KUFIKIRI NA KUTAFAKARI MAMBO
UTANGULIZI
Kiongozi hawezi kufanikisha mambo mengi iwapo haelewi matatizo yanayomkabili, ili kuyaelewa matatizo kwa undani kiongozi Hana budi awe na uwezo wa kufikiri, kuyachambua mambo na kuhakikisha kuwa, Hali halisi na matatizo yaliyopo yanaeleweka vyema. Hiyo ndiyo tunaita kufikiri na kutafakari vitu kwa makini.
Unajua jinsi inavyoweza kuwa vigumu kutekeleza hata yale uliyokuwa umepanga kuyafanya katika juma. Watu wanataka kukutembelea, marafiki wanataka kuongea nawe, hata unakosa muda wa kutosha kutekeleza yale uliyokusudia kuyafanya. Hivyo kujua namna ya kudhibiti wakati wako ni muhimu sana kama Unataka kupata matokeo yenye faida.
- Kama wewe ni muaminifu,
- Kama unajituma na kuwajibika,
- Kama unaweza kuchanganua mambo, na kujua hali halisi ya matukio vizuri.
- Na kama unadhibiti wakati wako kikamilifu
Upo uwezekano mkubwa kuwa wewe ni kiongozi mwenye ufanisi.
1. MAANA YA KUFIKIRI NA KUTAFAKARI
Kufikiri mambo kwa makini ni tabia, ni mbinu ya kuangalia na kuchambua Hali halisi ya matukio. Mbinu hii Ina mikakati miwili.
1). KUTULIA
2). KUFIKIRI
TULIA
Jambo la awali la kuangalia, ni kwamba katika Hali mbalimbali ambazo hukufikiria au kutegemea, kabla ya kutoa maamuzi, hauna budi kutulia na kuzitafakari.
Kurukia mwisho wa jambo kwa papara ni sawa kabisa na kuamua bila ya kufikiri, hiyo ni hatari. Unapojihisi Unataka Kurukia mwisho wa jambo kwa papara..........TULIA NA TAFAKARI.
KUFIKIRI.
Kufikiri ni kugumu, kunahitaji Faragha na muda mrefu wa kutafakari jambo fulani. Pia kufikiri kunaweza kuhitaji kuwashirikisha watu wengine, ili kupima mawazo
KUTAFAKARI.
Kutafakari, ni kufikiri vitu kwa makini inahitaji usiache kufikiri mpaka unapoelewa. Kufikiri na kutafakari ni sawa na kupita katika handaki lenye kiza hadi kufikia mwanga. Kwa hiyo tafakari kwa makini inamaanisha kukamilisha kufikiri. Usiache kufikiri na kutafakari kabla ya kukamilisha tafakari na kabla ya kuelewa vyema. Weka wazi matatizo yanayotakiwa kuwa wazi. kufikiri pamoja na wengine, na kuwaruhusu wakosoe fikra zako ni sehemu ya hatua za kufikiri.
2. JINSI YA KUTAFAKARI VITU MPAKA MWISHO
2.1. ZIPO HATUA MBILI.
1. Kufikiri peke yako faraghani.
2. Kuwashirikisha wengine fikra zako.
Tuone jinsi tunavyoweza kutumia mbinu hii katika uandishi wa taarifa (ripoti)
1. Fikiri juu ya taarifa, kusanya takwimu na habari zinazotakiwa kisha andika makala ya awali. Usihofu kuisahihisha makala yako ya awali. Na hata kuandika upya. Uichukulie kwa uzito wa kutosha ukiipa muda wa kutosha kuitafakari kwa makini.
2. Muonyeshe mtu mwingine makala yako ya mwanzo ili aisome na kuikosoa
3. Baada ya kukosolewa rejea kwenye makala yako na ufanye masahihisho yanayotakiwa. Hii shughuli itachukua muda mfupi zaidi kuliko ile ya kuandika makala ya mwanzo.
Hatua kama hizo ni lazima kwa kila aina ya tafakari. Hebu tuangalie mfano ufuatao:-
"Juma afisa mradi, alikuwa na matatizo na mmoja wa mafundi ukarabati. Mfanyakazi huyo alichelewa kufika kazini kila siku na alifunga kazi mapema pia alionekana akifanya kazi kidogo tu. Juma alizungumza na mfanyakazi huyo bila mafanikio. Jinsi alivyozidi kufikiria tatizo hilo aliona kwamba:-
1. Lazima achukue hatua fulani.
2. Amfukuze kazi.
3. Ambadilishe kazi.
Baadaye Juma akaamua kubadilishana mawazo na msaidizi wake. Msaidizi huyo akamueleza kuwa huyo fundi alikuwa hajawahi kufanya kazi kama hiyo na huenda hakuelewa alichotegemewa kufanya. Hatimaye Juma alitambua kuwa kama akimuomba mfanyakazi mwenye uzoefu amsaidie anaweza akafanya kazi yake vizuri"
Katika mfano huo unaweza kuona faida ya kubadilishana mawazo na wenzako. Katika tukio hili Juma alipata ushauri mzuri wa msaidizi wake.
2.2 RATIBU MAWAZO YAKO VIZURI
Kuratibu mawazo maana yake ni.
1. Kuweka mawazo yanayofanana katika mafungu.
2. Kuweka mafungu hayo ya mwanzo katika taratibu nzuri.
A) kwanza andika orodha ya shughuli zako zote.
B) kisha panga makusudio yako, kwa mpango ufuatao.
1. Muhimu sana.
2. Muhimu.
3. Kawaida.
3. KWA NINI UFIKIRI NA UTAFAKARI VITU
Sisi wote tunaanza kufikiri wakati tukitaka kuelewa jambo kwa undani, kama kiongozi ni lazima ufikiri siyo tu kwa kutaka kuelewa Bali pia kwa ajili ya kuchukua hatua za utekelezaji. Kuchukua hatua ni sababu moja kuu ya kukufanya wewe kiongozi kufikiri.
4. NINI KIFIKIRIWE KWA MAKINI
- Kufikiri na kutafakari ni tabia, TULIA!
Hali yoyote, tatizo lolote, uamuzi wowote utakaochukuliwa, vinahitaji kufikiri kwa makini.
- Kufikiri kwa makini ni stadi pia . FIKIRI!
Ratibisha mawazo vema. Pokea maoni ya wengine pamoja na masahihisho Yao. Halafu fikiri tena.
4.1 KUPANGA NA KUTATUA MATATIZO
Vipengele Maalumu vinavyohitaji uangalifu wa kufikiri ni KUPANGA NA KUTATUA matatizo.
Utatuzi wa tatizo na upangaji wa mipango ---Vinafanana sana.
Tofauti ya hayo mawili ni kuwa matatizo hutokea bila ya kutazamia na mara nyingi huhitaji utatuzi wa haraka. Bali yote mawili (utatuzi wa tatizo na upangaji mipango) huhitaji kufikiri kwa makini na ukosoaji wa mawazo.
Kupata mawazo, kunaweza kuanza na wazo lako halafu upate mawazo ya ukosoaji kutoka kwa wengine mawazo na ukosoaji wake vitakuwezesha kuyapata mambo ya hakika unayotakiwa kuyajua ili " kutatua tatizo" au " kutoa uamuzi kuhusu mipango" na kutekeleza.
Pia " kupata mawazo" kunaweza kuanzia kwa kuwaomba wengine watoe mawazo yao kwanza. Hapo jukumu lako litakuwa kuwawezesha kufikiri na kutafakari kwa makini. Hasa katika upangaji, ukosoaji wa mawazo huzalisha mawazo mapya na muunganisho mpya wa mawazo.
Matatizo ni jambo la kawaida ambalo mara nyingi utakabiliana nalo kama kiongozi. Wakati mwingine yatakuwa matatizo madogo madogo. Hata hivyo kama hutayafikiria na kuyakabili kwa makini, matatizo madogo madogo yanaweza kuwa makubwa.
MUHTASARI
Katika somo hili tumejifunza kwamba kufikiri na kutafakari kwa makini kuna maana ya:
KUTULIA -- Ni hali itakayokusaidia usirukie kutoa maamuzi.
KUFIKIRI -- Ni mazoea ya kuwa na subira na wasaa wa kufikiri juu ya swali hadi unapolielewa kikamilifu.
Pia tumejifunza mbinu mbali mbali na kutuwezesha kufikiri na kutafakari kwa makini.
KWANZA-: Badilishana mawazo yako na watu wengine, pokea ukosoaji wa wengine, Hii itakusaidia kufikiri zaidi na kukuongezea uelewa.
PILI -: Ratibu mawazo yako pamoja na mawaidha uliyoyapata katika utaratibu mzuri.
TATU -: Fikiri tena juu ya uamuzi unaotarajia kuchukua au kile unachotarajia kukipata kutokana na maamuzi yako.
KUFIKIRI NA KUTAFAKARI KWA MAKINI NI MOJAWAPO YA WAJIBU WAKO MUHIMU KAMA KIONGOZI.
AINA YA PILI YA KUTAFAKARI.
VIELELEZO VYA KUONA
Tunapozungumzia juu ya mawasiliano mara nyingi tunafikiria kuwa maneno ndiyo nyenzo pekee za mawasiliano. Pamoja na kuwa ni muhimu, Haina maana kwamba maneno peke yake ndiyo haleta ufanisi unaotakiwa. Fikiria kwa muda jinsi wanasaikolojia wanavyotuambia.
- Tunajifunza asilimia 11, kwa kusikia maneno.
- Tunajifunza asilimia 83, kwa kuona.
- Tunahifadhi asilimia 20, ya vile tunavyosikia.
- Tunahifadhi asilimia 50, ya vile tunavyoona na kusikia.
Kwa hiyo basi, mambo tunayoyaona ni muhimu sana kwa mawasiliano yenye ufanisi.
Neno ni alama inayosimama badala ya kitu au inayoelezea wazo. Watu wanaotumia lugha moja na wenye kutoka kwenye mazingira yanayofanana kwa kawaida huelewana kutokana na kuwepo kwa utamaduni mmoja wenye kutoa maana sawa ya maneno.
Uzoefu wa moja kwa moja unaohusu kujifunza kwa vitendo humsaidia mtu kuelewa vizuri zaidi somo na jambo linalohusika. Uzoefu ni muhimu katika utaratibu wa kujifunza, vielelezo vya kuona mara nyingi huweza kuwa na ufanisi zaidi kuliko maneno matupu. Lakini kila inapowezekana vinahitajika kuhusishwa na vitendo na uzoefu.
- Tunakumbuka asilimia. 20, ya yale tunayosikia.
- Tunakumbuka asilimia 50, ya yale tunayosikia na kuona.
- Tunakumbuka asilimia 90, ya yale tunayosikia, tunayoona na tunayotenda.
Vielelezo vya kuona huonyesha Hali halisi na hutoa habari sahihi na sawa. Huelezea kwa maumbo halisi na hivyo huleta maana sahihi ya vitu.
Vielelezo vya kuona huwasidia watu kujenga msingi wa majadiliano na uelewano. Huwafanya watu kuwa na fikira zinazolandana.
Vielelezo vya kuona hurahisisha taratibu za kujifunza.
Picha nzuri au onyesho zuri hutoa ujumbe haraka zaidi kuliko maelezo marefu.
Vielelezo vya kuona huwasidia watu kukumbuka vizuri zaidi. Kwa sababu vinarahisisha njia nzima ya kujifunza.
Vielelezo vya kuona husaidia katika utaratibu wa mawasiliano kwa kurahisisha kuelewa na kuongeza kiwango cha kuwashirikisha watu na kuhusishwa habari hizo mpya katika maisha yao ya kila siku.
Vielelezo vyote hivyo ni lazima vilingane na Hali ya kila siku ya maisha ya watu. Hivyo vinahitaji viandaliwe kwa uangalifu. Iwapo vitatumika vizuri basi vielelezo vitasaidia sana kuboresha mawasiliano.
Imetayarishwa na
Bashiru Madodi
No comments:
Post a Comment