MGODI UNAOTEMBEA;AIBU HII YA TINDIKALI ZANZIBAR HAIWEZI KUVUMILIKA
NI ajabu kama kuna Mtanzana mwenye mapenzi mema na Taifa lake, bila kuanagalia anatokea Tanzania Bara au Visiwani, kisha akatembea akicheka kwasababu ya matukio yanayoichafua nchi yake.
Watu hao ni wale wanaopita kona zote wakifanya fujo au hata kumwagia wageni acid tindikali, wakiwamo mabinti wawili wa nchini Uingereza waliojikuta wakikumbwa na balaa hilo mjini Zanzibar. Kirstie Trup na rafiki yake Katie Gee walikutana na dhahma hiyo, wakiwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yani Zanzibar, ambapo sasa wamerudishwa nyumbani kwao kwa matibabu.
Baada ya kutokea kwa kadhia hiyo ambapo ni mwendelezo wa matukio yanayoichafua Tanzania nje ya mipaka yake, kila mtu anasema lake, hasa vyombo vya habari vya Kimataifa vinavyoandika habari zinazoonyesha namna gani watalii hao wametiwa vilema vya maisha. Wapo wanaondika kwa kupoza, akiwamo mhariri wa masuala ya Utalii wa Gazeti la Mirror, nchini Uingereza aliyeandika kwa kupoza kidogo katika tukio hilo ambalo kila Mtanzania anapaswa kulikemea kwa vitendo.
“Ninaweza kusema kwamba hakuna sababu ya kutokwenda Zanzibar kwa vile ni mahali salama, panafurahisha na kuna fukwe nzuri na mambo ya kihistoria yenye umaarufu mkubwa,” aliandika Nigel Thompson kwenye gazeti hilo. Hizi ni miongoni mwa kauli mbalimbali zilizotolewa na wadau wa amani, utalii duniani, ikiwa ni saa chache baada ya raia wa Uingereza kumwagiwa tindakali, wakiwa mjini Zanzibar, Agosti 8 mwaka huu.
Kwa tukio kama hilo, hakika Dunia inatupa jicho lake visiwani Zanzibar, huku hisia za kila aina zikishika kasi katika wakati ambao kila Mtanzania anatamani kuona nchi yake inapiga hatua. Japo uchunguzi haujaweza kuthibitisha chanzo cha tukio hilo, zaidi ya wale wanaodhamiwa, akiwamo Sheikh Ponda Issa Ponda, aliyetajwa hadharani katika vyombo vya habari vya Kimataifa kuwa anajua kilichotokea juu ya tukio la kumwagiwa tindikali kwa mabinti wa Uingereza.
Hilo halijabainika, japo najua kuwa kitendo kama hicho ni kuichafua nchi katika ramani za Kimataifa, ukizingatia kuwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, hakuna anayepaswa kuchekea hilo.
Endapo nchi itatumbukia katika hatari hiyo ya kumwagia watalii tindikali, sekta ya utalii inaweza kushuka kwa kiasi kikubwa mno, hivyo kuufanya umasikini uote mizizi kwa Watanzania wote. Watalii zaidi ya 17,000 kwa mwaka wanaotembelea Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watasusa, wakihofia usalama wao ambao kwa siku za hivi karibuni habari mbaya zinaripotiwa kutokea.
Vyama vyote vya siasa sambamba na wadau wa utalii wanapaswa kuwa makini katika suala hili, ukizingatia kuwa ndio kinachoweza kukuza uchumi wan chi endapo suala la utalii litapiga hatua. Chama Cha Wananchi (CUF), Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama Cha Mapinduzi (CCM) TLP, UDP na vinginevyo vinatakiwa kuizungumza hoja hii bila woga kwa wanachama wao.
Dk Ali Mohamed Shein kama Rais wa Zanzibar kwa kushirikiana na serikali yake ya Umoja wa Kitaifa (SUK) sambamba na CUF, huku Maalim Seif Sharrif Hamad ambaye ndio Makamu wa Kwanza wa Rais, wanapaswa kuwa wamoja kujadili tukio hili na mengineyo yasiyokuwa na tija kwa Watanzania.
Hatuhitaji matukio hayo yawe sehemu ya kawaida kwa Tanzania, bila kusahau Zanzibar inayotegemea utalii ili kukuza uchumi wao. Vikundi vya kidini vinavyoibuka vinaishia kuivua nguo Zanzibar inayopendeza na kuvutia watu kuingia humo kujionea mambo ya kale na madhari inayovutia kuitazama kila wakati.
Uamsho wanaotajwa kila pembe ya nchi yetu nao wanapaswa kufahamu kelele zote zinazotokea sasa, ni kwa sababu ya amani iliyopo na uchumi unaokuzwa na sekta ya utalii. Lazima wajuwe kuwa wakitumia vibaya nafasi zao, kuheshimiwa kwao mbele ya jamii wataiweka Zanzibar katika wakati mgumu mno. Vizazi vijavyo havitaweza kuishi kwa amani na utulivu. Watoto wao watakufa njaa na kushindwa kuongoza, maana sekta ya utalii inayotegemewa itakuwa imeanguka.
Nani asiyejua kuwa Tanzania imekuwa ikitegema misaada ya wahisani kutoka nchi mbalimbali duniani. Wahisani ambao wanapojaribu kuja, wanahofia usalama wao, hivyo hili haliwezi kuchekewa. Sekta ya utalii ni muhimu na imekuwa ikitegemewa na Mataifa mengi duniani, ili kukuza uchumi wao, ingawa Watanzania wao hawaoni thamani hiyo na kujikuta wakiwakimbiza watalii.
Kuwamwagia tindikali wageni wetu ni kurahisisha umasikini wetu. Hatuna tunachoweza kuambulia katika suala hilo. Nini faida ya vitendo hivi? Nani amekusudia kuliangamiza Taifa nje ya mipaka yake. Hakuna dini inayoruhusu machafuko au kuwamwagia binadamu wenzao tindikali kwa faida wanayojua wenyewe. Kama hivyo ndivyo, hatuwezi kubaki kimya wakati nchi yetu inaangamia.
Haya ni mambo yanayotakiwa kupigwa vita na Watanzania wote, ndio maana hata Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi ambaye pia ni kiongozi kutoka CUF, Ismail Jussa, hajabaki nyuma kukemea suala hilo. Lazima serikali ifanye juhudi katika hili ili vikomeshwe. Kuna hatari ya Tanzania kushindwa kupiga hatua, kama watalii wataona nchi hii sio mahali sahihi kwa kuishi wala kutembelea.
Doria za polisi ndani ya Mji Mkongwe ambao bado unabakia kuwa ndiyo mji mkuu wa Zanzibar na pia kituo kikuu cha harakati zote za kiuchumi ikiwemo biashara na utalii, ziongezwe ili kupambana na watu wenye mtazamo wao usiokuwa wa Kitaifa zaidi.Wananchi nao waingie kwenye imani ya kulitetea Taifa, huku vitendo visivyokuwa na tija kupingwa, ukiwamo utaratibu wa kuwafichua watu wanaofanya uhalifu wa aina hiyo. Ni kweli Zanzibar inavutia. Inapendeza kutembelewa na kila mmoja wetu, lakini kama hakuna amani hizo ni porojo.
Hakuna anayeweza kujitoa mhanga katika hilo, ndio maana kuna haja sasa ya kuliwekea mkazo suala la amani, ushirikiano na kuwakemea wanaofanya vitendo vya uhalifu, hasa kuwamwagia tindikali na mengineyo. Zaidi Watanzania wenyewe tutajaribu kuharibu mfumo mzima wa utalii wetu, bila kujua athari zinazoweza kulitia Taifa katika umasikini wa milele. Naungana na Jussa aliposhauri kamera za mitaani za kufuatilia nyenendo za watu (Surveillance Cameras).
Mpango huu pia utaleta amani na kuondoa hofu watalii wanaoamua kuitembelea Tanzania ili wajionee vivutio vya utalii vilivyozagaa kila pembe ya nchi yetu. Kuiweka Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika hali ya amani na utulivu ni jukumu letu sote, maana jambo hilo litatuweka katika mazingira mazuri kwenye sekta ya utalii duniani.
Wapo wanaotaka Zanzibar liwe Taifa la Kiislamu. Hao wanafika mbali kwa kuingiza chokochoko za kila aina, ukiwamo mgogoro wa Muungano unaoleta vuta nikuvute kwa Watanzania wote. Kama kuna anayetaka kuleta chokochoko kwasababu za Muungano, basi ni bora akatumia njia nzuri ya maelewano, mazungumzo huku akichambua kwa hoja namna gani nchi ifuate anachotaka.
Lakini kuonyesha hasira zake kwa kutoa uhai wa mwingine au kumpa kilema cha maisha, ni jambo lisilovumilika hata kidogo. Tuyaseme haya bila woga kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Tanzania ni nchi yote. Tukiichafua kwa namna yoyote ile, hasara yake ni kubwa mno, hivyo lazima tuwe makini katika suala hili. Huu ndio ukweli wa mambo. Tuujuwe na kuuzingatia pia.
Chanzo cha habari:- www.michuzijr.blogspot.co.
No comments:
Post a Comment