Social Icons

Wednesday, 25 September 2013

TANZANIA NA RWANDA ZAUNDIWA BARAZA.


JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC), inatarajia kuunda Baraza la Usalama litakalotumika kutatua migogoro iliyopo ndani ya jumuiya, likianza na mvutano wa kidiplomasia ulioibuka hivi karibuni baina ya Tanzania na Rwanda. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtandao wa habari wa ‘Rwanda News’, ukimnukuu Naibu Katibu Mkuu wa EAC, Charles Njoroge, baraza hilo limetokana na juhudi za wakuu wa nchi wanachama zinazotarajia kuunda Shirikisho la Kisiasa.

“Tunategemea kuwa na Shirikisho la Kisiasa, pia tunakaribia kuanza kufikia makubaliano kuhusu suala hili la kuwa na Baraza la Usalama. Tunataka kuwa na Baraza la Usalama ambalo litakuwa chombo cha kutoa uamuzi kuhusu mambo mbalimbali yatakayoibuka ndani ya ukanda huu,” alisema Njoroge.

Aliutaja mgogoro wa kwanza utakaoshughulikiwa na baraza hilo baada ya kuundwa kuwa ni wa Tanzania na Rwanda.

Akizungumzia hatua ya Tanzania kutoshirikishwa katika muungano wa baadhi ya nchi wanachama wa EAC, kwa kutoa mifano ya miradi ambayo imeanza kutekelezwa na nchi za Rwanda, Uganda na Kenya, Njoroge alisema ni jambo ambalo linakubalika kwa mujibu wa taratibu za jumuiya hiyo.

“Hakuna tatizo kuwapo kwa jumuiya ndogo ndani ya jumuiya, ni kutokuelewa tu kwamba nchi mbili zinapounga kupata faida fulani ni jambo linaloruhusiwa,” alisema.

Hivi karibuni kumekuwapo na mikutano ya marais wa Kenya, Uganda na Rwanda ya kujadili kuboresha miradi ya miundombinu ikiwamo bandari.

Lakini Njoroge amekaririwa akieleza kuwa nchi za Sudani Kusini na Somalia, zinataka kujiunga na jumuiya hiyo jambo ambalo ni dalili njema za ukuaji wake.

Mgogoro kati ya Tanzania na Rwanda uliibuka baada ya Rais Jakaya Kikwete kumshauri Rais Paul Kagame wa Rwanda, kuzungumza na waasi wa nchi hiyo ili kumaliza migogoro inayoendelea.

Ushauri huo ulionekana kumkera Rais Kagame ambaye alianza kumrushia maneno makali yenye kejeli na dharau Rais Kikwete.

Wakati hayo yakiendelea, wiki chache zilizopita, mawaziri kutoka nchi za Kenya, Rwanda, Uganda na Burundi, walikutana kwa ajili ya kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la Jumuiya ya Afrika Mashakiri.

Kufuatia hatua hiyo, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta alisema kuwa ameliandikia barua baraza la mawaziri wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo, wakilalamikia hatua zinazoendelea kuchukuliwa na jumuiya hiyo bila kuishirikisha Tanzania.

Chanzo:- Mtanzania.

No comments:

 
 
Blogger Templates