FASILI YA DHANA YA MITAZAMO
UTANGULIZI.
Dhana ya mitazamo ni mchecheto unaoelezea namna ambavyo viamshi au vichocheo mbalimbali katika mazingira yetu huchujwa, kupangiliwa na kuratibiwa ili vilete maana au mantiki. Mchecheto huu huanzia katika ufahamu wa mtu, ili kuwezesha kutafsiri na kuvipa maana viamshi au vichocheo kama vile maumbo, watu, rangi, harufu, ladha, sauti, miondoko, vitendo, matukio, maneno, n.k
Kulingana na dhana hii basi, kila mtu anao ulimwengu wake mwenyewe au msingi ambao ni kisababisho cha kujipatia tafsiri maana na mantiki kutokana na viamshi au vichocheo vilivyomo katika mazingira yake. Kuhitilafiana kwa misingi hiyo ndiko kunakopelekea tofauti katika mitazamo baina ya mtu na mtu.
Kwa maana jambo au tukio lile lile linaweza kupewa mtazamo tofauti ama na mtu yule yule au na watu zaidi ya mmoja kwa kutegemeana na misingi na visababisho vya mtazamo husika. Mathalani kunaweza kukawa na tukio moja mahali fulani penye watu saba. Na watu hao saba kila mmoja akalielewa na kulitafsiri tukio hilo kwa maana yake, na hivyo kukawa na matukio saba tofauti ndani ya moja ambayo kila mmoja anaona mtazamo wake kuwa ndio sahihi na halisi. Kwa bahati mbaya, mitazamo inakuwa imejengwa juu ya misingi ambayo si rahisi kuibomoa, na inakuwa na mizizi ambayo vile vile si rahisi kuing'oa.
Tatizo linalojitokeza katika hali hiyo ni jinsi ya kumshawishi mtu akubaliane na mtazamo wa mtu mwingine. Hapo ndipo huhitajika jitihada za ziada, za dhati na za makusudi.
MISINGI NA VISABABISHO VYA UTOFAUTI KATIKA MITAZAMO
Vipo visababisho kadhaa na misingi inayofanya watu wahitilafiane katika mitazamo kwa leo tutaviangalia baadhi ya visababisho hivyo kama ifuatavyo:-
1. JINSI YA MTU
Jambo au tukio linaweza kupewa mitazamo tofauti kwa kutegemea kama muhusika ni mwanaume au mwanamke.
2. UKOMAVU WA AKILI.
Uwezo na ukomavu wa akili, pamoja na kiwango cha kupanuka kwa mawazo na upeo wa kuelewa.
3. ELIMU
Kiwango cha elimu na aina ya elimu, taaluma, mafunzo na kazi azifanyazo mtu.
4. MAPITO NA TAJRIBA ZA MAISHA.
Mambo ambayo yanatengeneza historia ya mtu, yawe magumu au rahisi, mazuri au mabaya likiwemo suala la malezi na makuzi.
5. UTAMADUNI.
Utamaduni, mila, desturi, itikadi (imani) na dini.
6. MALENGO.
Malengo katika ngazi binafsi, ngazi ya asasi, Taifa na jamii kwa ujumla.
7. MOTISHA.
Nia, hamasa na motisha vinavyomsukuma.
8. MUDA.
Kiasi cha muda kinachoruhusiwa kwa mtu kuchuja, kuratibu na kupangilia ili kupata tafsiri, maana au mantiki. Uzoefu unaonyesha kuwa mtazamo wa mtu huweza kuchukua sura tofauti kadiri wigo wa muda unavyozidi kupanuka au kuwa finyu
9. HADHI YA MTU.
Nafasi na hadhi ya mtu katika asasi au katika jamii.
KAULI MBIU KATIKA DHANA YA MITAZAMI ZINASEMA.
Mtazamo wako na unachokiona unategemea unatazama kutoka upande gani, na nafasi ipi.
Kwa mfano:
Tukiwachukua mwenda kwa miguu, abiria katika ndege na gari Moshi ni dhahiri kuwa watu hao wataona mandhari tofauti ya nchi hata kama wote wanatoka Mbeya kwenda D'Salaam.
Mara nyingi mtu ataona kile anachotarajia au anachopenda kuona na Kusikia kile alichotarajia au anachokipenda kukisikia kwa wakati na mahali anapotarajia
Imetayarishwa na
Bashiru Madodi
No comments:
Post a Comment