Makala hii ilitoka katika Raia Mwema Toleo la 007 | 12 Dec 2007
BAADA ya kueleza madhara tunayoyasabababisha kutokana na utamaduni uliojengeka wa kuuza na kununua kura, na pia madhara ambayo hatujayaona lakini ni dhahiri yanakuja, sasa napenda kuhitimisha sura hii kwa kufanya lile ambalo tumeambiwa kila mara kwamba hatulifanyi.
Mara nyingi katika jamii yetu wale wanaojitokeza kuyatambulisha matatizo yetu na kukosoa uendeshaji wa shughuli mbali mbali nchini, wamekuwa wakiambiwa kwamba wamekuwa mabingwa wa kukosoa lakini hawatoi mapendekezo ya njia mbadala ya kuendesha shughuli za kitaifa.
Hii imekuwa ni ‘kritiki’mwafaka ya wakuu wa siasa kuwaelekezea wale wanaowakosoa, hata pale ambapo njia mbadala zimekwisha kupendekezwa na zinajulikana, na baadhi zimetokana na uongozi huo huo unaotaka upewe mapendekezo. Ukweli ni kwamba kuna lindi kubwa hapa nchini kati ya kile kilichoamuliwa na kinachotekelezwa. Achilia mbali kwamba hata maamuzi yenyewe yamekuwa hayafanywi kwa wingi unaoendana na matatizo yaliyopo, na yale yanayofanyika yamebeba kila dalili ya kufanyika ama kwa haraka mno, ama kwa kuhakikisha utetezi wamaslahi ya watu fulani, ama kwa kutokujua nini kinaendelea, na kutokujali.
Hili nitalijadili baadaya katika mfululizo huu, lakini nikumbushe tu wa mfano wa kilimo chetu. Mwaka 1972, nikiwa ndiyo nimehitimu tu na nimeanza kufanya kazi ya uandishi, nilipata bahati ya kwenda kuripoti kuhusu mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC) ya TANU, chama tawala cha wakati huo, mjini Iringa.
Pasi na shaka hii ilikuwa ni heshima kubwa kwa kijana mpya kabisa katika shughuli ya uandishi kutumwa katika ngwe kama hiyo, lakini zaidi ya hilo nilivutiwa na mada kuu iliyojadiliwa katika semina ya wajumbe wa kikao hicho.
Mada ilihusu jinsi ya kuinua kilimo cha Tanzania na kumkomboa mkulima wa nchi hii kutokana na ngwamba anayoipata kutokana na kilimo vunja-mgongo cha enzi za Nabii Nuhu.
Mwisho wa semina hiyo, ndipo likatangazwa azimio ambalo kifupi lilijulikana kama ‘Siasa ni Kilimo’. Ndani ya azimio hilo viongozi wa wakati ule wameelezea uduni usiokubalika wa kilimo chetu, na namna gani kinaweza kikabadilishwa, kikaboreshwa, na mkulima mwananchi wa Tanzania akasaidiwa kuinua maisha yake: Matumizi bora zaidi ya ardhi na kinga dhidi ya uharibifu wa mazingira; matumizi ya pembejeo bora, kilimo cha umwagiliaji; matumizi ya wanyama-kazi, n.k.
Leo hii najiuliza ni viongozi au watawala wangapi wanajali azimio hilo lilisema nini. Nani anajisumbua kujua mna nini ndani ya tamko hilo, ni kwa nini halitekelezwi, na tunadiriki vipi kuwafanya wakulima wetu waendelee na kilimo chao duni huku tukitegemea watulishe, miaka thelathini na tano baada ya ‘Siasa ni Kilimo’? Leo hii kila ukiwasikia wakuu wa serikali unachosikia ni amri, amri, amri, na kila mmoja na zake. Katika hili ninalolijadili pia yamekuwapo maamuzi. Mwaka 1992, wakati tukijiandaa kuingia katika ‘mfumo wa vyama vingi’ (ingawa silipendi jina hilo, nalo linadhihirisha jinsi tusivyopenda kusumbua akili zetu hata kutafuta majina) yalifanyika mabadiliko ya kikatiba na kisheria ili kukidhi matakwa ya hali mpya ya kisiasa.
Baadhi ya mambo yaliyoandikiwa sheria mahsusi, ni masuala ya uendeshaji wa vyama vya siasa, uwajibikaji wa viongozi mbali mbali kuhusu masuala kadhaa, mojawapo kubwa likiwa ni suala la matumizi ya fedha katika kampeni za uchaguzi. Haya masuala na masharti yake yameainishwa wazi kabisa katika sheria hizo, ambazo si za zamani kama ‘Siasa ni Kilimo.’ Hata hizi tumekwisha kuzisahau? Ni nini hasa tatizo letu, kumbukumbu fupi? Uelewa mfinyu? Kutojali? Nini?
Pendekezo langu la kwanza ni kwamba watawala wetu walazimishwe kufuata maamuzi yao wenyewe. Hatuwezi kupiga hatua yo yote ya maendeleo iwapo hata maamuzi yetu sisi wenyewe hatuyaheshimu. Ni hivi: Yapo mambo mengi mno ambayo hayafanyiwi uamuzi ingawa yana umuhimu mkubwa. Tumejenga utamaduni ndani ya mifumo yetu wa kuamini kwamba tatizo ukiliacha bila kulishughulikia, litakaa muda mrefu hadi litakapojisikia limekuwa pweke, liondoke.
Labda matatizo ya zamani yalikuwa na tabia hiyo, siyo haya ya sasa. Tatizo la sasa ukilitelekeza, likabaki pembezoni wakati wewe unaendelea kubembea kwa raha za kuazima, utashitukia limekua, limekuwa dude, limeota sharubu na pembe, limefuga kucha mithili ya mambo, halafu limebeba lap-top. Huwezi kulidhibiti tena. Litakudhibiti wewe.
Msomaji atakumbuka jinsi gani baadhi yetu tulipiga kelele kuhusu kile kilichoitwa ‘takrima’. Baadhi yetu tulikataa kuchukuliwa kama vile tuna mtindio wa ubongo, kana kwamba hatujui mantiki ya takrima.
Eti tuamini kwamba unakwenda kutembelea kijiji, kijiji kinakupokea, halafu wewe unatoa ‘takrima’ kuwapa wanakijiji. Kwa maneno mengine wewe mgeni ndiye unawakirimu wenyeji wako! Kama si uhuni ni nini?
Lakini tukaruhusu uhuni huo mpaka ukaingia katika kamusi yetu ya upuuzi, hadi pale mahakama iliposema, acheni upuuuzi, na bado zikaendelea kusikika sauti za kutaka ‘kueleza’.
Ni uharibifu kiasi gani umefanyika katika fikra na saikolojia ya Watanzania katika kipindi chote hiki hatuwezi kujua kwa uhakika, na athari zake huja zikajitokeza katika namna ambayo haitabiriki kabisa. Tukubali tu kwamba mara nyingi upuuzi huwa ghali ingawa gharama yake hailipwi na wapuuzi peke yao.
Basi turudi katika sheria zetu zinazotakiwa kuendesha na kudhibiti uendeshaji wa vyama vya siasa na kampeni za uchaguzi. Kama ambavyo sheria zinasema, tuwatake wakuu wa vyama vya siasa kuonyesha ni kiasi gani cha pesa wanaingiza katika kampeni, na hizo fedha zimetoka wapi, ni kina nani wamechanga, n.k.
Hapana shaka kwamba uendeshaji wa shughuli za chama cho chote, na ushiriki katika uchaguzi wo wote vinahitaji fedha kwa sababu zipo gharama ambazo haziepukiki. Lakini gharama hizo haziwezi kukubalika kuwa ni pamoja na fedha za kuwanunua wapiga kura kwa kuwagawia fedha, kuwalisha pilau, kuwapa vitenge na khanga, au vitendo vyo vyote vinavyoashiria hongo.
Matumizi halali ya fedha ni pamoja na kuitisha na kuandaa mikutano mbali mbali ya ndani na ya hadhara; kusafirisha wajumbe na wapiga kampeni; kuandaa makabrasha, vipeperushi na matangazo mbali mbali ya kuwatambulisha wagombea, vyama vyao na sera zao, n.k.
Hizi zote ni fedha ambazo zinatakiwa zitolewe maelezo, zijulikane ni kiasi gani na zimetoka wapi. Katika nchi za wenzetu, ambao nao kwa viwango vyao na katika mazingira yao tofauti wanapambana na tatizo la matumizi haramu ya fedha, vimewekwa viwango vya uchangiaji kwa kila mchangiaji ili kujaribu kuzuia watu wachache wenye mapesa wasije wakanunua mchakato mzima wa uchaguzi na kisha wakajinufaisha kutokana na kuwa na wawakilishi na watawala walio na deni kwa kundi dogo la raia na makampuni makubwa makubwa ambayo yana maslahi yanayosimamiwa na serikali.
Nchini Marekani hili limekuwa tatizo kubwa, na asasi mbali mbali, ikiwa na pamoja na zile za kiserikali na nyingine za kiraia, zimekuwa zikipambana na ufisadi unaokataa kufa katika matumizi ya fedha. Hawajafanikiwa, lakini angalau wanajaribu, na jitihada zinafanywa kuwabana wale wanaohalifu misingi iliyokubalika. Hapa kwetu hata kuanza bado hatujaanza, pamoja na kwamba tunazo sheria katika vitabu vyetu, sheria ambazo ni kama vile tumeamua zibaki ndani ya vitabu kama mapambo. Sasa ni wakati wa kuziheshimu na kuzitekeleza.
Kwa maoni yangu sheria hizo, hata zikitekelezwa, bado hazijakidhi mahitaji yetu na zitahitaji kuboreshwa kila mara ili ziendane na mbinu mpya zitakazobuniwa na wanasiasa matapeli, ambao tunao wengi.
Lakini hatuwezi kutaraji kuboresha kitu ambacho hata katika upungugfu wake bado hatujajaribu kukitekeleza. Iwapo tunataka kuepukana na mabalaa yanayoweza kutokana na matumizi mabaya ya fedha katika michakato yetu ya uchaguzi, hatuna budi kuanza na utekelezaji wa sheria tulizo nazo, na kisha, katika utekelezaji wake, ndipo tugundue na kushughulikia kasoro zitakazojitokeza kadri tunavyokwenda. Watawala wetu wako tayari kulifanya hilo? Hilo tu, kwa sasa?
Chanzo:- Raia Mwema
No comments:
Post a Comment