Kilichoongeza hofu hiyo ni tukio la hivi karibuni la marais wa nchi wanachama, Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda ambaye ndiye Mwenyekiti wa sasa wa EAC, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Pierre Nkurunzinza wa Burundi kufikia makubaliano ya kuanzisha mchakato wa kuandikwa kwa Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la nchi wanachama wa EAC, bila kuishirikisha Tanzania.
Hatua hiyo ilitanguliwa na kile kilichobainika kuwa wataalamu kutoka nchi za Kenya, Uganda na Rwanda walikutana Kigali siku ya Alhamisi wiki hii kwa ajili ya kuendelea na mchakato wa kutekeleza maagizo ya wakuu wao wa nchi juu ya kuwa na viza ya pamoja kwa watalii kuanzia mwaka 2014 na kuendelea, itakayowawezesha watalii kutembea nchi zote tatu bila kutoa ada nyingine.
Tishio la uhai wa EAC lilianza kujengwa na vikao vilivyokuwa vikifanyika Mombasa nchini Kenya, ambavyo havikuishirikisha Tanzania, ambapo pamoja na mambo mengine ambayo bado hayajafahamika, nchi hizo ziliamua kwa pamoja kuanza mchakato wa kijiinua kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuanza ujenzi wa reli utakaoziunganisha nchi hizo, huku Tanzania ikiwekwa pembeni.
Hili linathibitishwa na kauli iliyotolewa mwanzoni mwa mwezi huu na Waziri wa Mambo na Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ambaye alisema kuwa Tanzania imetaka kupatiwa majibu ya nini kilichojadiliwa katika mikutano hiyo iliyofanyika mfululizo Mombasa, nchini Kenya.
Wakati hayo yakihojiwa, Sekretariati ya EAC imejitetea juu ya kuwepo kwa mgawanyiko ndani ya Jumuiya hiyo, ikisema kuwa mkataba wa Jumuiya unaruhusu nchi wanachama kusaini makubaliano kwa ajili ya utekelezaji wa mambo ambayo walikuwa wamekubaliana kwenye hatua ya kijumuiya, hata kama wengine watakuja kujiunga baadaye watakapokuwa tayari.
Hata hivyo, wachambuzi hao wamedai kuwa mwenendo unaoonekana kuonyeshwa sasa na nchi za Kenya, Uganda na Rwanda ambao unajengwa na mitazamo ya kimaslahi, ndio ambao ulisababisha kuvunjika kwa Jumuiya hiyo miaka 36 iliyopita, wakati huo ikiundwa na nchi za Kenya, Uganda na Tanzania.
Sababu hiyo, ikiwemo ile ya kutokuwa na dhamira ya kisiasa ambayo ilionekana wazi kabla ya Jumuiya hiyo kuvunjika imetafsiriwa na wachambuzi hao kuwa ndiyo inayoakisi mwenendo na matendo yanayotawala sasa ambayo kwa mtazamo wa moja kwa moja, yanajenga mazingira ya kuwapo kwa hofu ya kuvunjika tena kwa Jumuiya hiyo.
Ni kwa msingi huo, ndoto ya miaka mitatu iliyopita ya wachambuzi kwamba EAC ya sasa ingekuwa moja ya jumuiya kubwa na yenye nguvu kibiashara na kisiasa imeanza kufifia, hasa kwa wakati huu, ambapo inaonekana kugawanyika kutokana na mitazamo ya kimaslahi na ubinafsi.
Mambo hayo mawili yanatajwa kuwa ni sehemu mojawapo inayoweza kuharakisha kifo cha Jumuiya hiyo kabla ya kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Hata hivyo, wakati mgawanyiko huo ukishuhudiwa, ni Tanzania pekee ndiyo ambayo imejikuta ikipigwa vita, huku Burundi ikionekana kutokuwa na upande katika mzozo wa sasa wa EAC.
Pamoja na hayo, wachambuzi hao pia wanadai kuwa kinachochochea hali ya sasa ni kitendo cha nchi hizo kuiona Tanzania kama tishio kwa masilahi yao, kutokana na misimamo yake ambayo tayari imeonyesha katika mambo fulani Fulani, hasa yale yanayogusa uchumi wake.
Jambo hili linathibitishwa na kauli ya hivi karibuni ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ambaye alikuwa akizungumzia hatua ya Tanzania kutengwa katika kuelekea kwenye shirikisho la kisiasa.
Akifafanua kuhusu hilo, Sitta aligusia moja ya jambo ambalo Tanzania imeshindwa kukubaliana na wanachama wenzake ndani ya EAC, ambalo ni kibali cha utambulisho, akisema taratibu za Tanzania haziruhusu kutumika katika nchi zote wanachama, kwa sababu lazima raia wa nchi wanachama anapoingia Tanzania afuate taratibu za Uhamiaji.
Alisema licha ya hatua zinazochukuliwa na nchi wanachama wa EAC za kuitenga Tanzania katika baadhi ya mambo, bado itabaki na msimamo wake na haitakubali kuingia kwenye Shirikisho la Kisiasa kama ambavyo nchi nyingine zinataka, wakati ambapo masuala ya ushuru wa forodha, soko la pamoja na sarafu moja, hayajatengamaa.
“Huo ndio msimamo wa Tanzania, hivi vitu vinne vilikuwa bado havijakamilika, sasa wanaharakisha Shirikisho la Kisiasa, waache waende kwa sababu Katiba inawaruhusu na wana ajenda zao za siri,” alisisitiza Sitta.
Kwa mara ya kwanza, marais Kagame, Museveni na Kenyatta, walikutana na kufikia makubaliano ya kuharakisha uundwaji wa Shirikisho la Kisiasa kwa nchi zao kwa kuondoa vikwazo vya kiuchumi na kuweka hati ya vitambulisho vya pamoja na ushirikiano wa kibiashara sambamba na kuzindua mradi wa ujenzi wa gati ya Bandari ya Mombasa.
Hatua hiyo ndiyo iliyozaa mpasuko unaoshuhudiwa sasa, ambao kwa upande mwingine unarejesha kumbukumbu ya anguko la EAC la mwaka 1977, lililosababishwa na itikadi za kisiasa, licha ya kuasisiwa kwa nia njema na Marais, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Tanzania), Jomo Kenyatta (Kenya) na Dk. Milton Obote (Uganda).
Anguko hilo lilizifanya nchi wanachama kila moja kuchukua mali na madeni ya jumuiya hiyo, hata hivyo mgawanyo wa mali unaelezwa kuwa haukuwa wa haki.
Chanzo:- Mtanzania
No comments:
Post a Comment