OFISI ya Bunge, imeeleza kusikitishwa na vurugu zilizotokea bungeni, wakati wa mjadala wa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013. Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, katika mahojiano yake na MTANZANIA Jumatano, yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kuhusu chanzo cha vurugu na hatua zinazochukuliwa na Bunge kudhibiti mwenendo huo, alisema ni jambo la kusikitisha kuona mzozo wa aina hiyo ukiwahusisha wabunge wenye uwezo na weledi mkubwa wa shughuli za kibunge.
Dk. Kashilillah alisema, wabunge wana uwezo wa kufanyia mabadiliko kasoro zilizo katika muswada wowote hata baada ya kusainiwa na rais, lakini pia wana uwezo wa kufanya kabla ya kupitishwa kwa kufuata taratibu husika za Bunge.
Alizitaja taratibu hizo kuwa ni Mbunge kuwasilisha mabadiliko husika anayoyakusudia kwenye muswada katika ofisi yake na kusisitiza kuwa Bunge huwa haliangalii utashi wa chama kwenye maboresho ya muswada.
Aliwataja wabunge waliokuwa wamepeleka majina kwenye ofisi yake kwa ajili ya kuchangia muswada huo, kuwa ni Fausitine Ndugulile, Selemani Jafo na Luhaga Mpina wote wa CCM.
“Kanuni ziko vizuri tu, Mbowe bado anayo nafasi ya kuleta mabadiliko anayoyakusudia na yatafanyiwa kazi, kanuni ya 81 iko vizuri kabisa, fursa hiyo anayo. Wabunge wengi tu wanafanya hivi na kinara wa mabadiliko ni John Mnyika (Ubungo), sijui kwanini Mbowe haleti hili kwa mujibu wa taratibu,” alisema Dk. Kashilillah.
Alipoulizwa iwapo Mbowe kwa wadhifa wake wa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni anayo nafasi ya upendeleo maalumu anapotaka kuzungumza, Dk. Kashilillah alisema kanuni hazielekezi hivyo bali kiti huwa kinatumia busara kumruhusu kadri inavyowezekana kuzungumza.
“Hakuna kanuni inayompa fursa kiongozi wa upinzani bungeni kuzungumza kila anapohitaji kufanya hivyo, hakuna kanuni inayompa fursa Spika kumruhusu kuzungumza kila anapohitaji na wala hakuna kanuni inayoeleza kuwa Waziri Mkuu ambaye ni kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni, kila anaposimama ni lazima apewe fursa ya kuzungumza.
“Kilichopo ni kwamba, Waziri Mkuu ndiye kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni na asilimia 90 ya shughuli za Bunge zinatoka serikalini, sasa ni mazingira hayo ambayo hutumika kumpa nafasi ya kuzungumza kwanza Waziri Mkuu,” alifanunua Dk. Kashilillah.
Akizungumzia utendaji kazi wa Kamati za Bunge, Dk. Kashilillah alisema hazielekezi kuwafuata wadau bali wadau huitwa na kamati kwa maandishi kwa ajili ya kutoa maoni katika muswada husika.
Alisema, madai yaliyotolewa na baadhi ya wabunge kuwa wadau wa Zanzibar hawakushirikishwa si ya kweli, kwa sababu Kamati ya Katiba na Sheria, iliwapelekea wito na walifika kutoa maoni yao.
“Ieleweke kuwa kamati haiwafuati wadau bali inawatumia wito wa kuwaita na wanapaswa kufika mahali walipoelekezwa na kamati na wadau kutoka Zanzibar waliitwa na walifika kutoa maoni yao.
“Kanuni ya 114 (9) inasema, shughuli za kawaida za kamati zitaendeshwa kwa uwazi, ambapo itaalika wadau ili kupata maoni na ushauri wao kwa ajili ya kuboresha Muswada au jambo ambalo litakuwa linashughulikiwa na kamati hiyo.
“Ni mwaka 2011, ilitokea mara moja tu ambapo Spika alisimama juu ya sheria na kutaka kamati iwafuate wadau. Nangependa watu na hasa wabunge walielewe hili vizuri, wasilipotoshe,” alisema Dk. Kashilillah.
Hii ni mara ya kwanza kwa Dk. Kashilillah kuzungumzia mgogoro ulioibuka bungeni, ikiwa ni takribani wiki tatu baada ya kutokea huku chanzo chake kikiwa kuzuiliwa kwa Mbowe kuzungumza.
Mbowe alizuiliwa na Naibu wa Spika, Job Ndugai kuzungumza wakati wa mjadala wa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013.
Tayari wadau mbalimbali wa mambo ya kibunge, wamekwishaanza kumnyooshea kidole Mbowe kwa kukiuka kanuni za Bunge, kwa kile wanachokieleza kuwa anafanya makusudi kwa nia ya kujitafutia umaarufu wa kisiasa ama ni mbumbumbu wa kanuni hizo.
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, kanuni ya 60, fasiri yake ya kwanza inasema Mbunge akitaka kusema anaweza (a) kumpelekea Spika ombi la maandishi, (b) kusimama kimya mahali pale.
Fasiri ya pili inaeleza zaidi kuwa isipokuwa kwamba, Mbunge yeyote hataanza kuzungumza hadi aitwe na Spika ama kwa jina au wadhifa wake na kumruhusu kusema na wakati wa kusema ataelekeza maneno yake kwa Spika.
Mwongozo huu wa kanuni haukufuatwa na Mbowe ambaye baada ya kuzuiliwa kuzungumza na baadaye kuamriwa na Naibu Spika kutoka nje, baadhi ya wabunge wa upinzani walijitokeza kumuunga mkono, jambo ambalo lilisababisha kuzuka kwa mapambano baina yao na maaskari na wabunge.
Chanzo:- Mtanzania.
No comments:
Post a Comment