Social Icons

Sunday, 22 September 2013

AL-SHABAB WASHAMBULIA NAIROBI


WATU zaidi ya 30 wanahofiwa kuuawa, huku wengine zaidi ya 50 wakijeruhiwa, baada ya kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni magaidi, likiwa na silaha nzito, kuvamia na kuteka nyara maduka ya Westgate, maeneo ya Westland, jijini Nairobi. 

Tukio hilo lilitokea jana kati ya saa sita na saba mchana, hali iliyolilazimu Jeshi la nchi hiyo pamoja na watu wanaodhaniwa kuwa ni wa Shirika la Kijajusi la Marekani (CIA), kuingilia kati kuongeza juhudi za uokoaji, lakini pia kukabiliana na magaidi hayo.

Awali Polisi wakisaidiwa na Jeshi, walizingira eneo hilo ambapo sauti za risasi zilikuwa zikisikika kutoka ndani ya maduka hayo, huku kundi hilo likisemekana kuzingira eneo la paa na ghorofa za juu, hali iliyoleta ugumu wa kuwaokoa watu waliotekwa nyara waliokuwa ndani ya maduka hayo. 

Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Kenya, David Kimaiyo, aliwasili kwenye eneo la tukio kuongoza operesheni ya kuokoa watu waliotekwa nyara na kukamata magaidi hayo.

"Ni kweli kuna tukio limetokea Westgate na tunawaomba watu kutokwenda huko, maofisa wetu wanaendelea na operesheni ya kusaka wanaohusika na shambulio hilo,” alisema Kimaiyo.

Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Kenya, ilisema wametuma ulinzi wa anga na kudhibiti magaidi hayo ambayo yalikuwa yakijihami kwa silaha kali.

Ofisa wa Polisi, Benson Kibue, aliliambia Shirika la Habari la AP kuwa magaidi hayo yalijaribu kupora katika duka hilo.

Katika hatua nyingine, Shirika la Habari la Uingereza lilisema limepokea baruapepe nyingi kutoka ndani ya jengo hilo. Saa 11:33, asubuhi, mtu mmoja alisema amejificha ndani ya jengo hilo lakini mtu aliyekuwa karibu yake alikuwa amepigwa na bunduki huku akishuhudia mashambulizi mengine ya risasi.

Arjen Westra, ambaye alikuwa anakunywa kahawa katika eneo hilo, aliiambiwa BBC, Westgate ilikuwa imezingirwa na majambazi. “Nilisikia mlio wa risasi katika eneo la kuingilia. Watu walikuwa wanakimbia hovyo wakiwa wamechanganyikiwa, na wengi walianguka hovyo ndani ya jengo hilo.”

Timu ya madaktari wa dharura ilikuwa na wakati mgumu kuwapa huduma za kwanza na matibabu majeruhi wote nje ya jengo hilo, ambapo wengi walikuwa hawana nguvu za kuendelea kujiokoa.

Msemaji wa Ikulu nchini Kenya, Manoah Esipisu, alisema kuwa operesheni ya kuwaokoa watu waliokwama katika jengo hilo inaendelea, lakini amethibitisha kuwa watu zaidi ya 20 wamefariki dunia mpaka sasa. 

Alisema ni mapema mno kusema shambulio hilo ni la kigaidi, na hakuna shiriki lolote la kigeni lililosaidia kuokoa watu waliojeruhiwa. Jeshi la Uokozi limeungana na Jeshi la Polisi katika operesheni hiyo.

Hata hivyo katika siku za hivi karibuni, Kenya imejikuta katika tishio la kigaidi kutokana na hatua yake ya kupeleka majeshi yake kwenda kupambana na kundi la kigaidi la Al-shabab, nchini Somalia.

MATUKIO YA KIGAIDI KENYA 

Agosti 7, 1998 Ubalozi wa Marekani nchini Kenya ulilipuliwa kwa bomu katika shambulizi la kigaidi, mamia ya watu waliuawa. Shambulizi hilo lilisadikiwa kupangwa na kundi la Islamic Jihad la Misri, ambalo lina uhusiano na kundi la Al Qaeda.

Novemba 28,2002 shambulio la kigaidi lilifanyika katika Hoteli ya Paradise, iliyoko Mombasa. Shambulio hilo lilifanywa kwa kutumia ndege ambayo iligundulika kuwa mali ya Israel. Watu 13 walifariki dunia, huku wengine 80 wakijeruhiwa. Paradise Hoteli ilikuwa inamilikiwa na Israel na ilikuwa pekee kwenye mji huo. Magaidi walifanya shambulizi wakati wageni 60 walipowasili kutoka Israel. 

Taarifa za kijasusi zilimtaja Sheikh Omar Bakri Mohammed, kiongozi wa kundi la Islamic Organisation Al Muhajiroun ni mtu pekee aliyevionya vyombo vya dola kuwa makini na kutokea shambulio lolote mjini Mombasa.

WESTGATE MALL 

Westgate ni kituo maarufu cha biashara mjini Nairobi, ambacho kina miaka sita tangu kuanzishwa kwake. 

Kituo hicho kimepakana na Barabara ya Mwanzi eneo la Westlands, karibu na duka jingine maarufu la Sarif Centre.

Westgate Mall ina jumla ya vyumba 80 ambavyo vina bidhaa mbalimbali, ikiwemo nguo za kila aina, vyakula mbalimbali na huduma za burudani, pamoja na nyingine nyingi.

Chanzo:- Mtanzania

No comments:

 
 
Blogger Templates