.
Chanzo. VOA
No comments:
Post a Comment