Hongera Nchimbi, lakini kazi bado mbichi!
KWA UFUPI
- Askari wa barabarani nao ndio usiseme, rushwa nje nje, kiasi cha kuwa tayari kujishusha kwa madereva wa daladala ambao wakikamatwa wanakuwa tayari wanazo Sh2,000 zao pembeni za kumhonga askari aliyemkamata.
Kwanza tunachukua nafasi hii kumpongeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi kwa kuthubutu.
Wiki hii amewavua madaraka maofisa wanne wa polisi na kuwaachisha kazi askari saba. Hii ni mara ya pili kwa mwaka huu Dk Nchimbi kuwawajibisha watendaji wabovu, lakini jitihada hizo zilizochukuliwa, ni sawa tu na kuondoa gao la nywele kwenye kichwa chenye wastani wa nywele 100,000.
Dk Nchimbi ana kazi kubwa ya kuisafisha Wizara ya Mambo ya Ndani kuanzia Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa, Magereza hadi Uhamiaji. Huko kote kuna uoza wa kutisha ambao umefanywa kama ni mtindo wa maisha, kiasi cha kwamba umekuwa utani wenye ukweli kwa walio wengi mpaka upo msemo maarufu usemao; ‘kuingia polisi bure, kutoka kwa pesa.’
Uoza wa rushwa, polisi kushiriki katika ujambazi, kusafirisha dawa za kulevya na unyang’anyi wa ajabu hata kwa raia walio hohe hahe, ni baadhi tu ya vitendo vinavyokera na ambavyo havistahili kufumbiwa macho kwani ikiwa hali itaendelea kuwa hivi huko tunakoelekea si kuzuri hata kidogo kwa sababu wanaoonewa watachoka na watafanya kile watakachoona kuwa ni sawa katika kutuliza hasira zao.
Askari wa barabarani nao ndio usiseme, rushwa nje nje, kiasi cha kuwa tayari kujishusha kwa madereva wa daladala ambao wakikamatwa wanakuwa tayari wanazo Sh2,000 zao pembeni za kumhonga askari aliyemkamata.
Tabia hizi mbovu za polisi ndizo zinazowafanya raia wakae mbali nao, wawaogope na hata wasipende kutoa ushirikiano. Tabia kama zile za kuwabambikia kesi raia na hata kuwatesa pasipokuwa na ulazima ni baadhi tu ya vitendo vinavyosababisha raia wasiwe na imani na jeshi la polisi.
Leo hii kugundua kuwa kuna askari wa barabarani feki, kuna ofisa usalama feki, inadhihirisha kuwa hakuna mfumo mzuri wa utendaji na ufuatiliaji katika vitengo vya Wizara ya Mambo ya Ndani. Inawezekanaje askari wanaofanya kazi katika eneo moja wasifahamiane hata kwa sura miaka nenda, rudi?
Je, Wizara ya Mambo ya Ndani haina maofisa rasilimali watu? Je, wakuu wa idara hawawafahamu watu walio chini yao? Je, hakuna mgawanyo wa kazi unaoeleweka? Sasa kwa nini watokee polisi na maofisa wa usalama feki? Hii ni hatari, inaonyesha jinsi gani serikali isivyokuwa makini katika ufuatiliaji wa mambo yake ndiyo maana wako wafanyakazi hewa wengi na pia inalipa mabilioni ya shilingi kama mishahara hewa.
Waziri Nchimbi, fagio unalo, safisha Wizara ya Mambo ya Ndani hususan Jeshi la Polisi lakini usisahau kuitupia macho Idara ya Uhamiaji. Zipo pasi nyingi halali za kusafiria ndani ya mikono ya watu wasiostahili kuzipata (ambao si raia). Kuna rushwa nyingi zinazopita katika mikono ya maofisa uhamiaji, wako tayari kuvunja taratibu kwa ajili ya kupata Sh300,000 kutoka kwa mtu anayetaka pasi ya kusafiria.
Siku hizi dhana ya maadili na kuwajibika ni dhana ngeni kwa Watanzania walio wengi, uozo huu tunaouona katika sekta nyingi za umma ni zao la jamii yenyewe. Serikali inapaswa iweke mifumo yake vizuri na ifuatilie utendaji, kinyume cha hivyo tutakuwa tunatwanga kwenye kinu chenye maji!
Sisi wa Mwananchi tunasema; kazi unayofanya Waziri Nchimbi kwa kujaribu kuisafisha wizara yako ni nzuri lakini bado ni ndogo. Vuta soksi na pambana na wahalifu, weka historia.
Chanzo:- Mwananchi
No comments:
Post a Comment