Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya Mkoa wa Mbeya itafanya mkutano wenye lengo la kuzungumzia mchango wa dini katika kuleta amani ya taifa na dunia kwa ujumla.
Mkutano huo utafanyika siku ya Jumanne tarehe 20/08/2013 katika ukumbi wa mikutano wa Benjamin Mkapa kuanzia saa kumi Alasiri. Inshallah.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano huo. Aidha viongozi na watendaji kadhaa wa serikali katika ngazi mbalimbali mkoani Mbeya pamoja na viongozi wa Jumuiya za kidini na asasi sisizo za kiserikali wamealikwa kwenye mkutano huo, na baadhi yao watapata nafasi ya kuzungumza katika mada hiyo muhimu.
Jumuiya ya Waisamu Waahmadiyya inauona mkutano wa aina hii kuwa ni muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho taifa letu linapita katika wakati mgumu wa mivutano baina ya wanadini wenyewe kwa wenyewe na wakati mwingine na serikali.
Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya ambayo ni Jumuiya ya kimataifa ilianzishwa na Seyyidna Mirza Ghulam Ahmad a.s. katika kijiji cha Qadiani India mnamo mwaka 1889 kufuatia wahyi alioupokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwamba amemtuma ili kuwa Masihi na Imam Mahdi wa zama zetu. Hapa nchini Jumuiya ya Ahmadiyya ilisajiliwa rasmi mwaka 1934.
Tangu kusajiliwa kwake pamoja na kujihusiaha na masuala ya kueneza dini ya Kiislam kwa amani, Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya imesaidia kukuza Lugha ya Taifa kwa kutoa tafsiri ya kwanza ya Qu’ran Tukufu kwa Kiswahili mwaka 1953.
Jumuiya pia inajihusisha na utoaji wa hudum aza kijamii na misaada ya kibinadamu kila inapowezekana hasa kupitia shirika lake la Kimataifa Humanity First. Jumuiya imeweza kusaidia katika ukarabati wa visima vya maji safi vipayavyo 50 kwenye maeneo mbalimbali nchini katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Pia misaada ya vifaa vya maabara, kompyuta, mabegi ya shule, kalamu na madaftari ya kuandikia yametolewa kwenye shule kadhaa nchini yakilenga zaidi maeneo ya wanaohitaji. Kwa sasa Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya duniani inaongozwa na Khalifa wa Tano wa Masihi aliyeahidi Hadhrat Mirza Masroor Ahmad a.t.b.a. huku ikiwa na matawi yake katika nchi 202 duniani.
Wassalaam;
________________
Tahir Mahmood Chaudhry
AMIR – JAMAAT AHMADIYYA TANZANIA.
No comments:
Post a Comment