Jengo la Uhamiaji Mbeya
KATIKA kuhakikisha Wimbi la Uhamiaji Haramu linakomeshwa Mkoani Mbeya, Serikali imeagiza viongozi wa Serikali za Vijiji kusimamia uhalali wa Wakazi wanaoishi katika maeneo yao kisheria.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, wakati wa Hafla ya uzinduzi wa Jengo la Ofisi za Uhamiaji Mkoa wa Mbeya lililokuwa likifanyiwa ukarabati kufuatia uchakavu wa Ofisi ziliokuwepo awali.
Kandoro alisema Mkoa wa Mbeya umejipanga kuhakikisha Wimbi la Uhamiaji Haramu linakuwa Historia kwa kuwabana Viongozi wa Serikali za vijiji ambao watabainika kuishi na Wahamiaji haramu katika maeneo yao kinyume na utaratibu kwa kuwachukulia hatua za kisheria.
Mbali na hilo Kandoro alipongeza kuwa Serikali ya Mkoa imepanga na kupitisha agizo kuwa Mtu yeyote atakayebainika kuwasafirisha Wahamiaji Haramu atakamatwa pamoja na Gari lake na kuamriwa kuwarudisha alikowatoa chini ya uangalizi wa Maofisa Uhamiaji ikiwa ni pamoja na kutaifisha Chombo chake ili kupunguza msongamano wa watu magerezani.
“ Mnajua tunawahamiaji wengi sana magerezaji na wanatumia gharama kubwa za serikali kuwatunzia na kuwarudisha, hivyo tumeamua kuwa atakayekamatwa akiwasafirisha ama kuwahifadhi nyumbani kwake atalazimika kuwarudisha alikowatoa na nyumba au Gari vitataifishwa na kuwa mali ya Serikali” alisema Kandoro.
Alisema mbinu hiyo inaweza kusaidia kuondoa kabisa wahamiaji haramu wanaopita kwa wingi Mkoani Mbeya kwa ajili ya kwenda nchi jirani za Kusini mwa Afrika ambako wanaamini kuwa kunamaisha mazuri kuliko nchi za Kaskazini Mwa Tanzania.
Kwa upande wake Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mbeya, William Bambanganya, alisema wimbi la uhamiaji haramu bado ni changamoto katika Jeshi hilo kutokana na ukosefu wa vitendea kazi vinavyoweza kusaidia kuendeshea misako ya Wahamiaji na kuziba mianya na njia za panya wanazotumia kuvukia.
Alisema vitendea kazi vinavyotakiwa sana ni pamoja na Magari ya kufanyia Doria katika Maeneo yote ya Mipaka ambayo ndiko njia kuu za Wahamiaji ziliko na kuongeza kuwa pamoja na Wananchi kukosa ushirikiano na elimu juu ya madhara ya kuwaruhusu Wahamiaji haramu katika majumba yao bila kuwajua tabia zao.
Alisema kwa kipindi cha Mwezi wa Saba jumla ya Wahamiaji 106 walikamatwa ambao wengi wao ni raia wa Nchi jirani ya Ethiopia ambao bado wako Gerezani wakisubiri taratibu za kuwarudisha makwao.
Aidha akitoa taarifa za ukarabati wa Ofisi hizo, Afisa huyo alisema wameamua kukarabati ili kutekeleza agizo la Serikali la kuhakikisha Ofisi na Makazi ya Watumishi wa Serikali yanaboreshwa ili kuleta ufanisi wa utendaji wa kazi.
Alisema katika mpango huo jumla ya Shilingi Milioni 472,997000 zimetumika kukarabati jingo la Ofisi za Uhamiaji Mkoa wa Mbeya na Nyumba mbili za kuishi Watumishi katika kituo cha Tunduma Wilayani Momba.
Aliongeza kuwa awali Ofisi hizo zilikosa mvuta wa viongozi kutembelea kutokana na uchakavu wa Majengo na Thamani za ndani pamoja na eneo la kuegesha magari ambalo halikuwepo awali lakini limetengenezwa katika ukarabani huu.
Chanzo :- Mbeya yetu |
No comments:
Post a Comment