Chama tawala cha ANC kitafanya mkutano wa dharura leo Jumatatu(05.02.2018)kujadili hali ya baadaye ya rais Jacob Zuma baada ya kuzungumza usiku wa jana na kiongozi anayeandamwa na kashfa kushindwa kumshawishi kujiuzulu.
Jacob Zuma , ambaye yuko madarakani tangu mwaka 2009 , amekabiliwa na mbinyo unaozidi kuongezeka akitakiwa ajiuzulu tangu pale nafasi yake ya uongozi wa chama cha ANC kuchukuliwa mwezi Disemba na Cyril Ramaphosa, ambaye ni makamu wake wa rais. Chama cha ANC kiliitisha kamati ya taifa ya utendaji kukutana katika makao makuu ya chama katika jengo la Luthuli mjini Johannesburg kwa majadiliano.
Ili chama hicho kiweze kumlazimisha Zuma kujiuzulu kama rais wa nchi , kamati hiyo italazimika kuitisha mkutano wa kamati kuu ya taifa, ikiwa ni chombo chake kikuu cha maamuzi, kupiga kura kumuondoa Zuma.
Maafisa sita wa ngazi ya juu wa chama cha ANC walikutana na Zuma usiku wa jana Jumapili katika makao yake rasmi mjini Pretoria lakini hakuna tangazo lililotolewa kuhusiana na kikao hicho.
Kiongozi wa upinzani Julius Malema, mwanachama wa zamani wa ANC, amesema Zuma amekataa kujiuzulu katika mkutano huo Jumapili usiku.
"Amekataa kujiuzulu na aliwaambia wachukue uamuzi kumuondoa iwapo wanataka kufanya hivyo kwa sababu hajafanya chochote kibaya kwa nchi hiyo'', Malema aliandika katika ukurasa wa Twitter.
Waungaji mkono kuandamana
Katika ishara ya Zuma kung'ang'ania madarakani, kundi la waungaji wake mkono linalojulikana kama Waafrika kwanza nchi kwanza , wamesema wataandamana hadi katika jengo la Luthuli leo Jumatatu. Kwa upande mwingine , kundi linalomuunga mkono Ramaphosa la chama tawala cha ANC limesema litalilinda jengo hilo, na kuzusha uwezekano wa mapambano kati ya kambi tofauti za ANC.
Zuma ametengwa na washirika wake muhimu tangu Ramaphosa alipokuwa kiongozi wa chama pekee kuiongoza Afrika kusini tangu kumalizika kwa utawala wa Wazungu wachache mwaka 1994. Ramaphosa, mwenye umri wa miaka 65 yuko katika nafasi nzuri ya kuwa rais ajaye na amekuwa akiweka ushawishi wake ili Zuma aondolewe madarakani.
Zuma hajasema iwapo atajiuzulu kwa hiari kabla ya muda wake wa muhula wa pili kama rais kumalizika mwaka ujao. Vyama vya upinzani na baadhi ya wanachama wa ANC wanataka aondoke kabla ya hotuba ya hali ya taifa hilo katika bunge, hotuba iliyopangwa kutolewa hapo Alhamis.
Zuma ameponea mara kadhaa kuondolewa madarakani katika kura za kutokuwa na imani nae wakati wa utawala wake kutokana na kura za utiifu kwake za wabunge wa chama cha ANC, lakini uungaji mkono wa uongozi wake unapungua. licha ya kuwa Zuma anaendelea kuungwa mkono na baadhi ya makundi ndani ya ANC, hashikilii tena wadhifa wa juu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Daniel Gakuba
Chanzo.Dw.de
No comments:
Post a Comment