Social Icons

Friday, 20 September 2013

DR. KILAHAMA: NILIHONGWA GARI NA MAFISADI MALIASILI.

Wizara ya Maliasili na Utalii ni  miongoni mwa wizara zinazodaiwa kugubikwa na vitendo vingi vya rushwa. Katika mahojiano na gazeti hili hivi karibuni, kati ya Mwandishi Wetu EZEKIEL KAMWAGA na Dk. Felician Kilahama, Mkurugenzi wa Mwisho wa Idara ya Misitu na Nyuki, iliyokuwa chini ya wizara hiyo anaeleza changamoto alizowahi kukumbana nazo katika idara yake, ikiwa ni pamoja na maelezo yake kuhusu rushwa.

Raia Mwema: Umestaafu serikalini tangu Desemba mwaka jana, unaonaje maisha ya kustaafu? Je, tayari umeanza kuyakosa maisha ya ofisini?

Dk. Felician KilahamaDk. Kilahama: Hapana kwa kweli. Kwa bahati nzuri bado niko activesana kwenye mambo mengine. Niko kwenye bodi mbalimbali za asasi za kiraia, nafanya kazi zangu za kisomi.

Usisahau pia kwamba kwa sasa mimi ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Misitu ya Dunia mpaka Juni mwakani. Hii ni kamati inayoangaliwa misitu yote duniani na kuona kwamba inaangaliwa na kutunzwa kwa faida ya kizazi hiki na vingi vijavyo.

Kwa hiyo, kusema ukweli, bado niko busy kidogo na bado sijaanza kukaa tu bila ya kufanya lolote.

Raia Mwema: Ilikuwa ndoto yako kuwa mtaalamu wa masuala ya misitu tangu utotoni au hili ni jambo ambalo umekuja kukutana nalo ukubwani?

Dk. Kilahama: Mimi nimekulia kijijini na kusema kweli wakati ule tukikua kulikuwa hakuna mtaalamu wa misitu anayejulikana. Kulikuwepo na walimu, madaktari na watu wa fani nyingine lakini si wataalamu wa misitu.

Kwa hiyo misitu halikuwa chaguo langu la awali. Hata hivyo, nilikuwa nafaulu vizuri kwenye masomo ya Sayansi na nilichukua combination ya CBG (Chemistry, Biology and Geography) wakati nilipokuwa Sekondari ya Tosamaganga pale Iringa.

Nilipofaulu nikachaguliwa kusoma Shahada ya Misitu hapa Tanzania, nikasoma shahada ya pili kule Canberra katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Australia (Australia National University-ANU) na baadaye ndiyo nikapata shahada ya Uzamivu kwenye mambo hayohayo ya misitu.

Hivyo ni kitu ambacho nimekisomea baadaye nikatokea kukipenda na ndiyo maana kimenijengea heshima dunia nzima. Nawaambia watu kila siku kwamba ukiipenda kazi yako, utafahamu kila unalotakiwa kufahamu nab ado utaheshimika tu.

Raia Mwema: Umestaafu kutoka katika wizara ambayo inakumbwa na kashfa za rushwa kila kukicha. Nini siri ya mafanikio ya utendaji wako yaliyofanya ustaafu kwa heshima pasipo kashfa yoyote?

Dk. Kilahama: Unajua mimi nimeanza kazi mwaka 1977 na wakati ule, mtu aliyeitwa Bwana Miti hakuwa na shida ya utajiri zaidi ya kufanya kazi yake tu. Sasa hivi naweza kusema kwa dhati kabisa kwamba pepo mbaya ameingia kwenye utendaji wetu.

Pesa zimeanza kuwa tamu sana. Watu wako tayari kufanya chochote kile ili mradi wapate pesa. Wanataka majumba ya kifahari, wanataka magari ya kifahari na vitu vingine chungu nzima. Na unajua sasa mahitaji ya malighafi za misitu yamekuwa makubwa sana kwa vile dunia imekuwa kama kijiji.

Kwa sababu usafiri umeboreka, maana yake ni kwamba mtu wa arabuni anaweza kutumia mkaa wa Mtwara. Mtu wa China anaweza kutumia pembe za ndovu wa Katavi. Kwa hiyo changamoto ni kubwa sana.

Unaweza ukawa umekaa ofisini mara ukakuta mtu anakuletea samaki na anakwambia “ Mzee chakula cha watoto hicho.” Sasa mimi nilikuwa nauliza chakula cha watoto wa wapi hao? Nimekwambia kuna shida ya chakula nyumbani kwangu?

Nakumbuka sana Desemba mwaka 2007, nikiwa nkatika mji wa Bali, Indonesia, nilipata taarifa za kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki. Nikapata emails nyingi sana za pongezi.

Watu wengine sikujua hata email yangu wameipata wapi.

Niliporudi ofisini Dar, nikaona watu wamenibadilikia ghafla. Kila mtu anataka kunikumbatia na kunipongeza. Wananitazama kwa kutabasamu. Nikajiuliza, mbona haikuwa hivi kabla sijapewa huu ukurugenz? Mbona hizi bashasha sikuziona wakati ule?

Sasa wakati sikukuu ya Krismasi ikikaribia, zawadi zikaanza kumiminika ofisini kwangu. Watu wengine wakagoma kuziacha ofisini kwa madai kwamba wanataka kunipa mimi mwenyewe mkononi.

Sasa siku moja sekretari wangu akaniambia mzee kuna mgeni hapo nje anasema ana zawadi yako. Nikasema hawezi kuiacha hapo kwako? Akasema hapana anataka kukupa mwenyewe. Nikamwambia haya mwite na wewe uingie.

Basi wote wakawa ndani. Akanipa hiyo zawadi. Na hapohapo nikamwambia sekretari wangu aifungue. Nikamshukuru Yule bwana. Nikamwambia sekretari kwamba kuanzia siku hiyo, watu wote wanaoleta zawadi azichukue na zichukuliwe kwamba ni za idara na si zangu.

Maana kama zingekuwa zangu, mbona mwaka jana hawakunipa? Mbona mwaka juzi hawakunipa? Zawadi gani hizi zimeanza wakati nilipochaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara.

Mwaka uliofuata (2008), wakaleta tena zawadi lakini zilikuwa kidogo. Na zote nikawa nagawa idarani. Kuanzia hapo hadi nastaafu mwaka jana, hawakuleta tena zawadi zao.

Nakumbuka siku moja nilikuwa kwenye stendi ya daladala ya Ubungo pale. Kumbe kuna watu wakawa wameniona. Basi naenda ofisini kesho yake, kuna watu wakanifuata na kuniambia –mzee kwa heshima yako wewe si mtu wa kupanda daladala. Tunaomba tukununulie gari ili angalau urahisishe mambo ya usafiri.

Mimi nikawaambia mimi nina gari nimepewa na serikali. Nimepewa pia dereva wa kuniendesha. Ila Jumapili ni siku ya mapumziko na siwezi kumtumikisha dereva ili mradi watu wanione nina gari.

Na nikawaambia wasisumbuke kwa sababu mimi sikuzaliwa na gari. Magari nimeyakuta tu na niwe na gari au nisiwe na gari bado nitapanda daladala kama kawaida.

Kama ni mjinga unaweza ukasema du hawa jamaa wananipenda kwelikweli au siwezi kuacha gari la bure. Lakini kwa wenzako, hiyo ni opportunity to hook you (fursa ya kukunasa).

Ni kweli kwamba wizara ile ina majaribu mengi lakini la msingi ni kwako ku declare interests mapema. Kama hupendi rushwa, onyesha mapema sana na watu wakikuelewa hawatakufuata tena.

Raia Mwema: Umefanya kazi katika misitu ya Tanzania kwa zaidi ya miaka 30 kabla hujastaafu. Unadhani kuna changamoto zipi kubwa ambazo zinaikabili misitu yetu kwa sasa?

Dk.Kilahama: Changamoto kubwa kuliko zote ni umasikini walionao wananchi wetu. Kadri umasikini wa wananchi wetu unavyokithiri, ndiyo wananchi wanazidi kutegemea misitu kuendesha maisha yao.

Wakati mahindi yanaposhindwa kuota, watu wanakimbilia misituni. Kuna watu wanatoa hoja kwamba zipo jamii zinazotegemea mifugo, hii si kweli. Hata mifugo yenyewe inapelekwa misituni kulishwa.

Watu wakitaka kuni na mkaa wanakwenda msituni. Wakitaka madawa wanakwenda msituni. Wakitaka chakula wanakwenda msituni. Na kadri mtu anavyozidi kuwa masikini, utegemezi wake kwa mazingira yanayomzunguka unazidi.

Changamoto nyingine ni elimu ndogo waliyonayo wananchi kuhusu uhifadhi wa mazingira. Utakuta mtu anahitaji eneo dogo kwa ajili ya kilimo lakini anachoma moto msitu mzima. Au mtu ana shida ya vipande vya kuni lakini anakata miti na miti.

Jingine ni ukuaji wa watu. Idadi ya watu inavyozidi kuongezeka, mazingira yanaathirika kwa sababu yenyewe yako kama yalivyo. Hayaongezeki. Hivyo ongezeko kubwa la watu ni hatari sana kwa miti na mazingira kwa ujumla.

Nne ni ukosefu wa nishati mbadala kwa wananchi. Kwa sasa wananchi wengi wanategemea mazao ya msituni kama chanzo kikuu cha nishati. Hili lisipobadilika, hali itazidi kuwa mbaya.

Raia Mwema: Kutokana na unayoyafahamu, ni misitu ya mikoa gani ina hali mbaya zaidi kwa sasa hapa nchini na ya wapi walau ina nafuu?

Dk. Kilahama: Kwa ujumla hali ni mbaya kwa kweli. Nikisema hapa kuna maeneo yana hali nzuri haitamaanisha kwamba sasa watu ndiyo waende kuvamia. Hata hivyo, maeneo ambako hali ni nzuri, utakuta kuna jitihada za wananchi wenyewe kuilinda.

Kuna kitu tulikianzisha kinaitwa Usimamizi Shirikishi wa Misitu (USM), ambako wananchi, serikali na sekta binafsi wanashirikiana kuhakikisha misitu na mazao yanalindwa na wakati wa kuvuna, uvunaji unakuwa endelevu.

Mikoa ambayo ina hali nzuri kwa sasa ni ile iliyo katika tao la Mashariki. Misitu kama ile ya Nilo kule Korogwe. Kilombero mkoani Morogoro na Minziro kule Kagera iko vizuri.

Hata katika mikoa ya Kusini kama vile Lindi na Rukwa, hali si mbaya sana haswa baada ya wananchi kuwezeshwa kupitia USM na wanafanya makubwa sana, haswahaswa, Lindi, kulinda rasilimali zao.

Misitu iliyo katika hali mbaya hapa nchini ni ile iliyo katika mikoa ya Singida na Shinyanga. Same mkoani Kilimanjaro na ile ya Kisongo kule Arusha. Misitu ya mkoa wa Tabora nayo inaanza kuathirika na tatizo kubwa linatokana na ufugaji mbovu.

Unajua wapo watu ambao hadi leo wanaamini katika ufugaji wa mifugo mingi. Wenzetu wamehamia kwenye ufugaji wa mifugo michache lakini yenye tija na faida kubwa. Sisi mtu anakuwa na ng’ombe wengi lakini wanaishia kuharibu mazingira na kumtia mfugaji na taifa kwa ujumla hasara.

Raia Mwema: Umeondoka idara ya nyuki katika kipindi ambacho kumekuwapo na mwamko mkubwa katika ufugaji wa wadudu hao. Watu wanachofahamu zaidi kuhusu nyuki ni kwamba ni wadudu wakali na wanaong’ata. Ni namna gani mtu anafuga nyuki, wanyama ambao hawawezi kumfahamu hata mtu anayewafuga?

Dk. Kilahama: Kwanza si nyuki wote ambao wanauma. Kuna nyuki hawaumi kabisa watu. Pili ni muhimu pia kufahamu kwamba nyuki anayekuuma maana yake naye anakufa. Ile sindano anayokuchoma nayo ndiyo uhai wake.

Labda wanajua kwamba akikuuma anakufa. Labda hawajui. Lakini wakikuuma wanakufa. Na kwa kawaida nyuki haumi mtu bila ya kuchokozwa. Kama hujawachokoza au kuingilia kwenye mambo yao, nyuki hawawezi kukung’ata.

Kufuga nyuki ni muhimu kwa sababu soko la asali kwa sasa ni kubwa sana. Watu wamefahamu faida za asali na bidhaa hiyo imekuwa na faida kubwa sana. Hawana gharama ya kuwatunza na ukishakuwa na mizinga yako na eneo zuri, una uhakika wa faida.

Kwa bahati nzuri, kwa wale waoga wa kung’atwa, siku hizi kuna nguo na vifaa maalumu vya kuzuia using’atwe na nyuki. Ukivaa hata waje 200 kukung’ata wataishia kwenye nguo tu na hutahudhurika.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amefanya makubwa sana kwenye kuboresha mazingira ya biashara ya asali na ufugaji nyuki. Nafikiri huu ni wakati mzuri sana wa kufanya biashara hiyo.

Raia Mwema: Kuna tatizo la watu kuambiwa hii ni asali ya nyuki wadogo wakati ni ya nyuki wakubwa au asali zilizochakachuliwa. Mtu anafahamu vipi kwamba amenunua asali iliyo bora?

Dk.Kilahama: Asali ya nyuki wadogo ni nzuri kuliko ile ya nyuki wakubwa. Hii ni kwa sababu nyuki wadogo wanatembea zaidi kuliko wale wakubwa. Kutembea zaidi maana yake wanakwenda kwenye maua mengi zaidi kutafuta malighafi za nyuki.

Asali iliyotengenezwa kutokana na maua mengi zaidi ndiyo asali nzuri zaidi. Kwa kawaida, asali bora inakuwa na rangi nyeusi. Asali inavyozidi kuwa nyeusi, ndiyo inazidi kuwa bora. Ukiona asali si nyeusi ujue ubora umepungua pia.

Raia Mwema: Tumeongea mambo mengi ya kitaaluma. Hebu kidogo tuambie wakati ulipokuwa mwanafunzi au kijana mdogo ulikuwa mtu wa namna gani.

DK. Kilahama: Kusema ukweli mimi nilikuwa mwanafunzi mwenye heshima na nidhamu ya hali ya juu. Enzi zile, mwalimu alikuwa anaweza kumtuma mwanafunzi kumsaidia baadhi ya kazi zake na kwa kweli mimi nilikuwa nasaidia sana.

Nimefua, kuchota maji na kufanya usafi kwenye shule za walimu wangu. Kuna wakati ikifika wikiendi, walimu walikuwa wakishindana kuwa na mimi kwenye nyumba zao kwa vile nilikuwa na tabia nzuri.

Kuna mwalimu mmoja, nakumbuka alikuwa anaitwa Dina Nkongo, mwanamke huyu, yeye alikuwa ananituma kwenda kumnunulia hadi vitenge vyake vya kuvaa sokoni.

Kutoka shuleni ilikuwa umbali wa kama maili tano hivi. Kwa hiyo maili kumi ukijumlisha kwenda na kurudi lakini mimi nilikuwa nakwenda na kurudi bila ya sababu.

Pia, nilikuwa mwanafunzi mwenye uwezo mkubwa kitaaluma. Katika shule ya Biirabo kule Muleba mkoani Kagera ambako nilisoma, siku zote nilikuwa sehemu ya wanafunzi sita bora.

Nakumbuka wanafunzi ambao tulikuwa tukishindana nao mara kwa mara ni Nicodem Tibanyendera aliyekuja kuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Dk. Suleiman aliyekuja kuwa daktari pale Lugalo.

Kuna mwanafunzi mmoja ambaye siku zote alikuwa wa kwanza darasani kwetu lakini nimemsahau jina lake. Huyo bwana sikumbuki kama aliwahi kuwa hata wa pili. Ila mimi na hao wenzangu tulikuwa tunabadilishana tu namba.

Cha ajabu, katika mtihani wa kutoka Shule ya Kati (Middle School) kwenda Sekondari, katika shule yetu iliyokuwa na wanafunzi 196, wakafaulu watu 12 na jina langu halikuwepo.

Watu wa kwanza kusikitika wakawa walimu. Wakawashawishi wazazi wangu nirudie darasa. Nikarudia na nikawa miongoni mwa wanafunzi bora. Lakini ulipofika mtihani wa mwisho, sikuchaguliwa tena.

Walimu hao hao wakaniomba nikarudie katika shule nyingine iliyoitwa Nyakagoyagoye iliyopo wilayani Karagwe. Huko ndiyo hatimaye nikafaulu na kupata nafasi kwenda sekondari ya Kibaha mkoani Pwani.

Nilikuwa kiongozi wa Umoja wa Wanafunzi wa Kikristo (UKWATA) wakati nikiwa shuleni Tosamaganga katika ngazi ya mkoa na kitaifa. Utaona kwamba kwa kweli nilikuwa na maisha ya kimaadili.

Kuna wakati baadhi ya watu walihofu kwamba nitafeli masomo kutokana na kujihusisha sana na dini. Hata hivyo, Mungu alikuwa mkubwa na nikawa nafaulu tu.

No comments:

 
 
Blogger Templates