Mbunge wa chama cha Demokrat Joe Kennedy amesema kuwa uongozi wa Rais Donald Trump “ sio tu unalenga sheria zinazotuhami- lakini zinaishambulia dhana nzima ya kuwa sisi tunastahili kulindwa.”
Akitoa hisia za chama cha wachache (Demokrat) juu ya hotuba ya Hali ya Taifa iliyotolewa na rais Jumanne usiku, Kennedy amesema mamilioni ya Wamarekani wameachwa wakiwa na “wasiwasi, hasira na uwoga” katika kipindi cha mwaka wa kwanza wa uongozi wa Trump.
Amesema kuwa rais ameunda Kitengo cha Sheria ambacho “ kinarudisha nyuma haki za raia kila siku” kwa watu wasio wazungu na watu wa jinsia mmoja wenye mahusiano ya kimapenzi, watu waliobadili jinsia zao na “imetengeneza mvutano mkubwa” kati ya Wamarekani wenyewe kutoka pwani moja hadi nyingine.
Waliohudhuria mkutano huo katika Shule ya Ufundi ya Diman katika eneo la Fall River, Massachusetts, walimpongeza Kennedy aliposema kuwa uongozi wa Trump umeanzisha mapambano dhidi ya “Ahadi ya Marekani”… “ imani ya kuwa sote tunathaminiwa, sote tuko sawa na sote tunahitajiana.”
Wakati akiainisha kauli mbinu mpya za chama chake, “ Muwafaka Mzuri Zaidi,” Mjukuu wa marehemu Seneta Robert F Kennedy na mpwa wa marehemu Rais John F Kennedy amesisitiza kuwa Wademokrat wataendelea kupigania maslahi mazuri zaidi ya wafanyakazi na huduma ya watoto na nafasi za elimu ambazo watu watazimudu.
Pamoja na kuhakikisha huduma ya afya iliyokuwa inawasaidia watu, bila ya kubagua kama una maradhi ya saratani, msongo wa mawazo au utumiaji sugu wa madawa.” Pia alifagilia baadhi ya sera ambazo zinafanana na zile alizozitaja Trump katika hotuba yake, ikiwemo mikataba ya kibiashara “ ambayo ni ya haki” na kuboresha miundo mbinu.
Alishangiliwa kwa mara nyingine wakati alipotoa ahadi kwa wahamiaji wasio andikishwa milioni 1.8 walioletwa na wazazi wao wakiwa watoto wadogo wanaojulikana kama “Dreamers”: “Nyinyi ni sehemu ya suala letu, tutaendelea kuwapigania. Hatuwezi kuwaacha peke yenu.”
Kennedy alimaliza hotuba yake akiwataka Wamarekani “kumtanguliza Mungu… Hali ya Taifa ina matumaini, ni imara, itadumu.”
Chanzo. VOA
No comments:
Post a Comment